• HABARI MPYA

  Jumatatu, Desemba 16, 2013

  SIMBA SC WAENDA KAMBINI ZANZIBAR

  Na Mahmoud Zubeiry, Temeke
  SIMBA SC inaondoka leo Dar es Salaam kwenda kisiwani Zanzibar kuweka kambi ya kujiandaa na mchezo maalum wa Nani Mtani Jembe, dhidi ya mahasimu wao wa jadi, Yanga SC Jumamosi ijayo Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
  Kocha mpya, Mcroatia Zdravko Logarusic ameamua kwedna kambini wachezaji wote kujiandaa na mchezo huo, wakati wachezaji wapya kutoka Gor Mahia ya Kenya, kipa Ivon Philip Mapunda na beki Donald Mosoti Omwanwa watajiunga na timu hiyo visiwani humo.
  Kocha machachari; Zdravko Logarusic amechukua wachezaji wote kambini Zanzibar

  Simba inakwenda kambini siku moja tu baada ya kuwaonyesha mashabiki wake ni tishio chini ya kocha mpya, Logarusic kufuatia kuifunga KMKM ya Zanzibar mabao 3-1 katika mchezo wa kirafiki jana hii Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
  Katika mchezo huo, hadi mapumziko, tayari Simba SC walikuwa mbele kwa mabao 2-0 yaliyofungwa na Said Ndemla dakika ya 11 na Edward Christopher dakika ya 16.
  Kipindi cha pili, KMKM walibadilika na kuanza kupeleka mashambulizi langoni mwa Simba SC wakionana kwa pasi nzuri, ingawa pia Wekundu wa Msimbazi nao waliendelea kushambulia.
  KMKM ilipata bao lake la kufutia machozi dakika ya 71, mfungaji Ally Ahmed ‘Shiboli’ kwa penalti, baada ya beki wa Simba kumchezea rafu mchezaji huyo. 
  Baada ya bao hilo, Simba SC ikiongozwa na Uhuru Suleiman katika safu ya ushambuliaji iliongeza kasi ya mashambulizi kusaka mabao zaidi.
  Juhudi hizo zilizaa matunda dakika ya 89, baada ya Henry Joseph kufunga kwa penalti kufuatia mchezaji mmoja wa Simba kuchezewa rafu kwenye eneo la hatari.
  Matokeo haya yanamanisha kocha mpya wa Simba SC, Mcroatia Zdravko Logarusic ameanza vyema kazi, hii ikiwa mechi yake ya kwanza tangu aanze kuifundisha timu hiyo.   
  Mchezo wa Nani Mtani Jembe, umeandaliwa na wadhamini wa timu hiyo, Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) kupitia bia ya Kilimanjaro, ambao pia ni wadhamini wa Yanga.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: SIMBA SC WAENDA KAMBINI ZANZIBAR Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top