• HABARI MPYA

    Saturday, March 14, 2009

    NJOONI MUWAONE NYOTA WAPYA- MAXIMO


    KOCHA mkuu wa Taifa Stars, Marcio Maximo ameeleza kuwa ni zamu ya Watanzania kuona mabadiliko katika soka kwa kuiangalia timu mpya ya taifa.
    Alisema hayo juzi wakati akiwakaribisha kambini wachezaji wa Simba waliorejea kutoka kikosi chao kilichocheza juzi na kuchapwa mabao 2-1 na Vancouver Whitecaps kutoka Amerika ya Kaskazini.
    Aisema mechi ya leo dhidi ya wageni hao ni mahsusi kwa kuwaonyesha Watanzania jinsi timu yao ilivyo katika mabadiliko kimpira pamoja na kuwa na vijana wengi ambao watafanya vizuri pamoja na kuwa timu watakayocheza nayo ni nzuri.
    Akizungumza na Mwananchi, Maximo alisema kwa kuanza na vijana hao katika kikosi chake anajivunia kwani ana hakika hao ndio watakuwa wachezaji ambao ni vipaji vya kweli kwani asilimia nane ya wachezaji hao ni vijana wenye umri mdogo wa miaka17 na 20 na wanatoka katika timu ambazo hazina majina makubwa.
    "Kwa kuwa bado vijana hawa hawajazoea kucheza mechi za kimataifa ninatumia muda mwingi kuongea nao kuwapa ushauri na kuwafanya waelewe kiwango walichokuwa nacho sasa ni cha kimataifa na mchezaji wa kimataifa anatakiwa kuwaje.
    Endapo mchezaji atafuata maagizo atakayopewa bila shaka ndiye mchezaji bora ndio maana nimeamua kuwaeleza waachane na uzoefu, Wakubali kufundishika na makosa kama watakosea hii itatusaidia kuinua viwango vya wachezaji wetu pamoja heshima wanapokuwa uwanjani,"alisema.
    Aliongeza kuwa pamoja na kuwa mchezaji mwenyewe kuonyesha bidii, lakini bado atakuwa akihitaji kujengeka kimwili pia kwa kuwapatia chakula bora pamoja na mazoezi mengi mchanganyiko.
    Taifa Stars leo itajitupa uwanjani kupambana na timu ya Vancouver katika mchezo wao wa kirafiki ambapo timu hiyo kutoka Marekani ikiwa imefungwa mechi yao ya kwanza dhidi ya Yanga kwa mabao 3-0 na kushinda mechi yao dhidi ya Simba kwa 2-1.
    Maximo anategemea kuanza mechi hiyo huku akiwatumia wachezaji wake chipkizi katika kikosi cha kwanza kama vile, Razak Khalifan, Khalid Haji, Furaha Yahya, Haji Ally,Ahmed Hassan, Zahoro Pazi na Mwinyi Kazimoto .
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: NJOONI MUWAONE NYOTA WAPYA- MAXIMO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top