• HABARI MPYA

  Jumatano, Desemba 25, 2013

  MANJI AMEONYESHA UKOMAVU WA HALI YA JUU, SIMBA NAO WAJIANDAE KUKUBALI MATOKEO

  IMEKUWA kawaida, baada ya mechi za watani wa jadi, Simba na Yanga, timu inayofungwa huangushia mzigo wa lawama wachezaji na shutuma za kuhujumu, kiasi cha baadhi kuchukuliwa hatua ikiwemo kufukuzwa.
  Miamba hiyo ya soka ya Tanzania ilikutana Jumamosi Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam katika mchezo maalum wa Nani Mtani Jembe, ulioandaliwa na wadhamini wao, bia ya Kilimanjaro Premium Lager inayotengenezwa na Kampuni ya Bia Tanzania (TBL).
  Katika mchezo huo, Yanga SC walifungwa mabao 3-1, bao lao pekee likifungwa na mshambuliaji wao mpya, Emmanuel Okwi wakati mabao ya Simba yalifungwa na Amisi Tambwe mawili na moja Awadh Juma.

  Kipigo hicho kiliwakera mno wapenzi na mashabiki na hata wanachama wa timu hiyo, kiasi cha kila mmoja kuelekeza shutuma zake kwa anayeamini amesababisha timu ifungwe na zaidi viongozi walilaumiwa sana.
  Lakini mmoja wa wanachama wa siku nyingi wa klabu hiyo, Mzee Ibrahim Akilimali maarufu kama Abramovich aliulaumu uongozi kumsajili kipa Juma Kaseja aliyesimama langoni siku hiyo timu ikifungwa. 
  Wengi walitarajia uongozi nao ungeingia kwenye mkumbo wa kuwashika uchawi wachezaji, lakini hali imekuwa tofauti safari hii baada ya Mwenyekiti wa klabu hiyo, Yussuf Manji kuibuka na kusema mzigo wote wa lawama abebeshwe yeye na si mtu mwingine yeyote, iwe mchezaji au kiongozi wake.
  Na Manji akamtetea na Kaseja, akisema hawakumsajili kwa ajili ya kuifunga Simba SC, bali wamemsajili awasaidie kwenye michuano ya Afrika.
  Manji aliyasema hayo siku moja baada ya mechi, Jumapili asubuhi makao makuu ya klabu, Jangwani, Dar es Salaam wakati akizungumza na Waandishi wa Habari kumjibu Katibu wa Baraza la Wazee la Yanga, Mzee Ibrahim Akilimali aliyeushutumu uongozi kusajili Juma Kaseja ni makosa.
  “Huyu mzee nadhani umri umemzidi, lakini nataka nimkumbushe, huyo Ivo Mapunda aliondoka Yanga akiwa anatumikia adhabu ya kufungiwa miezi sita na uongzi wa wakati huo kwa tuhuma za kufungisha kwenye mechi na Simba SC,”.
  “Lakini pia nataka nimuulize, wakati Simba inarudisha mabao yote matatu Kaseja alikuwapo langoni? Nadhani hivi vitu si vizuri, tuache kulaumiana tushikamane kwa mustakabali mzuri wa timu,”alisema Manji.
  Manji alisema wanaheshimu uwezo wa Kaseja kwa sababu ndiye kipa aliyedaka mechi nyingi za mashindano ya Afrika kati ya makipa wote nchini, hivyo thamani yake haitashuka kwa kufungwa mabao matatu Jumamosi.
  Pamoja na hayo, Manji amesema kwamba mechi ya Jumamosi haikuwa na uzito wowote kwao ni sawa na bonanza au fete, hivyo kufungwa haijawaumiza. “Tuliamua kucheza kumfurahisha  mdhamini TBL, tumefungwa lakini bado tunaongoza ligi, hatujapoteza pointi hata moja, ile ilikuwa fete tu,”alisema Manji.
  Manji amekiri Simba SC walicheza vizuri zaidi siku hiyo na walistahili ushindi na akawapongeza kwa hilo, pamoja na wadhamini, TBL kwa kuandaa mechi hiyo.
  Manji alisema kuelekea mzunguko wa pili wa Ligi Kuu na Ligi ya Mabingwa Afrika wataboresha timu na benchi la ufundi na timu itaenda tena kambini Ulaya, hivyo anaamini mwakani makali yao yatafufuka na watatetea ubingwa.  
  Hiki ni kitu kipya kabisa katika utamaduni wa vigogo hao, kukubali kufungwa, kupongeza wapinzani na kuamua kuangalia mbele kwa kusahau yaliyopita.
  Na huu ni utamaduni ambao unapaswa kuenziwa kuanzia sasa, kwa sababu Simba na Yanga zitaendelea kumenyana milele na mshindi lazima apatikane au iwe sare- na hiyo ndiyo soka.
  Yanga wametoa mfano, wamepigwa tatu mchana kweupe, lakini wamekubali kipigo na wanajipanga kwa mashindano yajayo. Hiyo ndiyo soka. Na Simba SC siku wakifungwa, wasibughudhi wachezaji, wakubali matokeo, utamaduni mpya uchukue nafasi. Heri ya Krisimasi na mwaka mpya. 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: MANJI AMEONYESHA UKOMAVU WA HALI YA JUU, SIMBA NAO WAJIANDAE KUKUBALI MATOKEO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top