• HABARI MPYA

  Jumanne, Machi 24, 2009

  WAARABU WAANZA VITUKO MAPEMA


  MECHI YA MARUDIANO LIGI YA MABINGWA...
  Ahly waanza
  visa mapema
  .Waikwepa hoteli ya wenyeji, wajilipia Movenpick

  WAPINZANI wa Yanga Raundi ya Kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika, Al Ahly ya Misri imegoma kufikia katika hoteli ya Durban ambayo wameandaliwa na wenyeji wao hao, hivyo kuamua kujikodia wenyewe hoteli nyingine, Movenpick.
  Habari za kiuchunguzi ambazo DIMBA imezipata, Al Ahly inayonolewa na Mreno, Manuel Jose de Silva, itafikia katika hoteli hiyo ambayo watajigharimia wenyewe.
  Ofisa mmoja wa Movenpick ambaye hakutaka kutajwa jina lake, aliiambia DIMBA kwamba wameomba nafasi kwenye hoteli hiyo kwa siku tatu kuanzia Aprili 3, mwaka huu.
  Imekuwa ni kawaida kwa klabu za Misri, haswa Al Ahly kuwa na vitimbi zinapotua nchini na mara ya mwisho, walipokuja kumenyana na Majimaji mwaka 1999, katika michuano kama hii, waligoma kufikia kwenye hoteli ya Embassy na badala yake kwenda kujilipia wenyewe New Africa.
  Enzi hizo ikiwa chini ya Kocha Mjerumani, Rainer Zobel alisema kwamba hawezi kuishi Embassy Hotel kwa sababu pachafu na maji yake si mazuri, wachezaji wake wakioga watakuwa weusi, akiomtolea mfano mwandishi mmoja wa habari wa kike.
  “Mnataka tukae hapa tuwe weusi kama wewe,”alisema kocha akimtolea mfano mwandishi huyo wa kike, aliyekerwa na kauli hizo za kibaguzi za Mjerumani huyo aliyetimuliwa msimu huo huo Al Ahly.
  Kauli hizo za kocha huyo zilichukuliwa kama za kibaguzi na siku ya mchezo huo, ambao timu yake iliibuka na ushindi wa 3-0 alizomewa mno na mashabiki Uwanja wa Taifa, (sasa Uhuru) mjini Dar es Salaam.
  Yanga iliyofungwa 3-0 na Al Ahly wiki iliyopita, inatakiwa kushinda 4-0 ili isonge mbele, au ikishinda 3-0, mchezo utahamia kwenye mikwaju ya penalti, kuamua mshindi wa jumla.
  Mchezo wa marudiano baina ya miamba hiyo, utafanyika Aprili 4, mwaka huu mjini Dar es Salaam. Huo utakuwa mchezo wa sita kuzikutanisha timu hizo kihistoria, mitano ya awali Yanga ilifungwa mara tatu na kutoka sare mara mbili.


  Mgosi aangua kilio

  .Asema kuteuliwa kikosini CHAN kumemponza
  .Adai anakung’utwa kama ‘mwizi’ uwanjani
  .Asema ameshindwa kuvumilia, yeye si chuma

  MSHAMBULIAJI wa Simba ya Dar es Salaam, Mussa Hassan Mgosi, amesema kuteuliwa kwenye kikosi cha nyota wa Michuano ya Ubingwa wa Mataifa ya Afrika (CHAN) kumemponza, kwani hivi sasa anakamiwa na kuchezewa rafu mbaya kwenye Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania bara, inayoendelea nchini.
  “Ebwana nashindwa kuelewa, haya mambo ya CHAN yananifanya nikamiwe, nachezewa rafu ile mbaya, napigwa hadi nakosa raha uwanjani, cha ajabu na marefa wanashindwa kunilinda.
  Wachezaji wananichezea kwa wivu, sasa mimi siyo chuma, we kipa kaja kanipiga makusudi, refa kaona hajachukua hatua yoyote, nikashindwa kujizuia na mimi nikalipa,”alilalamika Mgosi.
  Hata hivyo, Mgosi alisema amejuta kwa nini alishindwa kuzuia hasira zake, kwani kitendo alichokifanya kimeigharimu pia na timu yake.
  “Kwa kweli nawaomba radhi wapenzi na mashabiki wa timu yangu, najua kosa hili limewaumiza, lakini mimi ni binadamu pia, hawana budi kunisamehe,”alisema Mgosi.
  Mgosi yuko hatarini kufungiwa na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kutokana na kutolewa nje kwa kadi nyekundu, baada ya kupigana na kipa wa Mtibwa Sugar, Shaaban Kado katika mechi baina ya timu hizo Uwanja wa Jamhuri, Morogoro Jumapili iliyopita.
  Kwenye mchezo huo wa Ligi Kuu ambao Simba ililala 1-0, Mgosi alikuwa kwenye wakati mgumu kutokana na kutandikwa ‘viatu’ na wachezaji wa Mtibwa waliotaka kuonekana wamemdhibiti nyota wa CHAN.

  Phiri ammezea
  mate Cannavaro

  KOCHA Mkuu wa Simba, Mzambia Patrick Phiri amesema anatamani kupata beki mahiri anayejituma kama alivyo beki wa kati wa watani wao Yanga Nadir Haroub ‘Cannavaro’.
  Akizungumza na DIMBA jumanne ya wiki iliyopita katika Hotel ya Mtanzania iliyopo Sinza jijini Dar es Salaam ambako anaishi, kocha huyo wa zamani wa timu ya taifa ya Zambia, alisema anatamani kupata beki ambaye anajituma uwanjani kama Canavaro ili timu yake iweze kufanya vyema msimu ujao wa Ligi.
  Alisema hiyo inatokana na hali mbaya ya kikosi chake, ambacho mabeki wameshindwa kuelewana kwani wanategeana katika kuwadhibiti wapinzani wao wakati wa mchezo.
  Akimsifu beki huyo, alisema ana vitu binafsi ndani ya moyo na akili yake kitu ambacho kinamsaidia kuwasumbua washambuliaji mbalimbali wenye historia kubwa.
  “Mimi ni kocha, naangalia mpira na kusoma mchezo kila siku, najua faida na hasara ya Canavaro, katika timu yangu kama nitapata beki kama huyu najua nitakuwa na furaha kubwa kwani ni mchezaji wa aina yake. Nitaongea vizuri na uongozi wangu ili katika usajili niweze kutafuta beki wa aina yake,”alisema.
  Alisema anafurahishwa naye kwani anaweza kucheza na kuongea na wenzake kila wakati na inapobidi kunyamaza anaweza kucheza hata katika sehemu ambayo kwake ilikuwa ni ngumu kucheza.
  Tatizo kubwa la wachezaji wake wa safu ya ulinzi, alisema ni kukosa kujiamini, kitu ambacho amekuwa akikipigia sana kelele lakini mabadiliko ni madogo.
  “Sina mashaka na safu yangu ya ushambuliaji, nina wachezaji wazuri tena wanaoweza kupasua ngome wakati wowote bila hofu, lakini kikwazo ni kidogo tu kama nitapata huyo beki msimu unaokuja nitawapa ubingwa Simba, na nina hakika nitapata ili kurejesha ubingwa kama ilivyokuwa miaka ya nyuma,”alisema.
  Alimkumbuka mlinzi Victor Costa na kusema ni pengo kubwa kwa Simba kwani alikuwa ni beki mwenye utulivu na mwenye kutumia akili nyingi akiwa katika mchezo.
  “Enzi naifundisha Simba miaka ya nyuma kulikuwa na mabeki kama Costa na Said Kokoo, ambaye sasa namwona yupo Moro United yaani wasi wasi nyuma ilikuwa hakuna lakini sasa hivi vijana wangu kwa kweli hawana uelewano ndio maana kuna mechi tunapoteza kwa uzembe tu,”alisema.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: WAARABU WAANZA VITUKO MAPEMA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top