• HABARI MPYA

    Monday, March 16, 2009

    YANGA HOI TENA AL AHLY


    MABAO mawili ya Mohamed Barakat na moja la Flavio Amado, jana yaliifanya Yanga ilale 3-0 kwenye Uwanja nternational mjini Cairo mbele ya wenyeji, Al Ahly katika mchezo wa awali wa Raundi ya kwanza ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
    Barakat alikuwa mwiba mchungu kwa ngome ya Yanga kwa kuifungia Al Ahly mabao mawili pamoja na lile la mapema zaidi katika sekunde ya 44 mwanzoni mwa mchezo.
    Mabingwa hao watetezi aliouanza mchezo kwa kasi na kutawala vema sehemu ya kiungo walipata bao hilo la mapema kwa mshambuliaji wa kimataifa wa Misri, Mohamed Barakat akipokea pasi ya Muhtaz Ino na kupachika mpira wavuni.
    Kuingia kwa bao hilo kuliamsha ari ya Yanga ilijibu shambulizi katika dakika ya pili kupitia mshambuliaji wake Bonifase Ambani aliyekosa bao la wazi kwakushindwa kuunganisha pasi nzuri ya Mrisho Ngasa.
    Baada ya kosa kosa hiyo mabingwa hao wa Afrika, Al Ahly waliutawala mchezo kwa zaidi ya dakika 16 Yanga ilifanikiwa kufika langoni kwa Wamisri hao mara moja, huku mashambulizi yao yote yakipitia upande wa kulia na kumpa wakati ngumu beki Amri Maftah.
    Kipa Obren Cirkovick ilimbidi kufanya kazi ya ziada kuokoa mpira wa kichwa uliopigwa na Ahmad Bilal katika dakika ya 12.
    Mshambuliaji wa kimataifa wa Angola, Flavio alitumia vizuri uzembe wa kipa Obren aliyeshindwa kuokoa kwa umakini krosi ya Barakat na kumkuta mfungaji dakika ya 20 kufanya matokeo kuwa 2-0 hadi mapumziko.
    Al Ahly wakionekana wameisoma vizuri Yanga na kutumia udhaifu wa beki za pembeni walipata bao la tatu lilofungwa tena na Mohamed Barakat aliyeunganisha vizuri krosi ya Ahmad Faraj katika dakika ya 53.
    Baada ya kuona hali inazidi kuwa mbaya kocha Dustan Kondic alifanya mabadiliko kwa kumtoa Godfrey Bonny, Ben Mwalala na Mrisho Ngassa na nafasi zao kuchukuliwa na Geogre Owino, Jerry Tegete na Mike Baraza.
    Mabadiliko hayo yalirudisha uhai wa Yanga na kufanya mashambulizi mengi na kushuhudia mashuti ya Boniphace Ambani na Nurdin Bakari yakigonga mwamba katika dakika 79 na 80, huku Mike Baraza akikosa bao yeye na kipa kwa shuti lake kupaa juu.
    Ili kuingia Raundi ya Pili ya michuano hiyo, hatua ambayo mara ya mwisho walifika mwaka 2007 na kutolewa na Esperance ya Tunisia kwa jumla ya mabao 3-0, Yanga sasa inahitaji kushinda 4-0 kwenye mchezo wa marudiano wiki mbili zijazo mjini Dar es Salaam.
    Aidha, kipigo hicho kimeifanya Yanga iendeleze unyonge wake kwa timu za Kaskazini mwa Afrika na mara ya mwisho ilitolewa na Al Akhdar ya Libya katika Raundi ya Kwanza, Kombe la Shirikisho Afrika kwa kufungwa mabao 2-1, baada ya sare ya 1-1 mjini Tripoli na kipigo cha 1-0, nyumbani Dar es Salaam.
    Huu ulikuwa mchezo wa tano kuikutanisha Yanga inayonolewa na makocha watatu wa Kiserbia, chini ya Dusan Kondic (pichani kulia), anayesaidiwa na Spaso Sokolovoski na Civojnov Serdan na Al Ahly.
    Katika mechi hizo, Ahly sasa imeshinda mechi tatu nyumbani na nyingine mbili ililazimisha sare ugenini, wakati Yanga haijawahi hata mara moja kushinda mbele ya mabingwa hao mara sita Afrika.
    Kwa mara ya kwanza Yanga ilikutana na Ahly mwaka 1982, katika michuano hii, enzi hizo ikijulikana bado kama Klabu Bingwa na mchezo wa kwanza mjini Cairo wavaa jezi za njano na kijani walitandikwa mabao 5-0 na mchezo wa pili, uliokuwa wa marudiano mjini Dar es Salaam, walilazimishwa sare ya kufungana bao 1-1.
    Mara ya tatu, Yanga ilikutana na Ahly mwaka 1988 na katika mchezo wa kwanza mjini Dar es Salaam, Aprili 9 mwaka huo, timu hizo zilitoka sare ya bila kufungana na kwenye mchezo wa mwisho kuzikutanisha timu hizo, uliokuwa wa marudiano, Aprili 22, watoto wa Jangwani walitandikwa 4-0.
    Si Yanga tu, hata timu nyingine zote zilizowahi kukutana na Ahly hazikuweza kuvuka, wakiwemo Simba, Pamba FC na Majimaji ya Songea.Mwaka 1985, Simba iliifunga Al Ahly mabao 2-1 Uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza, katika michuano ya Kombe la Washindi, kabla ya kwenda kufungwa 2-0 mjini Cairo.Mwaka 1993, Al Ahly iliifunga 5-0 Pamba mjini Cairo katika Kombe la Washindi pia, kabla ya kuja kulazimisha sare ya bila kufungana mjini Mwanza, wakati mwaka 1999, Waarabu hao walianza kwa kuichapa 3-0 Majimaji ya Songea, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, kabla ya kwenda kuwaongeza 2-0 mjini Cairo.Na hilo ndilo lilikuwa jicho la mwisho la Watanzania kwa Ahly, ambao wanatarajiwa kuonekana tena nchini wiki mbili zijazo kwa ajili ya mchezo wa marudiano.

    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: YANGA HOI TENA AL AHLY Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top