• HABARI MPYA

  Friday, March 20, 2009

  DALALI APIGA MBIU YA UMOJA MSIMBAZI


  UONGOZI wa klabu ya soka ya Simba, umewataka wapenzi na mashabiki wao kuungana ili timu yao iweze kushinda michezo iliyosalia na hatimaye wanyakue nafasi ya pili.
  Tangu ilipotolewa katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika na Enyimba ya Nigeria mwaka juzi, Simba haijashiriki michuano ya Ligi ya Mabingwa wala Kombe la Shirikisho.
  Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Simba, Hassan Dalali (pichani kulia mwenye mvi), alisema bila kuungana pamoja, klabu hiyo itakuwa ndoto kunyakua nafasi hiyo inayowaniwa pia na Mtibwa Sugar, Kagera Sugar na Prisons ya mjini Mbeya.
  Dalali alisema kwamba kuna baadhi ya wanachama na mashabiki wasiokuwa na mapenzi mema na klabu hiyo, wameanza kuleta chokochoko kwa kitendo chao cha kutukana viongozi katika mechi kati ya Simba na Moro United.
  Alisema hatua hiyo, ni mbaya kwa timu hiyo, baada ya kushindwa kushiriki michuano ya Kimataifa, takribani miaka miwili sasa na kutia aibu kwenye soka kupitia klabu.
  “Ndio timu yetu ipo katika mazingira mazuri ya kushika nafasi ya pili katika msimamo wa ligi kama itashinda mechi zake zilizosalia, lakini utulivu na mshikamano unaweza kufanikisha hilo,” alisema.
  “Vurugu za hapa na pale, hususan za mashabiki wachache zinaweza kuwa kikwazo cha kutimiza malengo hayo ya kucheza Kombe la Shirikisho baadaye mwakani.”
  Mwishoni mwa wiki hii, klabu hiyo ya Simba, inatarajiwa kuvaana na wakata miwa wa Mtibwa Sugar, mchezo utakaochezwa kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro.
  Endapo itashinda mechi hiyo, klabu hiyo itazidi kujiwekea mazingira mazuri katika ligi hiyo inayoelekea ukingoni.


  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  1 comments:

  Item Reviewed: DALALI APIGA MBIU YA UMOJA MSIMBAZI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top