• HABARI MPYA

    Friday, March 13, 2009

    LIGI KUU BARA YAREJEA LEO, YANGA WIKI IJAYO...

    Kocha wa Villa Squad, Kenny Mwaisalbula


    WAKATI Villa Squad ikianza kampeni zake za kukwepa kushuka daraja leo itakapokipiga na JKT Ruvu katika michuano ya Ligi Kuu Tanzania Bara, safari ya dakika 180 za Yanga kuelekea ubingwa huo zinatarajia kuanza Alhamisi ijayo.
    Villa yenye pointi 14 na kushika nafasi ya pili kutoka mwisho itaanza mbio za kukamilisha mechi zake saba zilizosalia kwenye kivumbi hicho kwa kucheza na 'Watoto wa Pwani', JKT Ruvu katika Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.
    Kimahesabu Yanga ambayo ni mabingwa watetezi wa ligi hiyo inahitaji ushindi ndani ya dakika mechi zake mbili na kutimiza dakika 180 ili kuweka kibindoni pointi sita zitakazowabesha ubingwa huo.
    Hadi sasa timu hiyo imefikisha pointi 42 na kama ikishinda mechi mbili kati ya saba zilizobaki itakuwa imetwaa ubingwa moja kwa moja.
    Yanga anaongoza ligi hiyo kwa idadi kubwa ya pointi dhidi ya Kagera Sugar inayoshika nafasi ya pili kutokana na kuwa na pointi 26.
    Vijana hao wa Kaitaba, Kagera kama watashinda mechi zao zote saba zilizosalia watafikisha pointi 47, moja pungufu dhidi ya Yanga ikiwa watacheza na kushinda mechi zao mbili kati ya saba zilizobaki.
    Kinyang'anyiro pekee kwenye ligi hiyo kilichobaki ni kuwania nafasi ya pili ili kukata tiketi ya kucheza michuano ya Kombe la Shirikisho barani Afrika (CAF).
    Mchuano huo unazihusisha Kagera, mabingwa wa Bara wa 2007, Simba yenye pointi 24, Tanzania Prisons pointi
    22, Mtibwa Sugar, Ruvu JKT na Toto African zenye pointi 21 kila moja.
    Yanga ambao keshokutwa itakuwa na kibarua kigumu mbele ya mabingwa wa Afrika, Al Ahly ya Misri wakati zitakapomenyana kwenye mcheza wa raundi ya kwanza ya Klabu Bingwa barani Afrika itasubiri hadi wiki ijayo kuanza dakika hizo 180 itakapocheza na Polisi Moro katika mchezo wa Ligi Kuu Bara.
    Simba itashuka dimbani kesho kuanza kuwania nafasi hiyo ya pili wakati itakapocheza na Moro United katika Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.
    Michezo mingine itakayofanyika kesho ni pamoja na Polisi Dodoma itakapokuwa kwenye Uwanja wa Jamhuri kukipiga na Kagera, wakati Azam FC itakuwa na mtihani mzito mbele ya Mtibwa keshokutwa.
    Polisi Dodoma, Villa na Polisi Moro ndizo zinazong'ang'ana mkiani mwa ligi hiyo na nafasi zao kutishiwa na Majimaji ya Songea, Manyema FC na African Lyon ambazo zitashiriki Ligi Kuu msimu ujao.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: LIGI KUU BARA YAREJEA LEO, YANGA WIKI IJAYO... Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top