• HABARI MPYA

    Monday, December 16, 2013

    SIMBA NA YANGA ZAKABIDHIWA JEZI ZA MPAMBANO WAO JUMAMOSI TAIFA

    Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
    KAMPUNI ya Bia Tanzania (TBL) kupitia bia yake ya Kilimanjaro Premium Lager imekabidhi jezi kwa timu za Simba na Yanga kwa ajili ya mechi ya Nani Mtani Jembe itakayochezwa Jumamosi kuanzia saa kumi kamili jioni kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
    Kampeni ya Nani Mtani Jembe  iliyozinduliwa Oktoba 6 mwaka huu itamalizika Jumamosi kwa klabu za Simba na Yanga kuchuana vikali pamoja na kuwania Sh milioni 100 zilizotengwa na Kilimanjaro Premium Lager ambao ni wadhamini wakuu wa timu hizo.


    George Kavishe - Meneja wa Bia ya Kilimanjaro Premium Lager inayozidhamini Simba na Yanga akiwakabidhi Makamu Mwenyekiti wa Simba, Joseph Itangare na Msemaji wa Yanga, Baraka Kizuguto jezi maalum zitakazotumika kwenye mechi ya Nani Mtani Jembe itakayozikutanisha Simba na Yanga kwenye uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam Jumamosi tarehe 21 Desemba. (Picha: Executive Solutions)

    Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Meneja wa Kilimanjaro Premium Lager George Kavishe alisema wanakabidhi vifaa hivyo vyenye thamani ya Sh milioni 6.8 kwa ajili ya kuzipa mwonekano mpya timu hizo katika mechi hiyo.
    “Bado tunaendelea kuhesabu siku kuelekea siku ya mwisho ya kampeni yetu ya Nani Mtani Jembe Desemba 21 mwaka huu, Yanga ndio hadi sasa wanaongoza wakiwa na Sh Mil 91 na Simba wao wana Sh Mil 9,” alisema.
     Katika kampeni hiyo ya Mtani Jembe mteja atabandua ganda la kizibo cha bia ya Kilimanjaro Premium Lager ataona namba. Ataandika jina la timu yake (SIMBA au YANGA) ikifuatiwa na namba hiyo ya kwenye kizibo kasha atatuma kwenda namba 15440 na kuipa nafasi timu yake.
     Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa Simba Joseph Itang’are ‘Mzee Kinesi’ aliwashukuru wadhamini hao Bia ya Kilimanjaro kwa vifaa hivyo huku akitamba timu yake kuibuka na ushindi.
    Naye Ofisa Habari wa Yanga Baraka Kizuguto aliwashukuru wadhamini hao kwa kuwafanyia mambo mazuri na kuahidi kuendeleza mambo mazuri kwao na wataibuka na ushindi katika mechi hiyo.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: SIMBA NA YANGA ZAKABIDHIWA JEZI ZA MPAMBANO WAO JUMAMOSI TAIFA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top