• HABARI MPYA

  Alhamisi, Desemba 26, 2013

  MESSI AMEIWEKA YANGA SC KATIKA WAKATI MGUMU MNO

  Na Mahmoud Zubeiry, Dar es Salaam
  KAMA kungekuwa na tuzo ya Mchezaji Bora wa mechi ya Nani Mtani Jembe, baina ya mahasimu wa jadi nchini, Simba na Yanga Jumamosi iliyopita Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam basi mtu ambaye angestahili kupewa ni Ramadhani Yahya Singano ‘Messi’.
  Katika mchezo huo ambao Simba SC ilishinda mabao 3-1, Messi alitokea benchi dakika ya 27 kwenda kuchukua nafasi ya Said Ndemla, wakati huo Simba SC inaongoza bao 1-0 lililofungwa na Amisi Tambwe.
  Kitoto Nuksi; Unadhani Ernie Brandts atakuwa na hamu ya kukutana na Ramadhani Singano kwa sasa?

  Mwisho wa mchezo, Simba SC ikashinda 3-1 na Messi alikuwa kila kitu uwanjani na aliweza kumpita kila mchezaji wa Yanga SC pamoja na kuwaadhiri wachezaji bora na ghali wa klabu hiyo kama Kevin Yondan, Haruna Niyonzima na David Luhende.
  Baada ya mchezo huo, Yanga imetangaza kumfukuza kocha wake Mholanzi, Ernie Brandts ambaye ilimuongezea Mkataba mwezi uliopita tu aliporejea kutoka mapumzikoni nyumbani kwao.
  Messi 'akimkosea adabu' Yondan
  Messi 'akimvunjia heshima' Haruna Niyonzima
  Messi 'akimdhalilisha' David Luhende

  Hili ni suala ambalo hakika halikuwa kabisa kwenye mipango ya Yanga SC, yaani limekuja ghafla. Yanga tayari walikuwa wana mipango mirefu na Brandts ambayo imevunjika ghafla na sasa viongozi wake wanahaha kutafuta kocha mbadala.
  Ni zoezi gumu kumpata kocha mzuri kwa haraka na katika mazingira kama haya ambayo Yanga wanatafutia kocha. Januari 1 wanatakiwa kuwa Zanzibar kwenye Kombe la Mapinduzi, wanalazimika kupata kocha haraka.
  Mwishoni mwa Januari mzunguko wa pili wa Ligi Kuu unaanza na Februari Ligi ya Mabingwa Afrika inaanza, Desemba ikiwa inaelekea ukingoni, Yanga hawajafanikiwa japo kuketi meza moja na kocha mpya.
  Kitoto hakifai kile; Kwa yote aliyoyafanya, Messi ameyafanya maisha ya hawa mabwana watatu yawe magumu kwa sasa. Kutoka kulia ni Kocha Ernie Brandts, kocha wa makipa Razack Ssiwa na Kocha Msaidizi, Freddy Felix Minziro

  Yanga inahitaji kuchukua kocha ambaye ana rekodi nzuri ye utendaji kazi, kuchukua mataji, nidhamu na mwenye kuweza kuvumilia shida na tabu za soka ya Afrika Mashariki.
  Wapinzani wao Simba SC safari hii wamefanikiwa katika hilo mbele ya Mcroatia, Zdravko Logarusic ambaye akiwa Gor Mahia ya Kenya aliipa mataji na yeye mwenyewe akashinda tuzo za kocha bora.
  Tazama mtihani ambao wanao Yanga hivi sasa kusaka kocha mpya na huwezi kukwepa kusema yote haya kayasababisha huyu mtoto Ramadhani Yahya Singano ‘Messi’.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: MESSI AMEIWEKA YANGA SC KATIKA WAKATI MGUMU MNO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top