• HABARI MPYA

    Sunday, December 08, 2013

    HIZI NI DALILI ZA MANJI NA TIMU YAKE ‘KUFELI’ YANGA

    WIKI hii klabu ya Yanga ya Dar es Salaam imetoa ripoti yake ya mapato na matumizi kwa kipindi cha miezi sita tangu Januari 14, 2013 hadi Julai 14, 2013 na kuonyesha kwamba bado haijimudu na inajiendesha kwa hasara.
    Hii ni mara ya pili kwa Yanga, chini ya Uenyekiti wa Alhaj Yussuf Mehboob Manji kutoa ripoti ya mahesabu hayo kwa ajili ya wapenzi, mashabiki, na wanachama na jamii  kwa ujumla.

    Kwa mujibu wa tovuti ya klabu hiyo, baadhi ya gharama kubwa kwa klabu ni pamoja na usajili wachezaji na mishahara. Katibu mkuu wa Yanga, Lawrence Mwalusako alisema mapato makubwa ya klabu yanatokana na viingilio vya mechi na ufadhili.
    Akasema juhudi mbalilmbali zinafanyika kuongeza kipato cha klabu kama kuingia mikataba ya ufadhili, kutumia hakimiliki za klabu na kwamba uongozi unajitahidi kuweza kudhibiti matumizi ya klabu kama njia moja ya kuhakikisha klabu inajitegemea.
    Akasema klabu bado inaendelea kutegemea udhamini wa Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) ambayo kwa sasa inatoa wastani wa Sh. Milioni 30. 25 kwa mwezi, kwa lengo la kuiwezesha klabu kulipia mishahara ambayo wastani wake ni zaidi ya Sh. Milioni 60 kwa mwezi. 
    Akasema tayari klabu imekwishaomba mazungumzo na TBL kuboresha mkataba huo na kwamba katika kipindi cha Januari 2013 hadi Julai 2013 klabu iliweza kupata Milioni 110 kama zawadi mbalii mbali za ushindi ikiwemo Milioni 15 kutoka Vodacom kwa kuwa timu yenye nidhamu.
    Bado kuna mali za klabu hazijathaminiwa zikiwemo majengo na kadhalika. Manji na Kamati yake ya Utendaji, tayari wametimiza mwaka mmoja zaidi tangu waingie madarakani.
    Watu wengi hata wasio wana Yanga, walifurahia kuingia kwa Manji na timu yake kuongoza klabu hiyo wakiamini na mwanzo wa mapinduzi ya kweli katika klabu hizo kongwe, pamoja na wapinzani wao wa jadi, Simba SC.
    Na Manji alionyesha dalili za matumaini baada ya kuingia madarakani, kutokana na mikakati aliyoianzisha kama kuunda Kamati mbalimbali zinazohusisha vigogo wa nchi hii kwa lengo la kuleta mapinduzi klabuni hapo.
    Majina ya watu kama Ridhiwani Kikwete, mtoto wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Balozi Ammy Mpungwe na Waziri, Kapteni George Mkuchika yalitajwa kwenye Kamati mbalimbali za kuboresha Yanga.
    Lakini kiasi cha mwaka mmoja baadaye, Yanga bado inaendelea na wimbo wa “Tunajiendesha kwa hasara”. Hizi ni dalili za uongozi kukosa ubunifu, jambo ambalo huwezi kuamini kwa mfanyabiashara mkubwa kama Manji na vigogo hao waliotajwa.
    Kwa ujumla viongozi wengi wa Yanga ni wafanyabiashara wenye mafanikio, mbali ya Manji, akina Abdallah Bin Kleb, Seif Ahmed ‘Magari’, Mussa Katabro na wengine na huwezi kuona kwa nini wameshindwa kuhamishia mafanikio hayo Yanga.
    Si ufahari Yanga yenye viongozi wa aina hiyo kulia eti wanajiendesha kwa hasaram, zaidi ni kujidhalilisha mbele ya watu walioawaamini na kuwapa dhamana. Nini kinashindikana Yanga!
    Hakuna kinachoshindikana, bali watu hawatilii mkazo, ama wametingwa na shughuli zao binafasi, hivyo wanakosa muda wa kutosha wa kufanya shughuli za Yanga au hawana imani.
    Yanga wana jengo Mtaa wa Mafia, Kariakoo, Dar ves Salaam ambalo Manji aliunda Kamati ya kulikarabati liwe jengo la kitegauchumi la klabu chini ya Mwenyekiti, Ridhiwani Kikwete, lakini hadi leo hakuna kilichofanyika.
    Yanga wana jengo kuu na eneo kubwa kubwa pamoja na Uwanja wa pale Jangwani, lakini tangu Manji aingie madarakani, hakuna japo ukarabati uliofanyika zaidi ya ule alioufanya mwaka 2007 akiwa bado mfadhili pekee.
    Hata ule mpango wa kupangisha wawekezaji kama taasisi za fedha na maduka pale Jangwani sijui uliishia wapi.    
    Kama Manji na timu yake hawatafikiria umuhimu wa kutumia rasilimali za klabu ikiwemo nembo yake kuifanya klabu iweze kujitegemea, basi kilio hiki cha “Tunajiendesha kwa hasara” hakitaisha.
    Maelfu wanavaa jezi za Yanga barabarani nchi nzima, na wananunua bidhaa nyingine kibao zenye nembo ya klabu hiyo ikiwemo hadi bendera, lakini leo inatoka ripoti ya mapato na matumizi, hakuna hata senti iliyotokana na eneo hilo. Hii tuiite nini?
    Najua, Yanga hawapendi kuambiwa ukweli na ukifanya hivyo unafufua chuki, lakini BIN ZUBEIRY ataendelea kuwa mvumilivu juu ya hilo. Ukweli ni kwamba, uongozi wa Yanga chini ya Manji kulia klabu inajiendesha kwa hasara wakati ina rasilimali nyingi, ni dalili za kufeli. Jumapili njema. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: HIZI NI DALILI ZA MANJI NA TIMU YAKE ‘KUFELI’ YANGA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top