• HABARI MPYA

  Ijumaa, Machi 20, 2009

  SERIKALI YAIPA TANO MISS TANZANIA

  Miss Tanzania 2008 mwaka jana, Nasreem Karim katikati akiwa na washindi wake wa pili Sylvia Mashuda na Pendo Lyser wa tatu.


  NAIBU Waziri wa Maliasili na Utalii, Ezekiel Maige, amesema kwamba ameitikia wito wa kuwa mgeni rasmi katika semina ya Mawakala wa Miss Tanzania, kutokana na kufurahishwa na kauli mbiu ya mwaka huu ya shindano hilo, inayohusu kukuza utalii wa ndani.
  Akizungumza kwenye ufunguzi wa semina hiyo, hoteli ya Regency Park mjini Dar es Salaam, Maige alisema kuwa kitu kingine kilichompa msukumo kuhudhuria ni jinsi Kamati ya Miss Tanzania inavyofanya mambo yake kwa uhakika, kwani haijawahi kusikia matatizo makubwa kama ilivyo kwa baadhi ya waandaaji wengine wa mashindano ya urembo.
  “Hii kauli mbiu inanigusa moja kwa moja, ndiyo maana nilipoalikwa sikusita kufika hapa, hasa ikizingatiwa kuwa Serikali hutegemea sana pato linalotokana na utalii,” alisema Maige.
  Naye Meneja Udhamini na Mawasiliano wa Kampuni ya Vodacom Tanzania, ambao ndio wadhamini wakuu wa shindano hilo, George Rwehumbiza, alisema kuwa mafanikio ya miaka mitatu ambayo kampuni hiyo imeyapata ndiyo yaliyochochea kusaini mkataba mwingine wa miaka miwili wa udhamini wa shindano la Miss Tanzania.
  Awali ya hapo, Kampuni ya Lino Agency, inayoandaa shindano hilo, ilisema haitaki kusikia kuwa kuna mrembo atakayeshinda kwa kutoa hongo au rushwa ya ngono.
  Akizungumza kwenye semina hiyo, Mkurugenzi wa kampuni hiyo, Hashim Lundenga, alisema kwamba mawakala wanaoandaa shindano hilo ngazi za mikoa wanapaswa kuwa makini na hilo.
  Alisema kuwa lengo la kampuni yake ni kupata warembo bora na wenye sifa ya kushiriki shindano la dunia, kama ilivyokuwa mwaka 2005, ambapo mrembo Nancy Sumary alikuwa mmoja wa warembo sita bora duniani.
  Kauli mbiu ya mwaka huu ni kukuza utalii wa ndani, ambako amedai kuwa utalii wa ndani unaweza kuongeza pato la Taifa kama utatangazwa vyema Tanzania.
  Vadacom imewataka mawakala kutafuta warembo wenye vigezo, kwani hivi sasa shindano hilo linaangaliwa na mashabiki wa fani ya urembo zaidi ya 10,000, achilia mbali ambao huangalia kupitia Televisheni.
  Taji la Vadacom Miss Tanzania mwaka 2008 linashikiliwa na Nasreem Karim, kutoka Mwanza.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: SERIKALI YAIPA TANO MISS TANZANIA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top