• HABARI MPYA

    Jumapili, Desemba 22, 2013

    IVO NA KASEJA, TUTAUONA MWISHO WAKE

    Na Mahmoud Zubeiry, Dar es Salaam
    KUNA kituko ambacho bila shaka wengi hawakukiona katika mchezo wa jana wa Nani Mtani Jembe baina ya Simba na Yanga Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
    Wakati wachezaji wa Simba SC iliyoshinda 3-1 wanakwenda kuwapa mikono wa Yanga, kabla ya mchezo kuanza, Juma Kaseja aliukwepa mkono wa Ivo Mapunda, tena akihama kabisa katika nafasi yake.
    Sababu nini? Bila kwenda mbali, ni uhasama ulioanzia wakati wa kocha Mbrazil, Marcio Maximo timu ya taifa, Taifa Stars mwaka 2006.
    Mahasimu; Ivo Mapunda na Juma Kaseja chini hawaivi chungu kimoja tangu mwaka 2006


    Wakati Maximo anakuja nchini, Juma Kaseja ndiye aliyekuwa kipa nambari moja, lakini akaamua kumpa nafasi hiyo Ivo, akisema kipa mwenye umbo dogo si bora zaidi ya mwenye umbo kubwa.
    Baada ya Taifa Stars kufungwa 4-0 na Senegal mjini Dakar mwaka 2007, Ivo akiwa langoni yakaibuka maneno eti Kaseja alimcheka mwenzake na Maximo akaamua kumtema moja kwa moja Juma katika timu yake.
    Wakati huo, Ivo anaingia timu ya taifa akitokea Yanga na Kaseja anadakia Simba SC. Kaseja aliendelea kufanya vizuri akiwa Simba SC wakati Ivo hakuweza kuibeba Taifa Stars kufanya vizuri.
    Ukafika wakati Maximo akaamua kuachana na Ivo na kusaka kipa mwingine, zoezi ambalo hakufanikiwa hadi anaondoka nchini, ingawa alimuita hadi Muharami Mohamed ‘Shilton’ kutoka Msumbiji alipokuwa anacheza. 
    Ivo akiokota tauli yake baada ya mechi jana akiiwezesha Simba kushinda 3-1 na chini akiugulia maumivu baada ya kuumizwa na wachezaji wa Yanga wakati akiokoa mpira wa kona


    Kaseja akasajiliwa Yanga mwaka 2009 kwa sharti la awe kipa namba moja na Ivo akauzwa St George ya Ethiopia. Maximo akaondoka na Jan Borge Poulsen akawa kocha mpya Stars mwaka 2010 na Mdenmark huyo akamrejesha Kaseja Stars.
    Kaseja alirejea na bahati akaiwezesha timu ya Bara, Kilimanjaro Stars kutwaa Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati, CECAFA Challenge baada ya miaka 16 katika michuano iliyofanyika Dar es Salaam 2010.
    Na tangu hapo, Kaseja ameendelea kuwa Tanzania One ingawa hakuisaidia timu hiyo kupata mafanikio zaidi hadi mwezi uliopita alipotemwa katika kikosi cha Bara kilichokwenda kucheza Challenge Kenya.
    Beki Mbuy Twite akimbembeleza Kaseja wakati analia baada ya kufungwa bao la tatu na chini mpira umetinga nyavuni mfungaji Awadh Juma anakimbia kushangilia


    Sababu kubwa ya Kaseja kutemwa na kocha Kim Poulsen, aliyerithi mikoba ya Mdenmark mwenzake, Jan Poulsen ni baada ya kuachwa katika kikosi cha klabu yake Simba SC na kukosa timu ya kuchezea mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu.
    Wakati huo huo, Ivo alipomaliza Mkataba wake Ethiopia alirejea nyumbani kuichezea kidogo African Lyon na baadaye akaenda Bandari ya Kenya, alikofanya vizuri hadi kusajiliwa Gor Mahia iliyomrejesha kwenye chati.
    Katika kusaka kipa mbadala, Kim alimuita Ivo kutoka Kenya baada ya kusikia sifa zake na akaenda kufanya vizuri kwenye michuano ya Challenge Kenya hadi amesajiliwa Simba SC na sasa ni kipa nambari moja wa timu hiyo ya Mtaa wa Msimbazi.
    Jana Ivo aliibuka shujaa dhidi ya Kaseja katika mchezo wa Nani Mtani Jembe na bila shaka huo ni mwanzo tu wa ushindani mpya wa makipa hao nguli katika soka ya Tanzania.
    Ivo alimyanyasa Kaseja mbele ya Maximo.  Ni kweli. Lakini Kaseja ndiye aliyefanya Ivo aondoke Yanga. Na sasa Ivo amemrithi Kaseja Simba na pia amempokonya namba timu ya taifa.
    Kaseja ana maisha mapya Yanga SC, lakini atalazimika kutetea nafasi yake timu ya taifa. Vita hii ya Ivo na Kaseja, tutauona mwisho wake. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 maoni:

    Item Reviewed: IVO NA KASEJA, TUTAUONA MWISHO WAKE Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top