• HABARI MPYA

  Jumamosi, Machi 14, 2009

  ALL THE BEST YANGA


  ALL the best, hilo ni neno la Kiingereza lenye kumaanisha, kila la heri.
  Naam, bila shaka hizo ndizo salamu za Watanzania wengi, hususan mashabiki wa klabu ya Yanga ya Dar es Salaam, kwa wawakilishi hao wa nchi kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika kesho.
  Wafalme hao wa Tanzania Bara, kesho saa 1:30 usiku watakuwa wakimenyana na mabingwa watetezi wa Ligi ya Mabingwa Afrika, Al-Ahly (National) katika Uwanja wa International mjini Cairo, huo ukiwa mchezo wa awali wa Raundi ya kwanza ya michuano hiyo.
  Yanga, ambayo kikosi chake kinaundwa na wachezaji 10, waliokuwa na timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars kwenye Michuano ya Ubingwa wa Mataifa Afrika (CHAN), kesho inawania kujiwekea mazingira mazuri ya kuingia Raundi ya Pili ya michuano hiyo, hatua ambayo mara ya mwisho walifika mwaka 2007 na kutolewa na Esperance ya Tunisia kwa jumla ya mabao 3-0.
  Lakini Yanga itashuka kwenye Uwana huo, ikijua fika haina ngekewa ya kufurukuta mbele ya timu za Kaskazini mwa Afrika na mara ya mwisho ilitolewa na Al Akhdar ya Libya katika Raundi ya Kwanza, Kombe la Shirikisho Afrika kwa kufungwa mabao 2-1, baada ya sare ya 1-1 mjini Tripoli na kipigo cha 1-0, nyumbani Dar es Salaam.
  Kwa sababu hiyo, ‘Watoto wa Jangwani’, wanaonolewa na makocha watatu wa Kiserbia, chini ya Dusan Kondic (pichani kulia), anayesaidiwa na Spaso Sokolovoski na Civojnov Serdan, watakuwa pia kwenye vita ya kuhakikisha wanavunja mwiko wa kukomolewa na Waarabu.
  Kihistoria huu utakuwa ni mchezo wa tano kuzikutanisha timu hizo, Ahly ikiwa imeshinda mechi mbili nyumbani na nyingine mbili ililazimisha sare ugenini, wakati Yanga haijawahi hata mara moja kushinda mbele ya mabingwa hao mara sita Afrika.
  Kwa mara ya kwanza Yanga ilikutana na Ahly mwaka 1982, katika michuano hii, enzi hizo ikijulikana bado kama Klabu Bingwa na mchezo wa kwanza mjini Cairo wavaa jezi za njano na kijani walitandikwa mabao 5-0 na mchezo wa pili, uliokuwa wa marudiano mjini Dar es Salaam, walilazimishwa sare ya kufungana bao 1-1.
  Mara ya tatu, Yanga ilikutana na Ahly mwaka 1988 na katika mchezo wa kwanza mjini Dar es Salaam, Aprili 9 mwaka huo, timu hizo zilitoka sare ya bila kufungana na kwenye mchezo wa mwisho kuzikutanisha timu hizo, uliokuwa wa marudiano, Aprili 22, watoto wa Jangwani walitandikwa 4-0.
  Si Yanga tu, hata timu nyingine zote zilizowahi kukutana na Ahly hazikuweza kuvuka, wakiwemo Simba, Pamba FC na Majimaji ya Songea.
  Mwaka 1985, Simba iliifunga Al Ahly mabao 2-1 Uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza, katika michuano ya Kombe la Washindi, kabla ya kwenda kufungwa 2-0 mjini Cairo.
  Mwaka 1993, Al Ahly iliifunga 5-0 Pamba mjini Cairo katika Kombe la Washindi pia, kabla ya kuja kulazimisha sare ya bila kufungana mjini Mwanza, wakati mwaka 1999, Waarabu hao walianza kwa kuichapa 3-0 Majimaji ya Songea, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, kabla ya kwenda kuwaongeza 2-0 mjini Cairo.
  Na hilo ndilo lilikuwa jicho la mwisho la Watanzania kwa Ahly, ambao wanatarajiwa kuonekana tena nchini wiki mbili zijazo kwa ajili ya mchezo wa marudiano.
  Kabla ya kwenda Cairo, Yanga ilijipima nguvu na mabingwa wa Ligi Daraja la kwanza Amerika Kaskazini, Vancouver Whitecaps na kuibuka na ushindi wa mabao 3-0, siku hiyo Mkenya Mike Barasa akifunga kwa mara ya kwanza tangu amejiunga na timu hiyo, wakati mabao mengine mawili yalitiwa kimiani na chipukizi Jerry Tegete.
  Baada ya mchezo huo, Kocha Mkuu wa Yanga, Profesa Kondic, alisema kwamba ana matumaini ya kwenda kufanya vizuri Cairo, kwani aliutumia mchezo huo kutengeneza mipango yake.
  Kondic ambaye hutumia mifumo ya 4-4-2, 3-5-2 na 4-3-3, amepania kufanya vizuri ili kuweka rekodi, kwani wanamenyana na timu kubwa na nzuri.
  Katika mchezo wa leo utakaoanza majira ya saa 1: 30 usiku, huenda Kondic akaanza na kikosi hiki; Obren Curkovic, Nsajigwa Shadrack, Nurdin Bakari, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, George Owino, Geoffrey Boniphace, Mrisho Ngassa, Athumani Iddi ‘Chuji’, Jerry Tegete, Boniphace Ambani na Shamte Ally.
  Katika benchi wanaweza kuwapo Juma Kaseja, Wisdom Ndlovu, Fred Mbuna, Abdi Kassim, Amir Maftah, Kigi Makasi, Vincent Barnabas, Ben Mwalala na Mike Barasa.
  Kikosi cha Ahly kilichopo chini ya kocha, Manuel Jose bila shaka leo kitaongozwa na Mwanasoka Bora Afrika kwa mujibu wa Shirika la Utangazaji Uingereza (BBC), kiungo Mohammed Aboutrika, ambaye atakuwapo atakuwa na shughuli pevu mbele ya viungo wa Yanga, Chuji na Bonny. Wengine wanaotarajiwa kuiongoza Ahly leo ni viungo Ahmed Hassan, Ahmed Fathi na Hossam Ashour na washambuliaji Osama Hosny na Flavio Amado.
  Hakika huu utakuwa mchezo mgumu, je, Yanga itaweza kuvunja mwiko wa Ahly kuzitambia timu za Tanzania? Bila shaka hilo ni jambo la kusubiri na kuona. Mungu ibariki Yanga, ibariki Tanzania. Amina.

  MATOKEO YA JUMLA YANGA VS AL AHLY
  P W D L Ga Gf Pts
  Al Ahly 4 2 2 - 10 1 6
  Yanga 4 - 2 2 1 10 -
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: ALL THE BEST YANGA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top