• HABARI MPYA

    Tuesday, December 10, 2013

    STARS YAFA KIUME CHALLENGE

    Na Mahmoud Zubeiry, Nairobi
    TANZANIA Bara ‘Kilimanjaro Stars’, imefungwa 1-0 na Kenya ‘Harambee Stars’ katika Nusu Fainali ya Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati, CECAFA Challenge Uwanja wa Nyayo, Nairobi, usiku huu ikisindikizwa na mvua.
    Kwa matokeo hayo, sasa Stars itamenyana na Zambia katika mechi ya kusaka mshindi wa tatu keshokutwa mchana Uwanja wa Nyayo tena, wakati Kenya itamenyana na Sudan katika Fainali jioni yake.
    Mshambuliaji wa Tanzania Bara, Mbwana Samatta akiwatoka mabeki wa Kenya, Joackins Atudo kulia na Aboud Omar kushoto Nyayo usiku huu

    Katika mchezo huo, uliochezeshwa na refa Thiery Nkurunziza wa Burundi, aliyesaidiwa na Idam Hamid wa Sudan na Mussie Kinde wa Ethiopia, hadi mapumziko, tayari wenyeji walikuwa mbele kwa bao hilo 1-0, lililowekwa kimiani na mshambuliaji wa Thika United, Clifton Miheso dakika ya nne kwa shuti la umbali wa mita 20, baada ya kupokea pasi fupi ya Alan Wanga na kumchungulia kipa Ivo Mapunda.
    Baada ya bao hilo, Stars walizinduka na kuanza kushambulia, lakini ukuta wa Kenya ulikuwa imara kuzuia mashambulizi yote. 
    Mbwana Samatta akipambana na mabeki wa Kenya
    Kikosi cha Stars leo
    Kikosi cha Harambee leo
    Kiungo wa Stars aliyekuwa nje leo kwa sababu ya kadi nyekundu, Salum Abubakar 'Sure Boy' kushoto akitazama mechi
    Farid Mussa akipambana na Clifton Miheso wa Kenya, huku Michael Pius akiwa tayari kutoa msaada 

    Nafasi pekee nzuri ambayo Stars waliipata ilikuwa dakika ya 44, wakati kona nzuri ya Mrisho Ngassa ilipopanguliwa na kipa Duncan Ochieng, lakini Mbwana Samatta akachelewa kuunganisha, Joackins Atudo akaondosha kwenye hatari. 
    Kipindi cha pili Stars ilicheza vizuri zaidi, lakini bado ukuta wa Harambee ulikuwa mgumu na nafasi pekee nzuri katika kipindi hicho ilikuwa dakika ya 88, wakati Mbwana Samatta alipomtoka beki wa Kenya na kuingia vizuri ndani ya 18, lakini akapiga juu.
    Baada ya mchezo huo, wachezaji wa Stars walikuwa wakilia na ikabidi viongozi wachukue jukumu la kuwabembeleza. Nahodha Kevin Yondan ndiye alikuwa ana hali mbaya zaidi. 
    Kikosi cha Stars leo kilikuwa; Ivo Mapunda, Michael Pius, Erasto Nyoni, Said Morad, Kevin Yondan, Frank Domayo, Mrisho Ngassa, Hassan Dilunga/Athumani Iddi ‘Chuji’ dk65, Thomas Ulimwengu, Mbwana Samatta na Amri Kiemba/Farid Mussa dk65.
    Kenya; Duncan Ochieng, Allan Wanga/Noa Wafula dk81, James Situma, Aboud Omar, Joackins Atudo, Peter Opiyo, Francis Kahata, Anthony Akumu, Clifton Miheso/Paul kiongera dk88, David Ochieng Owino na Edwin Lavatsa.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: STARS YAFA KIUME CHALLENGE Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top