• HABARI MPYA

  Jumatatu, Desemba 30, 2013

  ZAHOR PAZI: BABA ANANINYIMA RAHA SIMBA SC HADI NAJUTA

  Na Mahmoud Zubeiry, Dar es Salaam
  MSHAMBULIAJI wa Simba SC, Zahor Pazi amesema kwamba anajikuta katika wakati mgumu tangu baba yake, Iddi Pazi kuajiriwa kuwa kocha wa makipa wa Simba SC, jambo ambalo linamnyima raha.
  Akizungumza na BIN ZUBEIRY jana, Zahor alisema kwamba yeye alisajiliwa Simba SC mwanzoni tu mwa msimu, wakati baba yake ni mwezi huu ameajiriwa kuwa kocha wa makipa, lakini inaonekana kama yeye aliingia timu hiyo kwa mgongo wa baba yake huyo, kipa wa zamani wa kimataifa nchini.
  Mtoto wa kocha; Zahor Pazi amelalamikia kuonekana kama aliingia Simba kwa mgongo wa baba yake

  “Inanikera sana, kila mtu mtoto wa kocha mtoto wa kocha, utafikiri mimi baba yangu ndiye aliyenisajili timu hii, mimi niliingia Simba SC kabla ya baba, yeye kaja kanikuta. Na pia mimi siyo kipa, mimi nipo chini ya Logarusic (Zdarvko, kocha Mkuu) na Matola (Suleiman, kocha Msaidizi), yeye baba anahangaika na akina Ivo huko (Mapunda, kipa),”alisema Pazi.
  Zahor amesema anaamini juu ya uwezo wake na iko siku nyota yake itang’ara Simba SC kwa kuwa yeye ni mchezaji mzuri. “Nimesajiliwa hapa kutokana na uwezo wangu, basi iko siku nitaonyesha uwezo wangu. Sikuja hapa kwa msaada wa baba,”alisema Zahor.
  Zahor alisajiliwa Simba SC mwanzoni mwa msimu akitokea JKT Ruvu ambayo nayo ilimtoa Azam FC alikotua akitokea Mtibwa Sugar. Ni kati ya vijana wanaochipukia vizuri katika soka a Tanzania, ambao wanatarajiwa kuwa tegemeo la taifa baadaye. 
  Kama si kuwekwa benchi na makocha waliotangulia, chini ya Kocha Mkuu Alhaj Abdallah Athumani Seif ‘King Kibaden’ na Msaidizi wake, Jamhuri Mussa Kihwelo ‘Julio’, bila shaka Zahor angeendelea kuwa mchezaji wa timu ya taifa kama alivyokuwa wakati anasajiliwa na Wekundu hao wa Msimbazi.      
  Iddi Pazi ‘Father’ alikuwa kipa hodari na tegemeo la Simba SC miaka ya 1980 hadi 1990 mwanzoni na amewahi kuwa kocha wa makipa mara kadhaa baada ya kustaafu.

  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: ZAHOR PAZI: BABA ANANINYIMA RAHA SIMBA SC HADI NAJUTA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top