• HABARI MPYA

  Ijumaa, Desemba 20, 2013

  OKWI: NIKIPANGWA KESHO NITACHEZA VIZURI NA KUFUNGA, NGASSA NA KIIZA WOTE NIMECHEZA NAO TIMU MOJA

  Na Mahmoud Zubeiry, Dar s Salaam
  MSHAMBULIAJI mpya wa Yanga SC, Emmanuel Arnold Okwi amesema japokuwa hajapata fursa ya kufanya mazoezi na timu yake mpya, lakini hana wasiwasi akipangwa Jumamosi katika mechi dhidi ya timu yake zamani, Simba SC atacheza kwa uelewano mzuri na wachezaji wenzake wapya, kwa kuwa yeye ni mchezaji wa kimataifa.
  Okwi aliyewasili jana Dar es Salaam akitokea kwao, kampala, Uganda kuja kuanza kuutumikia Mkataba wake wa miaka miwili, aliiambia BIN ZUBEIRY jana kwamba hana shaka akipangwa atacheza vizuri na kuwafurahisha mashabiki wa timu yake hiyo mpya kwa sababu ana uzoefu wa kimataifa.
  Okwi kushoto akiwa na Mussa Katabaro, Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Yanga

  “Kwanza mtu kama (Mrisho) Ngassa nimecheza naye Simba SC, na (Hamisi) Kiiza tunacheza naye timu ya taifa (Uganda), hakuna wasiwasi, mimi nikipangwa nao tutacheza kwa uelewano sana pale mbele  na nitafunga,”alisema Okwi.
  Lakini Okwi amesema kwa ujumla anaijua Yanga vizuri na anajua uchezaji wa wachezaji wake wengi, hivyo anaweza kucheza vizuri katika mfumo wa timu.
  “Unaweza kuitwa timu ya taifa, siku mbili kabla ya mechi na wakati mwingine unakuta wachezaji wengi hujawahi kucheza nao kabisa, lakini mnafanya mazoezi siku moja mnaelewana na mnacheza vizuri,”alisema Okwi.  
  Simba na Yanga zitamenyana Jumamosi katika mchezo wa Nani Mtani Jembe Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, unaoandaliwa na wadhamini wa klabu hizo, Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) kupitia bia ya Kilimanjaro Premium Lager.
  Katika mchezo huo, utakaochezeshwa na refa Ramadhan Ibada ‘Kibo’ kutoka Zanzibar, atakayesaidiwa na Ferdinand Chacha wa Bukoba na Simon Charles kutoka Dodoma, iwapo dakika 90 zitaisha kwa sare, sheria ya mikwaju ya penalti itatumika kuamua mshindi.
  Viingilio vya mechi hiyo ni Sh. 5,000 kwa viti vya rangi ya kijani, bluu Sh. 7,000, rangi ya chungwa Sh. 10,000, VIP C Sh. 15,000, VIP B Sh. 20,000 wakati VIP A Sh. 40,000 na tiketi za mchezo huo utakaoanza Saa 10:00 jioni zitaanza kuuzwa leo katika vituo mbalimbali.
  Vituo hivyo ni Shule ya Sekondari Benjamin Mkapa, Sokoni Kariakoo, mgahawa wa Steers ulioko mtaa wa Ohio/Samora, Oilcom Ubungo, Kituo cha Mafuta Buguruni, Dar Live Mbagala, Uwanja wa Uhuru, na BMM Salon iliyoko Sinza Madukani.
  Wachezaji wanaoruhusiwa kucheza mechi ya kesho ni wale waliosajiliwa ama kikosi cha kwanza au timu ya vijana pamoja na wapya ambao wameombewa usajili katika dirisha dogo.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: OKWI: NIKIPANGWA KESHO NITACHEZA VIZURI NA KUFUNGA, NGASSA NA KIIZA WOTE NIMECHEZA NAO TIMU MOJA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top