• HABARI MPYA

  Jumamosi, Desemba 21, 2013

  SIMBA SC YADHIHIRISHIA UBABE KWA YANGA, YAWAPIGA 3-1 NA OKWI WAO

  Nahodha wa Simba SC, Haruna Shamte akiwa ameinua Kombe baada ya kukabidhiwa na mgeni rasmi, Waziri wa Sheria na Katiba, Mathias Chikawe mwenye suti nyeusi kulia baada ya kuifunga Yanga SC mabao 3-1  
  Na Mahmoud Zubeiry, Dar es Salaam
  SIMBA SC ndiye Mtani Jembe 2013. Hiyo inafuatia Wekundu hao wa Msimbazi kuwafunga watani wao wa jadi, Yanga mabao 3-1 Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
  Mabao ya Simba yamefungwa na Amisi Tambwe mawili na Awadh Juma moja, wakati la Yanga lilifungwa na Emmanuel Okwi. 
  Katika mchezo huo, Yanga ilimaliza pungufu baada ya beki wake, Kevin Yondan kutolewa nje kwa kadi ya pili ya njano, baada ya kumchezea rafu Ramadhani Singano ‘Messi’. 
  Mfungaji wa mabao mawili ya Simba SC leo, Amisi Tambwe akipongezwa na Issa Rashid 'Baba Ubaya'
  Hadi mapumziko, tayari Simba SC walikuwa mbele kwa mabao 2-0 ambayo yote yalifugwa na Amisi Tambwe dakika ya 14 na 44.

  Tambwe alifunga bao la kwanza baada ya kupokea pasi ya kiufundi ya Said Hamisi Ndemla na kumtungua kipa Juma Kaseja.
  Mpira uliozaa bao hilo ulianzia kwa Jonas Mkude aliyeinasa pasi ya Athumani Iddi ‘Chuji’ kuelekea kwa Frank Domayo, akampasia Henry Joseph ambaye alimpelekea Ndemla, aliyempa mfungaji.
  Tambwe alifunga bao la pili kwa penalti baada ya beki wa Yanga, David Luhende kumchezea rafu Ramadhani Singano ‘Messi’ aliyeingia kipindi cha kwanza kuchukua nafasi ya Ndemla. 
  Kwa ujumla, Simba SC ndiyo waliocheza vizuri kipindi cha kwanza wakionana kwa pasi za uhakika, wakati wapinzani wao walikosa mbinu za kuipenya ngome ya Wekundu wa Msimbazi, iliyoongozwa na Mkenya Donald Mosoti Omwanwa.
  Krosi nyingi za Mrisho Ngassa kutoka kulia ama zilidakwa na Ivo Mapunda au zilipitiliza nje.
  Kipindi cha pili, Yanga SC walianza kwa mabadiliko, wakiingiza wachezaji watatu kwa mpigo, Emmanuel Okwi, Simon Msuva na Hassan Dilunga kuchukua nafasi za Hamisi Kiiza, Didier Kavumbangu na Athumani Iddi ‘Chuji’.  
  Lakini mabadiliko hayo hayakuisaidia Yanga SC kwani wapinzani wao Simba walifanikiwa kupata bao la tatu lililofungwa na Awadh Juma.
  Bao hilo lilitokana na makosa ya beki Mbuyu Twite kumrudishia mpira mfupi kipa Juma Kaseja, ambaye alijaribu kuuweka sawa, lakini akazidiwa na Awadh aliyeupokonya na kuusukumia nyavuni.
  Baada ya bao hilo, Simba walianza kucheza kwa kujiamini zaidi wakipiga pasi za kusisimua na kuwafurahisha mashabiki wao, huku Yanga wakihaha kusaka bao la kufutia machozi.
  Alikuwa Okwi aliyeifungia Yanga bao la kufutia machozi dakika ya 87, akiunganisha krosi ya Haruna Niyonzima. 
  Baada ya mchezo huo, Yanga walikabidhiwa Medali za Fedha Kombe dogo na hundi milioni 98.9, wakati wapinzani wao walivalishwa Medali za Dhahabu, Kombe kubwa na hundi ya Sh. Milioni 1 kutokana na promosheni ya Nani Mtani Jembe.
  Katika mchezo huo, kikosi cha Yanga kilikuwa; Juma Kaseja, Mbuyu Twite, David Luhende/Oscar Joshua dk79, Nadir Haroub ‘Cannavaro’/Juma Abdul dk53, Kevin Yondan, Athumani Iddi ‘Chuji’/Hassan Dilunga dk46, Haruna Niyonzima, Frank Domayo, Didier Kavumbangu/Simon Msuva, Mrisho Ngassa/Jerry Tegete dk69 na Hamisi Kiiza/Emmanuel Okwi dk46.
  Simba SC; Ivo Mapunda, Haruna Shamte, Issa Rashid ‘Baba Ubaya’, Joseph Owino, Donald Mosoti, Jonas Mkude, Haroun Chanongo/Uhuru Suleiman dk55, Henry Joseph/Ramadhani Chombo ‘Redondo’ dk34/Abdulhalim Humud dk72, Amisi Tambwe/Amri Kiemba dk54, Said Ndemla/Ramadhani Singano ‘Messi’dk27 na Awadh Juma. 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: SIMBA SC YADHIHIRISHIA UBABE KWA YANGA, YAWAPIGA 3-1 NA OKWI WAO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top