• HABARI MPYA

  Alhamisi, Machi 19, 2009

  SHIRIKISHO LA SOKA BRAZIL KUSAIDIA TFF

  Rais waTFF Tenga akiwa Jamal Malinzi
  SHIRIKISHO la Soka la Brazili (CBF) limetuma mwaliko kwa wenzao wa Tanzania kwa ajili ya kuwawezesha kwenda nchini humo kujifunza mambo mbalimbali yanayohusu uendeshaji wa soka pamoja na kutafuta uwezekano wa kubadilishana mechi za kirafiki baina ya timu za nchi hizo mbili.
  Kauli hiyo ilitolewa na kocha mkuu wa Taifa Stars, Marcio Maximo jana wakati akiishukuru TFF kwa kuridhishwa na kiwango chake cha ufundishaji kwa Stars na kumwongezea muda zaidi wa mwaka mmoja.
  Akizungumza na waandishi wa habari, Maximo ambaye anaondoka leo nchini kwenda Brazil kwa mapumziko ya wiki mbili, alisema amefurahishwa na hatua iliyofikiwa na TFF ya kutambua umuhimu wake wa kuendelea kuifundisha Stars na kuahidi kuifikisha timu hiyo mbali zaidi kisoka.
  Kocha huyo ambaye amekuwa katika mzozo na baadhi ya wachezaji wake, Athuman Idd, Haruna Moshi Boban na Amir Maftah akiwatuhumu kwa utovu wa nidhamu aliwataka wachezaji wa soka wa Tanzania kuweka mbele utaifa .
  Alisema wao kama wachezaji wa taifa, wanatakiwa kutambua kuwa wao ndio wawakilishi wa nchi na wenye dhamana ya kuitangaza katika medani ya soka ndani na nje ya nchi.
  Aliongeza kuwa kwa muda wote ambao amekuwa nchini amekuwa akitambua umuhimu wa mpira wa miguu na lengo lake kwa sasa na tangu aanze kuifundisha timu hiyo ni kuona ikipata mafanikio zaidi ya kuweza kushiriki soka la kulipwa na kuiwakilisha vyema Tanzania ndani na nje.
  Aidha, Maximo alisema wakati wa likizo yake akiwa Brazil ataitumia kutafuta makocha ambao atakuja na wasifu wao na endapo watakubalika na shirikisho hilo, basi ataungana nao katika kufundisha timu ya vijana.
  "Nitajaribu kutafuta makocha wenye ujuzi ambao nitaungana nao katika kukuza vipaji kwa vijana hapa Tanzania na nitakapokuwa katika mapumziko yangu nitaandaa programu ambazo nitazitumia kwa wachezaji wangu hasa vijana kwani ndio hasa nimewalenga na ambao wengi ndio wataunda kikosi cha timu ya taifa,"alisema.  FILAMU MACHI 20 NEW WORLD CINEMA


  UBALOZI wa Mataifa ya Asia nchini umeandaa onyesho la filamu litakalofanyika Machi 20 hadi 27 kwenye Ukumbi wa New World Cinema Mwenge.
  Onyesho hilo litaonyesha kazi za filamu kutoka nchi mbalimbali ikiwemo Iran, China, Korea Kusini, India, Indonesia, Vietnam na Japan.
  Mratibu wa onyesho hilo, Saeed Omid alisema lengo la kuanda onyesho hilo hapa nchini ni kujenga utamaduni na umoja baina ya nchi hizi pamoja kuleta ushirikiano katika michezo.
  "Lengo hasa la kuandaa onyesho hilli ni kujenga utamaduni baina ya Tanzania na nchi hizi pamoja na kujifunza mambo mbalimbali yanayohusiana na michezo ya kuigiza ili kuleta mshikamano na umoja," alisema Saeed.
  Alisema siku ya kwanza wataonyesha filamu ijulikanayo kwa jina la God is near kutoka Iran, Together kutoka China na The Big Swindle kutoka Korea Kusini.
  Nyingine ni Taare Zameen Par India, Ayat Ayat Cinta Indonesia White Silk Dress Vietnam na Death Note kutoka Japan.  DROO YA NMB, 500 WAULA  WATU 500 kutoka maeneo mbalimbali nchini wameshinda zawadi mbalimbali katika droo ya Weka Amana Ushinde inayoendeshwa na Benki ya NMB.
  Meneja Mwandamizi wa Masoko na Mawasiliano wa NMB, Imani Kajula aliwaambia waandishi wa habari jana kuwa mpango mzima ulianza mapema mwaka huu lengo likiwa kuwapeleka mashabiki Ivory Coast katika fainali za CHAN.
  “Tulifanya droo kubwa ya kwanza na washindi wawili walikwenda Ivory Coast na kuangalia mechi ya Taifa Stars bure.
  “Droo hii ya sasa ni kwamba washindi 200 wanapata jezi za Taifa Stara wakati washindi wengine 150 weanapata miavuli na idadi nyingine kama hiyo wanapata fulana,” alisema Kajula.
  Alisema kuwa droo ya tatu, itawakutanisha washindi watatu watakaojiongezea amana ya Sh300,000 na washindi 100 kushinda kofia na wengine 150 fulana.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: SHIRIKISHO LA SOKA BRAZIL KUSAIDIA TFF Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top