• HABARI MPYA

  Alhamisi, Desemba 19, 2013

  DAKIKA 90 SARE MTANI JEMBE, PENALTI ZITAAMUA MSHINDI SIMBA NA YANGA JUMAMOSI

  Na Mahmoud Zubeiry, Dar es Salaam
  IWAPO dakika 90 za mchezo wa Nani Mtani Jembe baina ya Simba SC na mahasimu wao, Yanga zitamalizika kwa sare Jumamosi Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, basi moja kwa moja sheria ya mikwaju ya penalti itachukua nafasi yake, imeelezwa.
  Kaimu Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Boniphace Wambura Mgoyo ameiambia BIN ZUBEIRY mchana huu kwamba, klabu hizo mbili zilikutanishwa katika kikao na kukubaliana mambo kadhaa kuhusu mchezo huo.
  Wambura amesema walikubaliana lazima mshindi apatikane na iwapo dakika 90 zikimalizika kwa sare watapigiana penalti tano tano kusaka mshindi.
  Mechi iliyopita ya watani wa jadi iliisha kwa sare ya 3-3 Uwanja wa Taifa, lakini Jumamosi lazima mshindi apatikane

  Mchezo huo, unaoandaliwa na wadhamini wa klabu hizo, Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) kupitia bia ya Kilimanjaro Premium Lager, unatarajiwa kuchezeshwa na refa Ramadhan Ibada ‘Kibo’ kutoka Zanzibar, atakayesaidiwa na Ferdinand Chacha wa Bukoba na Simon Charles kutoka Dodoma, wakati refa wa akiba atakuwa Israel Nkongo wa Dar es Salaam na mtathimini wa waamuzi ni Soud Abdi wa Arusha.
  Viingilio vya mechi hiyo ni Sh. 5,000 kwa viti vya rangi ya kijani, bluu Sh. 7,000, rangi ya chungwa Sh. 10,000, VIP C Sh. 15,000, VIP B Sh. 20,000 wakati VIP A Sh. 40,000 na tiketi zitaanza kuuzwa siku moja katika vituo mbalimbali, mchezo huo utakaoanza Saa 10:00 jioni.
  Vituo ambavyo tiketi hizo zitauzwa kesho (Ijumaa) ni Shule ya Sekondari Benjamin Mkapa, Sokoni Kariakoo, mgahawa wa Steers ulioko mtaa wa Ohio/Samora, Oilcom Ubungo, Kituo cha Mafuta Buguruni, Dar Live Mbagala, Uwanja wa Uhuru, na BMM Salon iliyoko Sinza Madukani.
  Wachezaji wanaoruhusiwa kucheza mechi ya kesho ni wale waliosajiliwa ama kikosi cha kwanza au timu ya vijana pamoja na wapya ambao wameombewa usajili katika dirisha dogo.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: DAKIKA 90 SARE MTANI JEMBE, PENALTI ZITAAMUA MSHINDI SIMBA NA YANGA JUMAMOSI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top