• HABARI MPYA

  Friday, March 20, 2009

  YANGA UBINGWA HUOOO, BADO POINTI MOJA


  YANGA imezidi kujihakikishia ubingwa wa Tanzania Bara baada ya kuifunga Polisi Moro bao 1-0 katika mchezo mkali wa Ligi Kuu uliofanyika kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.
  Kimsingi, Yanga imejipoza kwa timu hiyo baada ya kupata kipigo cha mabao 3-0 kutoka kwa Al Ahly ya Misri katika mfululizo wa michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, mjini Cairo wiki iliyopita.
  Aliyeipa raha Yanga jana alikuwa Boniphace Ambani aliyefunga bao la 14 msimu huu kwa mkwaju wa penalti katika dakika ya 44.
  Adhabu hiyo ilitolewa na mwamuzi baada ya Tafawa Daudi Poneka kuunawa mpira akiwa ndani ya eneo la hatari na mfungaji hakufanya ajizi kuukwamisha mpira wavuni.
  Matokeo hayo yameifanya Yanga kufikisha pointi 45 sasa inataka sare tu iweze kutangaza ubingwa wa Tanzania kwa mwaka wa pili mfululizo.
  Yanga ilianza kwa kasi mchezo huo na kufanya mashambulizi katika dakika za tatu, 28 na 42 ambapo wachezaji wake, Athumani Idd ‘Chuji’ na Ambani walikuwa wakiitesa timu hiyo.
  Wachezaji wa Polisi Moro, Nicholaus Kabipe, Imani Mapunda na Ali Moshi walilisakama lango la wapinzani wao, lakini hata hivyo bahati haikuwa yao.
  Kipindi cha pili kila timu ilishambulia kwa nguvu, lakini hata hivyo, ngome za kila upande zilijipanga vizuri na kutoruhusu nyavu kutikishwa.
  Kocha wa Polisi Moro, John Simkoko alisema kuwa wachezaji wake wamecheza vizuri, lakini hawakuwa na bahati ya ushindi. “Tunaangalia mechi zijazo zilizosalia, tutajitahidi.”
  Kocha wa Yanga Dusan Kondic aligoma kuzungumzia mchezo huo licha ya kufuatwa mara kadhaa kutakiwa kuzungumzia ushindi wake.
  Kondic amekuwa akigoma kutokana na baadhi ya waandishi (siyo wa Mwananchi) kuandika sivyo yale anayoyazungumza.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: YANGA UBINGWA HUOOO, BADO POINTI MOJA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top