• HABARI MPYA

  Ijumaa, Machi 27, 2009

  Watanzania wa ughaibuni wampongeza Kikwete kwa mafanikio ya Stars


  WATANZANIA waishio nchini Comoro wamempongeza Rais Jakaya Kikwete (pichani juu) kwa kuiweka nchi katika kiwango kizuri katika michezo hasa soka jambo linalowafanya watembee kifua mbele mitaa ya nchi hiyo. Pia wamemwomba Rais Kikwete kuhakikisha kasi hiyo ya michezo nchini inakua na haishii katika soka tu bali katika michezo mingine kama mpira wa kikapu, mikono na riadha. “Mheshimiwa Rais, tunafarijika sana na namna unavyoendesha nchi kwa kuweka kipaumbele katika michezo pia, tulikuwa nyuma sana katika kipindi cha nyuma lakini sasa tunaweza kusema sisi ni Watanzania na kwenye soka tumo,” alisema Manamvua Ngocho aliyesoma risala kwa niaba ya wenzake katika mkutano wao na Rais Kikwete juzi jioni kwenye Hoteli ya Itsandra Beach mjini hapa. Huku akishangiliwa na Watanzania wenzake mara alipogusa michezo, Ngocho alisema imekuwa ni furaha kwao kusikia jinsi timu ya taifa (Taifa Stars) inavyofanya vizuri katika soka la Afrika na wanategemea kidunia siku si nyingi, Tanzania itavunja rekodi. Akitolea mfano mechi kati ya Taifa Stars na Zambia ya michuano ya Mataifa Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN) iliyofanyika nchini Ivory Coast hivi karibuni na kutoka sare ya bao 1-1 na ile ya Yanga iliyoichapa timu ya Etoile d’or ya Comoro mabao 6-0, Ngocho alisema hizo ni baadhi ya mechi zilizoonyesha Tanzania ipo pazuri kisoka. Kwa upande wake, Rais Kikwete alisema ni kweli mabadiliko ya soka nchini yamefanyika na kiwango kimepanda jambo aliloahidi sasa kuwa kilichofanyika katika soka kitafanyika pia katika riadha. “Tunaelekeza nguvu pia katika riadha, kama mnakumbuka wengi miaka ya nyuma mliwasikia kimataifa majina ya akina Bayi (Filbert), Suleiman (Nyambui) na wengine wengi, tunataka majina kama hayo tena yarejee nchini na tumeanza juhudi,” alisema Kikwete. Serikali ya Rais Kikwete ndiyo inamlipa mshahara Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Mbrazil, Marcio Maximo, aliyekuja nchini Agosti mwaka 2006. Rais Kikwete anatarajia kurejea nchini leo baada ya kumaliza ziara yake ya kikazi ya siku tatu nchini hapa.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: Watanzania wa ughaibuni wampongeza Kikwete kwa mafanikio ya Stars Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top