• HABARI MPYA

  Ijumaa, Machi 13, 2009

  MARLON JAMES AIUA SIMBA SC

  MABAO mawili yaliyofungwa na mshambuliaji Marlon James, raia wa St. Vincent & Grenadines, jana yaliizamisha Simba 2-1 mbele ya Vancouver Whitecaps ya Canada katika mchezo uliofanyika kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
  Timu hiyo ilikuja kufanya ziara ya kimichezo hapa nchini imepata ushindi huo wa kwanza baada ya Jumatatu iliyopita kunyukwa na mabingwa wa Bara, Yanga kwa mabao 3-0.
  Vancouver iliishitua Simba kwa bao la dakika ya kwanza lililowekwa kimiani na Marlon James baada ya kumalizia krosi safi iliyopigwa kutoka wingi wa kushoto.
  Bao hilo liliichanganya Simba na kulazimika kufanya mabadiliko ya mapema baada ya kumtoa Adam Kingwande na kuingizwa Haruna Moshi 'Boban' katika dakika 15.
  Boban ambaye aliingia uwanjani hapo na kulipua shangwe za mashabiki wa timu hiyo ya Msimbazi, alilipa fadhila kwa kumalizia pasi maridadi ya Henry Joseph na kutumbukiza mpira kwenye nyavu za Vancouver katika dakika 22.
  Marlon alionekana kuwa vyema kwenye mchezo huo na kutumia makosa ya mabeki wa Simba na kufunga kirahisi dakika moja kabla ya mapumziko na kuwafanya 'watalii' hao kutoka Canada kwenda mapumziko wakiwa mbele kwa mabao hayo mawili.
  Lakini timu hiyo inayonolewa na Mzambia Patrick Phiri itabidi ijilaumu baada ya mshambuliaji wake mahiri na nyota aliyemo kwenye kikosi cha CHAN, Mussa Hassan 'Mgosi' kukosa penalti mwanzoni mwa kipindi cha pili iliyotokana na Wes Knight kuushika mpira katika eneo hilo la penalti.
  Katika kipindi hicho cha pili, Simba iliwatoa Ulimboka Mwakingwe na Deo Boniventure na kuwaingia Ally Mustapha 'Barthez' na Emeh Izuchukwu jambo ambalo halikuweza kuisaidia timu hiyo kujiokoa na kipigo.
  Vancouver nayo ilifanya mabadiliko kwa kuwatoa Tyrell Burgess, Knight na Justin Thordson na kuwaingiza Gordon Chin, Luca Bellisono na Mason Tranfford.
  Mabingwa hao wa Bara wa 2007, Simba watashuka tena dimbani kesho kumenyana na Moro United katika mchezo wa Ligi Kuu Bara iliyokuwa kwenye mapumziko kupisha michuano ya CHAN iliyomalizika hivi karibuni nchini Ivory Coast.
  Vancouver inatarajia kukamilisha ratiba yake ya kujipima na timu za hapa nchini kwa kumenyana na Taifa Stars katika mchezo wa kirafiki wa Kimataifa utakaofanyika kesho kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: MARLON JAMES AIUA SIMBA SC Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top