• HABARI MPYA

  Jumanne, Desemba 31, 2013

  SIMBA SC YAREKEBISHA DOSARI KATIKA USAJILI WAKE, SASA HAKATWI MTU MSIMBAZI

  Na Mahmoud Zubeiry, Dar es Salaam
  KLABU ya Simba SC ya Dars Salaam, imesema kwamba imekwisharekebisha dosari zilizokuwapo kwenye usajili wake na sasa haitakuwa na sababu ya kupunguza mchezaji yeyote kwenye kikosi chake.
  Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Simba SC, Swedi Nkwabi ameiambia BIN ZUBEIRY jana kwamba, wachezaji wote wapya waliosajiliwa katika dirisha dogo wataendelea kuitumikia timu hiyo baada ya kurekebishwa kwa dosari hizo.
  Hakatwi mtu; Simba SC sasa haitatakiwa kupunguza mchezaji mpya baada ya kuwasilisha fomu za kuvunjiana Mkataba na Sino Augustino

   Alisema dosari yenyewe ilikuwa ni kutopeleka fomu za kuvunjiana Mkataba na mchezaji Sino Augustino, hivyo Ikaonekana klabu hiyo imesajili wachezaji zaidi tofauti na nafasi yake.
  “Tatizo lilikuwa tulisahau kupeleka fomu za kuvunjiana Mkataba na Sino Augustino, kwa hivyo ikaonekana kwamba tulisajili wachezaji wengi kuliko idadi tuliyotakiwa, kumbe kulikuwa kuna nafasi ya kuziba pengo la Sino,”alisema Nkwabi.
  Wachezaji waliosajiliwa Simba SC katika dirisha dogo ni makipa Ivo Mapunda, Yaw Berko, beki Donald Mosoti, viungo Awadh Juma, Uhuru Suleiman na mshambuliaji Ali Badru.
  Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) iliyokutana Jumamosi iliyopita kujadili mambo mbalimbali yaliyofikishwa mbele yake ikiwemo usajili wa dirisha dogo, ilibaini dosari kadhaa na kuzipa nafasi klabu zenye matatizo kuwa zimeyarekebisha hadi Januari 10 mwakani.
  Simba ilitajwa kuzidisha idadi ya wachezaji, hivyo kupewa hadi muda huo kupunguza na ikishindwa kazi hiyo itafanywa na Kamati yenyewe. Ilielezwa Simba ilikuwa ina nafasi tano za kujaza kwenye dirisha dogo, lakini ikawasilisha majina ya wachezaji sita.
  Pia klabu nyingine zimetakiwa ama kuvunja mikataba ya wachezaji au kuendelea kuwa nao, na si kuendelea kuwalipa mishahara wakati imeshawaondoa katika orodha yao.
  Kuhusu mshambuliaji Mganda, Emmanuel Okwi aliyesajiliwa Yanga, TFF ilisema inafahamu kuwa klabu ya Simba bado haijalipwa fedha za kumuuza klabu ya Etoile du Sahel ya Tunisia na itasaidia kufuatilia FIFA fedha za mauzo ya mchezaji huyo.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: SIMBA SC YAREKEBISHA DOSARI KATIKA USAJILI WAKE, SASA HAKATWI MTU MSIMBAZI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top