• HABARI MPYA

  Alhamisi, Desemba 26, 2013

  AZAM FC YAWAPA ZAWADI NONO YA KRISIMASI MASHABIKI WAKE, YAIFUMUA RUVU YA MKWASA 3-0

  Na Mahmoud Zubeiry, Chamazi
  AZAM FC imewapa kifurishi cha zawadi mashabiki wake, baada ya ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Ruvu Shooting ya Pwani katika mchezo wa kirafiki uliofanyika Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam jioni hii.
  Hadi mapumziko, tayari Azam FC, walio chini ya kocha mpya Mcameroon, Joseph Marius Omog walikuwa mbele kwa mabao 2-0.
  John Raphael Bocco alitangulia kuifungia Azam bao la kwanza dakika ya 10 kazi nzuri Mganda, Brian Umony ambaye anaonekana kurudi katika kasi yake ya mchezo baada ya kuandamwa na majeruhi msimu uliopita. 
  Wauaji; John Bocco akipongezana na Kipre Tchetche jioni ya leo Chamazi

  Bao la pili liliwekwa nyavuni kwa mkwaju wa penalti na mshambuliaji wa Ivory Coast, Kipre Herman Tchetche dakika ya 30, baada ya Ayoub Kitala kuurudisha kwa mkono mpira uliokuwa unaelekea nyavuni.
  Refa Israel Mujuni Nkongo alimpa kadi nyekundu beki wa Ruvu na kuifanya timu ya Charles Boniface Mkwasa ‘Master’ imalizie dakika 50 za pambano hilo ikiwa pungufu.
  Mchezo ulikuwa mzuri kipindi cha kwanza timu zote zikicheza soka ya kufundishwa na makocha waliosomea Ujerumani, Mkwasa wa Ruvu na Omog wa Azam FC.
  Kipindi cha pili timu zote zilifanya mabadiliko karibu ya vikosi vizima na aliyekuwa kivutio katika ngwe hiyo ni mshambuliaji mpya kutoka Ivory Coast Muamad Ismael Kone aliyeingia pia kwa upande wa Azam. 
  Kone alionyesha uwezo mkubwa sana wa kucheza soka na akafunga bao zuri la tatu dakika ya 57.
  Baada ya mechi hiyo, Azam inatarajiwa kwenda Zanzibar kutetea Kombe la Mapinduzi, michuano inayoanza mapema Januari 1, mwakani, wakati Ruvu itaendelea na maandalizi ya mzunguko wa pili wa Ligi Kuu.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: AZAM FC YAWAPA ZAWADI NONO YA KRISIMASI MASHABIKI WAKE, YAIFUMUA RUVU YA MKWASA 3-0 Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top