• HABARI MPYA

  Saturday, March 14, 2009

  SIMBA DIMBANI KESHOKUTWA, WASSO AKUBALI YAISHE KWA JABU


  WAKATI Simba kesho inatarajiwa kuanza tena kampeni zake za kuwania nafasi ya pili katika Ligi Kuu ya Vodacom, Tanzania Bara, beki wa kushoto wa timu hiyo, Ramadhan Wasso (aliyeruka juu pichani kulia), amesema hana kinyongo na Juma Jabu aliyempora namba hivi sasa.
  Simba kesho itamenyana na Moro United, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, mchezo ambao italazimika kupigana kiume, ili ishinde na kujitengenezea mazingira ya kupata nafasi ya pili, inayowaniwa pia na Kagera Sugar ya Bukoba, JKT Ruvu, Prisons, Toto na Mtibwa Sugar. Simba ina pointi 24 sawa na JKT yenye mechi moja zaidi ya kucheza, Prisons 22 na Toto 21.
  Akizungumza na DIMBA, Wasso alisema: "Hapa tupo kama timu, mimi sina kinyongo na wala sijisikii vibaya kwa kuwa hiyo ndiyo soka. Nimecheza muda mrefu na tupo pale kwa maslahi ya Simba. Huwezi kucheza mechi zote, muhimu timu ishinde, siyo nani kacheza," alisema.
  Mrundi huyo aliyetua Simba mwaka 2002 na kuwa chaguo la kwanza kabla ya kuhamia kwa watani wa jadi, Yanga mwaka 2005, tangu amerejea mwaka 2007 ameshindwa kuendeleza cheche zake kiasi cha kuwashawishi makocha kumrejeshea mikoba yake.
  "Kiwango changu hakijashuka, ni suala la kupeana nafasi ya kucheza. Kocha anaona huyu anafaa mchezo huu anacheza, siku nyingine ataona mimi ninafaa nitacheza. Ukianza kuona ni lazima ucheze wewe, utaleta mgawanyiko katika timu, siko peke yangu ambaye sichezi, lakini wote tuna furaha," alisema.

  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: SIMBA DIMBANI KESHOKUTWA, WASSO AKUBALI YAISHE KWA JABU Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top