• HABARI MPYA

    Sunday, March 01, 2009

    STARS FUNGU LA KUKOSA

    Mfungaji wa bao la kuongoza nla Stars, Nsajigwa Shadrack


    na abdul mohammed, bouake
    KISICHO riziki hakiliki, walisema wahenga, naam usemi huo ulidhihirika jana mjini hapa kwenye Uwanja wa Stade de la Paix, baada ya Tanzania, Taifa Stars, kulazimishwa sare ya 1-1 na Zambia katika mchezo wa kuwania kuingia Nusu Fainali ya Michuano ya Ubingwa wa Mataifa ya Afrika (CHAN), inayoendelea nchini hapa.
    Stars ilikuwa ya kwanza kupata bao kwenye mchezo huo, dakika ya 87, mfungaji akiwa Nahodha, Nsajigwa Joel Shadrack Mwandemele kwa mkwaju wa penalti, baada ya beki mkongwe wa Zambia Elijah Tana kuunawa mpira kwenye eneo la hatari.
    Nsajigwa alijitolea kwenye kupiga penalti hiyo ya lawama iliyotolewa na mwamuzi Arbitre Ibrahim Chaibou wa Niger na kumchambua kipa wa Zambia, Kaumbwa Davy.
    Lakini Dennis Banda, aliisawazishia Zambia katika dakika za nyongeza, (dakika ya 94) kufuatia kona iliyoelekezwa langoni mwa Stars.
    Kwa matokeo hayo, Zambia inaungana na Senegal kutinga Nusu Fainali, wakati Tanzania inarejea nyumbani Dar es Salaam kutokana na kushika nafasi ya tatu kwa pointi zake nne, mabao mawili ya kufunga na mawili ya kufungwa.
    Kabla ya mechi ya jana, Tanzania ilifungwa mechi ya kwanza na Senegal 1-0, kabla ya kushinda mechi ya pili na wenyeji Ivory Coast walioshika mkia kwenye kundi hilo, A kwa kuambulia pointi moja.
    Zambia imeongoza kwa pointi zake tano, mabao manne ya kufunga na moja la kufungwa, wakati Senegal kwa pointi zake tano pia na bao moja la kufunga, ikiwa haijafungwa hata bao moja nayo imeingia Nusu Fainali kama mshindi wa pili wa kundi hilo.
    Stars ambayo ilikwenda kupumzika ikiwa imepata kona tatu ambazo zote hazikuzaa matunda, pia ilipata nafasi nyingine kadhaa ambazo ilishindwa kuzitumia.
    Mfano dakika ya tano, Mussa Hassan Mgosi alimpa ‘pande’ safi Kiggi Makasy, lakini akapiga shuti kali lililopaa juu ya lango na dakika ya nane pia Mrisho Ngasa alimpa pasi nzuri Nizar Khalfan ambaye naye shuti lake la chini chini lilipanguliwa na kipa wa Zambia, Kaumbwa Davy na kuwa kona,
    Kipindi cha pili Stars iliendelea kupigana uwanjani na dakika ya 66 Ngassa alifanikiwa kuitoka ngome ya Zambia, lakini akachezewa rafu na beki mmoja wa Chipolopolo na mwamuzi kuamuru ipigwe, ambayo ilipigwa na Abdi Kassim ‘Babbi’ lakini haikuzaa matunda.
    Mwamuzi wa mchezo huo, alikuwa ni Arbitre Ibrahim Chaibou wa Niger, aliyesaidiwa na Diarra Balla wa Mali na Haruna Ayuba wa Ghana upande wa pili, wakati mezani alikuwepo Doue Nomandiez Desire wa Ivory Coast.
    Mechi kati ya wenyeji na Senegal ilichezeshwa na Arbitre Lwanja Verson wa Malawi, aliyesaidiwa na Edibe Peter wa Nigeria na Saadallah Chokri wa Tunisia, wakati mezani alikuwepo Labrosse Jean Claude wa Shelisheli.
    Baada ya mchezo huo, wachezaji wa Stars walikuwa wenye huzuni kubwa, wengine wakianguka chini na kuinuliwa na wenzao ambao kidogo walijimudu licha ya mfadhaiko uliowakuta kwa kuzamishwa dakika za majeruhi.
    Pamoja na kutolewa, Stars ilipigana kiume kuanzia mchezo wa kwanza na hasa jana.
    Kikosi cha Stars jana kilikuwa Shaaban Dihile, Nsajigwa Shadrack, Juma Jabu, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Salum Sued, Nurdin Bakari, Henry Joseph, Nizar Khalfan/Abdi Kassim, Mussa Mgosi, Mrisho Ngassa na Kiggi Makasi.
    Zambia: Kaumbwa Davy, Mulenga Nyambe, Sakuwaha Jonas, Tana Elijah, Banda Dennis, Banda Henry Phiri, Kasunga Patrick, Njobvu William, Chilufya Jimmy Chisenga, Singuluma Given na Lwipa Ignatius.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: STARS FUNGU LA KUKOSA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top