• HABARI MPYA

    Saturday, December 28, 2013

    SIMBA SC KWENDA ZANZIBAR BILA LOGARUSIC, MATOLA AANZA KUSUKA KIKOSI CHA UBINGWA MAPINDUZI

    Na Mahmoud Zubeiry, Dar es Salaam
    KOCHA Mkuu wa Simba Mcroatia, Zdravko Logarusic ataungana na timu visiwani Zanzibar Januari 2, mwakani atakaporejea kutoka likizo ya mapumziko ya mwaka mpya, imeelezwa.
    Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Simba SC, Swedi Nkwabi ameiambia BIN ZUBEIRY leo kwamba wakati kocha huyo akiwa bado likizo, tayari kikosi kimeanza mazoezi tangu jana kwenye Uwanja wa Kinesi, Urafiki, Dar es Salaam chini ya kocha Msaidizi, Suleiman Matola.
    Logarusic kulia akiwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba SC, Zacharia Hans Poppe kushoto na Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya TFF, Geoffrey Nyange 'Kaburu'

    Nkwabi amesema kwamba wachezaji wote wa timu hiyo wapo mazoezini na kikosi kinatarajiwa kuondoka Dar es Salaam kati ya Desemba 30 na 31 kwenda visiwani Zanzibar kwa ajili ya Kombe la Mapinduzi.
    “Leo tutakuwa na kikao cha kuamua siku rasmi ya kwenda Zanzibar, lakini itakuwa kati ya Desemba 30 na 31,”alisema Nkwabi.
    Aidha, Mjumbe huyo amesema kwamba kufuatia kuachia ngazi kwa aliyekuwa Ofisa Habari wa klabu, Ezekiel Kamwaga ‘Mr. Liverpol’, Stanley Philip ameteuliwa kushika nafasi yake, wakati mchakato wa kumpata mrithi wa Katibu Mkuu, Evodius Mtawala aliyeng’atuka pia bado unaendelea.
    Tayari Kamati ya Mashindano ya Kombe la Mapinduzi, imetangaza makundi na ratiba ya hatua ya awali ya michuano hiyo itakayokwenda sambamba na sherehe za miaka 50 ya Mapinduzi ya Zanzibar Januari mwakani.
    Ratiba iliyotolewa na kamati hiyo, inaonesha kuwa jumla ya timu 12 zitaumana kuwania taji hilo, ambazo zimegawiwa katika makundi matatu, kila moja ikiwa na timu nne.
    Timu hizo ni Mbeya City, Pemba Combine, Chuoni na URA kutoka Uganda ambazo zinaunda kundi A, huku kundi B likiwa na timu za Simba, KMKM, AFC Leopards ya Kenya pamoja na KCC kutoka Uganda.
    Mabingwa watetezi wa michuano hiyo Azam FC watakuwa katika kundi C pamoja na makamu bingwa Tusker ya Kenya, Yanga SC na Unguja Combine.
    Kwa mujibu wa ratiba hiyo, pazia la ngarambe hizo litafunguliwa Januari 1, 2014, kwa mechi mbili za kundi B katika uwanja wa Amaan, ambapo wakati wa saa 10:00 mabaharia wa KMKM watapambana na Manispaa ya jiji la Kampala (KCC).
    Aidha saa 2:00 usiku, wekundu wa Msimbazi Simba SC, watakuwa kibaruani dhidi ya AFC Leopards.
    Januari 2, 2014, kutakuwa na mechi nne, katika kila uwanja, kati ya Amaan Unguja na  Gombani Pemba, kutakuwa na michezo miwili.
    Zile za Amaan, ni kati ya Azam FC na Unguja Combine (saa 10:00 jioni) na Yanga dhidi ya Tusker itakayorindima kuanzia saa 2:00 usiku, na huko Gombani shughuli itakuwa kati ya URA na Chuoni (kundi C) watakaovaana saa 8:00 mchana, huku Mbeya City ikitoana jasho na Pemba Combine, saa 10:00 jioni katika mchezo wa kundi A.
    Fainali ya ngarambe hizo itapigwa uwanja Amaan Januari 12 wakati wa saa 2:00 usiku, ambayo ndiyo kilele cha maadhimisho ya sherehe za miaka 50 ya Mapinduzi ya Zanzibar.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: SIMBA SC KWENDA ZANZIBAR BILA LOGARUSIC, MATOLA AANZA KUSUKA KIKOSI CHA UBINGWA MAPINDUZI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top