• HABARI MPYA

  Jumanne, Machi 17, 2009

  MAXIMO MWAKA MMOJA ZAIDI TAIFA STARS


  KOCHA wa Taifa Stars, Marcio Maximo (pichani) amekubali na kusaini mkataba mpya wa mwaka mmoja zaidi wa kuinoa timu hiyo.
  Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Leodegar Tenga alisema jana kuwa alikuwa na mazungumzo na Maximo na alikubali kuingia mkataba wa mwaka mmoja zaidi baada ya ule wa awali unaomalizika Julai mwaka huu.
  Tenga alisema kuwa kuwa kilichowavuta hata kuongeza mkataba na kocha huyo ni kutokana na kuonyesha kiwango cha timu hiyo tangu alipoichukua miaka mitatu iliyopita.
  Baadhi ya wadau wa soka wamekuwa wakitaka TFF kusaka kocha mwingine kutoka nchi kama Ufaransa, Jamhuri ya Czech, Serbia, Ubelgiji ambao viwango vinaonekana kuwa vya juu.
  '' Lengo letu sisi TFF na Tanzania kwa jumla tangu mwanzo tulikuwa tunataka tukae na Maximo kwa miaka minne na tulikuwa tunaamini kwa muda huo atakuwa ametusaidia kuiweka timu yetu katika hali nzuri na mafanikio makubwa,'' alisema Tenga.
  Alisema kwa zaidi ya miaka 29 iliyopita kwa mara ya kwanza timu hiyo haijawahi kucheza fainali zozote na kocha huyo kwa mwaka huu katupeleka huko.
  Rais huyo alisema pia Maximo katika kipindi chake chote hicho, Stars imecheza mechi 47, imeshinda mechi 21 sare 14 kufungwa 12 na hiyo siyo hatua ndogo ukizingatia timu ya Taifa Stars bado changa.
  Aliwashukuru wadau wote wa michezo walioifikisha timu hiyo hapo ilipoakiwemo Rais Jakaya Kikwete, mawaziri,wabunge na kuahidi kutafuta wadhamini zaidi.
  Alisema wamefurahishwa na uamuzi huo na hasa kukubali kwa Maximo kuongeza mkataba mwingine wa mwaka mmoja kwa kuwa ni kocha ambaye ana nia ya kukuza soka nchini kwetu hasa kwa kutaka kuwainua zaidi vijana.
  Rais huyo wa TFF alisema matumaini ya watu wengi saidi ni kuona Stars safari ijayo inacheza fainali za CHAN mwaka 2011 nchini Sudan na mwaka 2014 inashiriki Kombe la Dunia nchini zitakazochezwa
  Brazil.
  Alisema lengo lao ni kuhakikisha wanakaa pamoja na watahakikisha kila tarehe ya kalenda ya Fifa (Shirikisho la Soka la Kimataifa) ya kuwa mechi ya kirafiki, timu hiyo nayo inacheza mechi ili kujiweka fiti.
  Kuhusu wasaidizi wa Maximo, Tenga alisema nafasi ya Marcus Tinocco na Itamar Amorin, zitajazwa na makocha atakaowatafuta Maximo.
  Katika hatua nyingine, Tenga alisema ameunda kamati ya kusimamia makusanyo ya fedha za wahisani kwa ajili ya timu hiyo.
  Kamati hiyo inaundwa na Dk Ramadhan Dau, Shabir Abji, Meja Jenerali Mstaafu Said Kalembo, Mussa Azzan Zungu (Mbunge) , Jackson Songera na Henry Tandau .
  Wale watakaoshughulika na uchapishaji tiketi ni Kamanda wa Polisi, Kanda Maalum, Suleiman Kova, Mohammed Chiko (ofisa mwandamizi wa polisi), Kanali Idd Kipingu, Yusuph Njoa, Deo Lijato na ofisa mmoja kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru).
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: MAXIMO MWAKA MMOJA ZAIDI TAIFA STARS Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top