• HABARI MPYA

  Jumatano, Desemba 25, 2013

  KIPA SIMBA SC AFARIKI DUNIA

  Na Princess Asia, Dar es Salaam
  KIPA wa zamani wa klabu ya Simba SC ya Dar es Salaam, James Kisaka amefariki dunia asubuhi ya leo katika hospitali ya Burhan, Dar es Salaam.
  Mdogo wa marehemu, Benny Kisaka ameiambia BIN ZUBEIRY asubuhi hii kwamba, James Kisaka amefariki baada ya kusumbuliwa na maradhi ya kichwa, macho na miguu kwa muda mrefu.
  Pumzika kwa amani James Kisaka, utakumbukwa daima

  Benny amesema mwili wa marehemu kwa sasa bado upo hospitali na wanafamilia wanajikusanya kukutana kupanga utaratibu wa mazishi.
  Kisaka mara ya mwisho alikuwa kocha wa makipa wa Simba SC na alifanya kazi hiyo hadi mwishoni mwa mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu ya Bara msimu huu.
  Baada ya hapo ndipo alipoanza kusumbuliwa na maradhi hadi hali yake ilivyokuwa mbaya kiasi cha kuaga dunia.  
  James Kisaka kuia akiwa na Alhaj Abdallah Athumani Seif 'King Kibaden' na Jamhuri Kihwelo 'Julio' na James Kisaka katika moja ya mechi za mzunguko wa kwanza Ligi Kuu ya Bara. Pumzika kwa amani James. Chini marehemu James akimpa mazoezi kipa wa zamani wa Simba, Juma Kaseja.


  James Kisaka alizaliwa mwaka 1955 mjini Dar es Salaam na alipata elimu yake ya Msingi katika shule ya Oysterbay na baadaye sekondari za Mzizima na Tambaza, Dar es Salaam pia.
  Alianza kupata umaarufu wa soka tangu anasoma na haikushangaza aliposajiliwa na Sigara akiwa kijana mdogo chini ya umri wa miaka 20.
  Baadaye alichezea Nyota Nyekundu, Simba SC, Small Simba ya Zanzibar, Volcano ya Kenya alipokwenda na Zamoyoni Mogella na LiIa Shomari (pia marehemu) na Ndovu ya Arusha.
  Alikuwemo kwenye kikosi cha Simba kilichokwenda ziara ya mafunzo nchini Brazil mwaka 1981.
  Kisaka atakumbukwa kwa upole wake na ufanyaji kazi kwa bidii enzi za uhai wake. Mungu aiweke pema peponi roho ya marehemu. Amin.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: KIPA SIMBA SC AFARIKI DUNIA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top