• HABARI MPYA

    Tuesday, December 10, 2013

    STARS DHIDI YA KENYA ‘INAYOBEBWA VIBAYA’ NA MAREFA CHALLENGE 2013, PATACHIMBIKA MACHAKOS LEO

    Na Mahmoud Zubeiry, Machakos
    TANZANIA Bara ‘Kilimanjaro Stars’, leo inashuka dimbani kwenye Uwanja wa Kenyatta, Machakos, kumenyana na wenyeji, Kenya ‘Harambee Stars’ katika Nusu Fainali ya Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati, CECAFA Challenge kuanzia saa 7:00 mchana.
    Hii ni mara ya pili mfululizo kwa Stars chini ya kocha Mdenmark, Kim Poulsen kufika Nusu Fainali ya michuano hiyo, baada ya mwaka jana pia mjini Kampala, Uganda ambako ilitolewa na wenyeji, Uganda ‘The Cranes’ kwa kufungwa mabao 3-0.
    Lakini Kim, amelipa kisasi kwa The Cranes, baada ya Stars kuivua ubingwa Uganda Jumamosi kwa kuitoa kwenye Robo Fainali, Uwanja wa County ya Mombasa, zamani Manispaa kwa penalti 3-2, kufuatia sare ya 2-2 ndani ya dakika 90. 

    Mungu Ibariki Tanzania: Kikosi cha Stars Challenge 2013 na chini ni Harambee....na "Washindwe".

    REKODI YA BARA NA KENYA CHELLENGE TANGU 1973…

    Septemba 27, 1973
    Tanzania 2-1  Kenya (Kundi B)
    Septemba 25, 1974
    Tanzania 0- 0  Kenya (Kundi A)
    Novemba 7, 1975
    Kenya 3- 2 Tanzania (Nusu Fainali)
    Novemba 6, 1976
    Kenya 1-1 Tanzania (Kundi B)
    Novemba 3, 1979
    Kenya 0-0 Tanzania (Kundi A)
    Novemba 20, 1981
    Tanzania 1-0 Kenya (Kundi A)
    Novemba 28, 1981
    Kenya 1- 0 Tanzania (Fainali)
    Novemba 18, 1983
    Kenya 0-0 Tanzania (Kundi A)
    Oktoba 8, 1985
    Kenya 3-2 Tanzania (Kundi A)
    Desembar 16, 1987
    Kenya 3- 2 Tanzania (Kundi A)
    Novemba 10, 1988
    Kenya 0-0 Tanzania (Kundi A)
    Deaemba 5, 1989
    Kenya A 2-1 Tanzania (Kundi A)
    Novemba 22, 1992
    Tanzania (Kakakuona) 0-0 Kenya (Kundi A)
    Desemba 1, 1994
    Kenya A 0-1 Tanzania (Kundi A)
    Novemba 30, 2002
    Tanzania 1-0  Kenya (Kundi A)
    Desemba 14, 2002
    Tanzania 2-3 Kenya (Fainali)
    Desemba 8, 2007
    Tanzania 2-1  Kenya (Kundi A)
    Januari 11, 2009
    Kenya 2-1 Tanzania (Nusu Fainali)
    Desemba 10, 2013 
    Tanzania Vs Kenya; Nusu Fainali
    Baada ya kumaliza shughuli hiyo pevu, Kim anakabiliwa na jukumu lingine zito mbele yake, ambalo ni Nusu Fainali dhidi ya Kenya, ambayo imeonekana ‘kubebwa’ mno na marefa hadi sasa katika mashindano haya.
    Kenya imekuwa ikipewa penalti katika mechi zote kuanzia hatua ya makundi hadi Robo Fainali na hali hiyo inatarajiwa kwa kiasi kikubwa kuendelea na leo pia Machakos.
    Beki wa Azam FC, Joackins Atudo amepiga penalti nne na kufunga tatu hadi sasa, wakati moja alikosa katika mechi ya Kundi A dhidi ya Sudan Kusini.
    Habari njema ni kwamba, kipa wa Stars, Ivo Mapunda anaheshimika mno kwa uhodari wa kucheza penalti, lakini pia Wakenya wanamuamini mno Atudo katika upigaji.
    Mechi hiyo imeteka hisia za wengi na sababu za Shirikisho la Soka Kenya (FKF) kuipeleka Uwanja wa Kenyatta badala ya Nyayo, Nairobi ni kutokana na imani kwamba watu wa huko huishagilia mno Harambee Stars inapocheza.  
    Wakati Stars iliitoa Uganda, Kenya waliingia Nusu Fainali baada ya kuifunga 1-0 Rwanda ‘Amavubi’ kwa bao la penalti iliyotolewa katika mazingira ya utata iliyopigwa na Atudo kama kawaida.
    Kenya ina ukuta imara, safu nzuri ya kiungo, lakini haina makali sana katika safu yake ya ushambuliaji, wakati Tanzania Bara japokuwa itamkosa kiungo wake, Salum Abubakar ‘Sure Boy’ aliyeonyeshwa kadi nyekundu dhidi ya Uganda, bado ina viungo wengine bora wa kuziba pengo hilo.
    Kuna chipukizi Hassan Dilunga wa Ruvu Shooting na mkongwe Athumani Iddi ‘Chuji’ wa Yanga, ambao yeyote kati yao Kim anaweza kumpa jukumu la kuziba pengo la kiungo wa Azam FC, Sure Boy.
    Stars ina ukuta imara kama ilivyo kwa safu ya kiungo na utamu zaidi ni safu yake ya ushambuliaji inayoundwa na wakali wawili wa TP Mazembe ya DRC, Mbwana Ally Samatta na Thomas Emmanuel Ulimwengu kwa pamoja na Mrisho Khalfan Ngassa wa Yanga.    
    Jianguasheni huko tupewe penalti; Tegemeo la mikwaju ya penalti la Harambee, Joackins Atudo, leo atapiga?

    Iwapo hali ya Ngassa haitakuwa imeimarika, hakuna shaka ‘viberenge’ vya Simba SC, Haroun Chanongo na Ramadhani Singano ‘Messi’ mmoja wao anaweza kuchukua nafasi na akafanya kazi nzuri- lakini pia kuna makinda mengine mawili ya Azam FC, Joseph Kimwaga na Farid Mussa pia wanaweza kucheza nafasi hiyo.
    Litakuwa pengo kumkosa Ngassa kutokana na uzoefu wake ambao tayari anao hivi sasa kisoka, lakini pia itakuwa nafasi nzuri kwa chipukizi hao kuupambanua uwezo wao, iwapo watapewa nafasi.
    Ataziba pengo la Sure Boy; Athumani Iddi 'Chuji' alicheza vizuri alipoingia dhidi ya Uganda na akafunga penalti
    Nyama; Thomas Ulimwengu alimaliza mechi na Uganda akiwa analalamika maumivu ya nyama
    Himid Mao amemaliza adhabu ya kadi na baada ya kuwa nje ya Uwanja katika mechi dhidi ya Uganda, leo anarudi kwenye mashindano na litakuwa jukumu la Kim kumchezesha kiraka huyo wa Azam, au kumpanga tena Michael Aidan wa Ruvu Shooting. Nusu Fainali nyingine ni kati ya Zambia na Sudan mjini Mombasa. Kila la heri Tanzania Bara ‘Kilimanjaro Stars’. 
    Askari wa JK; Wachezaji wa Stars wako tayari kwa kuitoa Kenya leo
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: STARS DHIDI YA KENYA ‘INAYOBEBWA VIBAYA’ NA MAREFA CHALLENGE 2013, PATACHIMBIKA MACHAKOS LEO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top