• HABARI MPYA

  Jumanne, Desemba 31, 2013

  YANGA SC YASEMA ZFA INAWACHELEWESHA KWENDA ZANZIBAR KUSHIRIKI KOMBE LA MAPINDUZI

  Na Mahmoud Zubeiry, Dar es Salaam
  YANGA SC imesema haijapata barua ya mwongozo kuhusu Kombe la Mapinduzi kutoka kwa Chama cha Soka Zanzibar (ZFA) na ndiyo maana hadi sasa wanshindwa kupanga safari ya kwenda huko.
  Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano ya Yanga SC, Mussa Katabaro ameiambia BIN ZUBEIRY jana kwamba, waliwaandikia barua ZFA juu ya hilo, lakini hadi sasa hawajapata majibu.
  Hatumuogopi mtu; Mussa Katabaro aliyekumbatiana na Hamsi Kiiza amesema ZFA inawachelewesha kwenda Zanzibar  kwenye Kombe la Mapinduzi

  “Tunashindwa kwenda kwa sababu hatujatumiwa tiketi, hatujui tukienda tutapokewa na nani, tutafikia wapi, tumeandaliwa utaratibu gani, kufanya mazoezi, kula na nini. Haya ni mambo ambayo lazima tuyajue, hatuwezi kwenda tu,”alisema Katabaro.
  Kiongozi huyo amesema kamwe haiwezekani wao kugoma kwenda kushiriki mashindano hayo kwa sababu hakuna wanachohofia. 
  “Nasikia watu wanasemasema ooh Yanga hawapeleki timu Zanzibar, kwa nini, tuogope nini? Tumuogope nani? Naomba wana Yanga waachane na fikra hizo, sisi tutakwenda na tutafanya kitu ambacho wengi hawatarajii, wewe subiri,”alisema.
  Katabaro alisema huwezi kuitenganisha historia ya Yanga na Zanzibar, kwa sababu mwasisi wa Serikali huru ya Mapinduzi ya Zanzibar, hayati Abeid Amaan Karume alichangia sana ustawi wa klabu hiyo.
  “Na njia pekee na kubwa ya kumuenzi marehemu Karume ni kushiriki haya mashindano, hususan haya ya mwaka huu ambayo Wazanzibari wanasherehekea miaka ya 50 ya Mapinduzi,”alisema.
  Wakati huo huo: Wachezaji wawili Waganda wa Yanga SC, Emmanuel Arnold Okwi na Hamisi Friday Kiiza wanatarajiwa kuwasili leo Dar es Salaam kujiunga na wenzao kwa maandalizi ya safari ya Zanzibar.
  Ofisa Habari wa Yanga SC, Baraka Kizuguto alisema jana kwamba amezungumza na wachezaji hao na wamethibitisha kwamba wanakuja leo. 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: YANGA SC YASEMA ZFA INAWACHELEWESHA KWENDA ZANZIBAR KUSHIRIKI KOMBE LA MAPINDUZI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top