• HABARI MPYA

  Jumamosi, Machi 07, 2009

  SIMBA YAPATA NEW KISIGA


  KLABU ya soka ya Simba ya Dar es Salaam, inawawania wachezaji wawili wanaong’ara kwenye Ligi Daraja la Kwanza, Tanzania Bara, Mbwana Samatta wa African Lyon ya Temeke na Juma Mpola wa Majimaji ya Songea.
  Mjumbe mmoja wa Kamati ya Usajili ya Simba, ambaye hakupenda kutajwa jina lake gazetini, alisema kwamba kocha Patrick Phiri amevutiwa na uwezo wa wachezaji hao na amewaingiza kwenye hesabu zake za msimu ujao.
  Alisema wachezaji hao wameonyesha kiwango kizuri katika Ligi Daraja la Kwanza, inayoendelea kwenye Uwanja wa Uhuru, zamani Taifa mjini Dar es Salaam na wanaamini kabisa wataisaidia timu hiyo msimu ujao.
  "Huyu Juma Mpola ni New Kisiga, mtoto anaujua sana, yaani we acha tu, sisi tunasema kuanzia mwakani ndio itaanza kuonekana Simba ya ukweli, kuna makosa tulifanya hapa katikati, lakini tumeshajifunza na sasa tunafanya kweli,"alisema.
  Baada ya kwenda mrama kwenye mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara ikiwa chini ya Mbulgaria, Krasmir Bezinski, Simba ilimtimua kocha huyo na kumrejesha kocha wake wa zamani, Patrick Phiri kutoka Zambia ambaye yupo kwenye harakati za kuhakikisha angalau timu hiyo inashika nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi. Simba inashika nafasi ya tatu kwenye ligi hiyo, ikiwa na pointi 24, Kagera Sugar inayoshika nafasi ya pili ina pointi 26.
  Tayari watani wao wa jadi, Yanga wameukaribia ubingwa wa ligi hiyo, wakiwa wana pointi 42 na wanahitaji kushinda mechi moja tu kujihakikishia ubingwa huo, kwa mara ya pili mfululizo.
  Baada ya mapumziko ya tangu mwanzoni mwa Februari, Ligi Kuu inatarajiwa kuendelea Machi 13, mwaka huu wakati JKT Ruvu inayowania pamoja na Simba nafasi ya pili, itakapomenyana na Villa Squad inayopiga kasia kujiepusha na wimbi la kushuka daraja na siku inayofuata Simba itakuwa mwenyeji wa Moro United, Polisi Dodoma mwenyeji wa Kagera Sugar.
  Machi 15, Azam itaikaribisha Mtibwa Sugar Uwanja wa Uhuru, zamani Taifa mjini Dar es Salaam, wakati ikirejea kutoka Misri, Yanga itakuwa mwenyeji wa Polisi Morogoro Machi 19, siku ambayo wanaweza kutangaza ubingwa na kulicheza rhumba kwa furaha tele. Toto nayo siku hiyo itakuwa ikimenyana na Prisons mjini Mwanza.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: SIMBA YAPATA NEW KISIGA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top