• HABARI MPYA

  Jumapili, Desemba 15, 2013

  KAMA ULIKUWA HUJUI, HIYO NDIYO YANGA BWANA!

  SIKU kadhaa baada ya klabu ya Yanga ya Dar es Salaam kutoa ripoti yake ya mapato na matumizi kwa kipindi cha miezi sita tangu Januari 14, 2013 hadi Julai 14, 2013 na kuonyesha kwamba bado haijimudu, ikiwa inajiendesha kwa kutegema wafadhili na wadhamini, Mwenyekiti na Mfadhili Mkuu wa klabu hiyo, Yussuf Mehboob Manji anaibuka na kusema hatagombea tena atakapomaliza muda wake Julai mwakani.
  Manji hajataja sababu za kuamua kutoendelea kuongoza Yanga atakapomaliza muda wake, zaidi amesema uamuzi huo ni hiari yake na hakuna shinikizo.

  Manji ameifanyia mengi Yanga tangu alipojitokeza mwaka 2006 na sasa watu wamesahau shida na dhiki za klabu hiyo- mashabiki na wanachama wa klabu hiyo wanatembea kifua mbele siku hizi, wakiamini klabu yao ni tajiri.
  Wanaona klabu yao tajiri kwa sababu wachezaji wanapandishwa ndege kwenda na kurudi kuweka kambi Pemba katika hoteli ya nyota tano kujiandaa na mapambano ya watani, Simba SC.
  Wanaona klabu tajiri, kwa sababu wanasajiliwa wachezaji wa ndani wa nje kwa mamilioni ya fedha- na kwa ujumla klabu haina matatizo na kwa michuano ya nyumbani na ukanda wa Afrika Mashariki na Kati inafanya vizuri.
  Lakini sasa wakati Manji anasema anataka kuondoka- bila shaka vichwa vimeanza kuwauma, kwa sababu huyo ndiye anayetoa fedha zake kwa gharama zote hizo.
  Wadhamini wa klabu, Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) wanatoa fungu la wastani wa Sh. Milioni 30. 25 kwa mwezi, ambalo halitoshelezi hata kwa mishahara ya wachezaji wote. Hiyo inaweza kuwa ni nusu tu ya mshahara wa mtaalamu mmoja wa benchi la Ufundi, Kocha Mkuu, Mholanzi, Ernie Brandts.
  TBL wanaoidhamini Yanga kupitia bia ya Kilimanjaro kwa pamoja na mahasimu wao wa jadi, Simba SC hawatoi fedha za timu kusajili. Hawatoi tiketi za ndege timu kwenda Pemba kuweka kambi. Hawatoi gharama za kambi katika hoteli za nyota tano.
  Hawatoi bonasi ya Sh. Milioni 100 kwa wachezaji wakiwafunga wapinzani wao wa jadi, Simba SC. Sasa na haya ndiyo mambo ambayo yanawafanya Yanga watembee vifua mbele kwa sasa ambayo yote yanafanywa na Manji.
  Kweli, Manji kaahidi kujenga Uwanja wa kisasa na inaonekana kama ameshindwa- lakini bado umuhimu wake ni mkubwa mno katika timu hiyo, kama ilivyo kwa Kapteni wa zamani wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), Zacharia Hans Poppe anavyoibeba Simba SC.
  Wazi sasa, kama yupo mwanachama au mpenzi wa Yanga alikuwa ana kiherehere cha kutaka kuhoji juu ya ahadi ya Manji ya Uwanja wa kisasa, sasa hataweza kufanya hivyo na badala yake anafikiria hali itakavyokuwa baada ya mfanyabiashara huyo kung’atuka.
  Je, klabu itarudi kule kule kwenye kutembeza bakuli jukwaani kuchangisha fedha za kusaidia wachezaji? Wachezaji watarudia kuwekwa kambini ‘gesti bubu’ kujiandaa na mechi za michuano ya Afrika.
  Ndivyo ilivyokuwa, Yanga chini ya Nahodha Ally Mayay Tembele ‘Meja’ walitokea gesti moja Ubungo kwenda kucheza na Kwara United ya Nigeria Kombe la Shirikisho mwaka 1999, wakafungwa 3-0, wakati mchezo wa kwanza ugenini walifungwa 1-0 tu.
  Unajua kwa nini? Walipokuwa Kwara wenyeji waliwaweka katika hoteli nzuri, walilala vizuri, wakala vizuri wakaingia uwanjani wakacheza mpira mkubwa sana na wakafungwa 1-0 tena kwa mbinde. 
  Lakini kwa sababu ya malazi mabovu, lishe ya ovyo na mazingira mabovu kwa ujumla ya maandalizi wakiwa nyumbani- wakafungwa 3-0. Sasa tafakari, Manji akiondoka hali itakuwaje Yanga na kwa nini tusikae tayari kumsikia Mzee Akilimali Yahya na wazee wenzake wanakwenda kumpigia magoti Manji kumuomba asiondoke. Hiyo ndiyo Yanga bwana!
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: KAMA ULIKUWA HUJUI, HIYO NDIYO YANGA BWANA! Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top