• HABARI MPYA

  Ijumaa, Desemba 20, 2013

  KOCHA AZAM AJA KESHO KUANZA RASMI KAZI CHAMAZI

  Na Mahmoud Zubeiry, Dar es Salaam
  KOCHA mpya wa Azam FC, Mcameroon Joseph Marius Omog anatarajiwa kuwasili kesho mjini Dar es Salaam kuanza rasmi kazi ya kukinoa kikosi cha timu hiyo kwa ajili ya michuano ya Kombe la Mapinduzi pamoja na mzunguko wa pili wa Ligi Kuu ya Bara na Kombe la Shirikisho Afrika mwakani.
  Mwalimu huyo aliyeipa Leopard FC ya Kongo Brazaville Kombe la Shirikisho Afrika mwaka jana, awali alikuja nchini Novemba 30, mwaka huu na kusaini Mkataba wa kuifundisha timu hiyo, kisha kurejea kwao kujipanga.
  Anawasili kesho; Kocha mpya wa Azam, Joseph Marius Omog anakuja leo kuanza kazi Chamazi

  Kocha Msaidizi wa Azam FC, Kalimangonga Sam Daniel Ongala aliiambia BIN ZUBEIRY jana kwamba, Omog atatua kesho kuanza rasmi kazi.
  Tayari wachezaji wa Azam wapo mazoezini kwa zaidi ya wiki moja Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam wakiongozwa na Kali kwa kushirikiana na kocha wa akademi ya klabu hiyo, Vivik Nagul. 
  Omog, mchezaji wa zamani wa Yaounde ni mwalimu wa kiwango cha juu cha ufundishaji soka na mazoezi ya viungo aliyehitimu vizuri mafunzo yake katika Chuo cha Vijana na Michezo, INJS mjini Yaounde, Cameroon. Alikwenda kujiendeleza kielimu nchini Ujerumani na kwa pamoja na Pierre Njili na Martin Ndtoungou walipata Stashahada za ukocha na leseni za UEFA daraja la B mwaka 1987. 
  Aliporejea nchini mwake, Joseph Marius Omog, alifundisha timu kadhaa kama Fovu ya Baham na Aigle ya Menoua na akazifikisha fainali ya Kombe la Cameroon klabu zote. 
  Mwaka 2001 aliteuliwa kuwa Msaidizi wa kocha Mjerumani, Winfried Schafer katika timu ya taifa ya Cameroon, Simba Wasiofungika chini ya Nahodha Samuel Eto’o haswa kutokana na kujua kwake Kijerumani, kwa sababu kocha huyo alikuwa hazungumzi Kiingereza wala Kifaransa, lugha zinazotumika nchini humo. 
  Mwaka 2003 aliteuliwa kuwa kocha Mkuu wa timu ya taifa baada kuondoka kwa Winfried Schafer, lakini akafukuzwa mwaka 2010 kutokana na matokeo mabaya na kushindwa kuiwezesha Cameroon kufuzu Fainali za Mataifa ya Afrika.
  Akaamua kutoka nje ya nchi na mwaka 2011 alijiunga na AC Leopard ya Kongo, ambayo aliiwezesha kutwaa Kombe mwaka huo huo na kuipa tiketi ya kucheza Kombe la Shirikisho. 
  Na akafanikiwa kuiwezesha timu hiyo kutwaa Kombe hilo la Afrika kwa kuifunga Djoliba ya Mali mabao 2-1 katika mchezo wa marudiano na kutengeneza ushindi wa jumla wa 4-3.
  Je, mafanikio hayo atayahamishia Azam? Bila shaka hilo ni jambo la kusubiri na kuona.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: KOCHA AZAM AJA KESHO KUANZA RASMI KAZI CHAMAZI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top