• HABARI MPYA

  Jumatatu, Desemba 23, 2013

  DONALD MOSOTI OMWANWA NI SULUHISHO LA UKUTA WA SIMBA SC?

  Mahmoud Zubeiry, Dar es Salaam
  KWA muda mrefu Simba SC imekuwa ikihangaikia mabeki wa kati na imekuwa ikisajili wachezaji wengi wa nafasi hiyo na kuwaacha baada ya kuona hawafai.
  Msimu uliopita pekee walisajiliwa Paschal Ochieng kutoka Kenya na Komabil Keita kutoka Mali, lakini wote wakaonekana hawafai.
  Simba SC imekuwa ikisajili hadi mabeki wazawa kama Obadia Mungusa ‘Terminator’ lakini hakuonekana anafaa pia akatemwa.
  Beki Adui; Donald Mosoti Omwanwa akienda chini kuokoa mpira dhidi ya Mrisho Ngassa wa Yanga SC juzi, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

  Msimu huu, Simba SC ilileta mabeki wawili kutoka Uganda, Samuel Senkoom na Assumani Buyinzi, lakini wote pia wakaonekana wa ‘kazi gani’.
  Baadaye Simba SC ikasajili mabeki wawili, Joseph Owino kutoka Uganda aliyewahi kuitumikia timu hiyo hapo awali na Gilbert Kaze kutoka Burundi.
  Hawa walicheza pamoja katika beki ya kati mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu msimu huu, lakini hawakuonekana kuwavutia sana mabosi wa Wekundu hao wa Msimbazi na Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba SC, Zacharia Hans Poppe akabomoa benki mwezi juu kusajili beki mwingine.
  Omwanwa na Ngassa ilikuwa shughuli oevu juzi
  Cheki kazi hiyo
  Hii inaitwa ng'ado kwa ng'ado

  Huyo ni Donald Mosoti Omwanwa kutoka Gor Mahia ya Kenya aliyetua Msimbazi pamoja na kipa Ivo Mapunda kutoka klabu hiyo ya Nairobi.
  Wawili hao ni pendekezo la kocha mpya wa Simba, Mcroatia Zdravko Lugarusic aliyetokea Gor pia na kwa mara ya kwanza waliichezea Simba SC juzi katika mechi ya Nani Mtani Jembe.
  Baada ya dakika 90 Simba SC ikishinda 3-1 dhidi ya Yanga yenye washambuliaji wakali na hatari kama Emmanuel Okwi aliyefunga bao pekee la wana Jangwani hao, Mrisho Ngassa, Didier Kavumbangu na Hamisi Kiiza mashabiki wa timu hiyo waliipenda kazi ya Omwanwa.
  Wanaamini wamepata suluhisho la kudumu la tatizo la safu yao ya ulinzi mbele ya Mkenya huyo maarufu kama ‘Beki Adui’ nchini Kenya kutokana uchezaji wake wa ‘kiroho mbaya’.
  Na kweli, Omwanwa alicheza kwa uelewano mkubwa na Owino na kwa urefu wake alikuwa akiicheza mipira yote mirefu langoni mwake na mingine akimuachia Ivo, ambaye tayari amekwishacheza naye Kenya.  
  Beki la kazi; Huyu ndiye Donald Mosoti Omwanwa, Kenya wanamuita Beki Adua

  Aliwadhibiti vizuri washambuliaji wote wa Yanga akina Kavumbangu, Ngassa na Kiiza na hakika hawakuweza kufurukuta na kwa sababu hiyo tayari Omwanwa ameingia kwenye ‘mioyo’ ya mashabiki wa Simba SC.
  Lakini hiyo ilikuwa mechi moja tu beki huyo anacheza na watu watahitaji mechi zaidi kumuona ili kujiridhisha kama kweli suluhisho la tatizo la safu ya ulinzi ya Simba SC imepatikana.  Je, Omwanwa amekuja kumaliza tatizo la muda mrefu Simba SC? Bila shaka hilo ni jambo la kusubiri na kuona.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: DONALD MOSOTI OMWANWA NI SULUHISHO LA UKUTA WA SIMBA SC? Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top