• HABARI MPYA

  Jumamosi, Machi 14, 2009

  MO DEWJI ATAMBA KUFANYA MAKUBWA AFRICAN LYON  MMILIKI wa klabu ya African Lyon iliyopanda Ligi Kuu, Mohammed Gulam Dewji (pichani kulia), ameahidi makubwa kwa timu hiyo yenye makazi yake wilaya ya Temeke, jijini.
  African Lyon, zamani ilikuwa inajulikana kwa jina la Mbagala Market, kabla ya kununuliwa.
  Dewji, maarufu kwa jina la Mo, jana aliandaa sherehe fupi ya kuwapongeza wachezaji wa timu hiyo katika hoteli ya Coliseum, iliyopo Masaki, jijini.
  Dewji pia alitangaza mikakati ya kuiendesha klabu hiyo kwa njia za kisasa, ikiwamo kujenga hosteli na viwanja vya soka katika eneo la Mbagala.
  “Nimeshanunua eneo na sasa hivi nakwenda kulitazama. Nataka tujenge uwanja mmoja mkubwa na vingine vidogo, pia nataka nijenge hosteli ya kisasa kwa ajili ya wachezaji,” alisema Dewji
  “Lakini pia nataka kuongeza utaalamu wa watu wa benchi la ufundi ambalo limeiwezesha timu hii kupanda daraja,” aliongeza Dewji
  Katika sherehe hiyo, Dewji aliwatunukia tuzo mbalimbali wachezaji wa African Lyon ambao waliibuka kuwa vinara katika nidhamu, ubora wa uwanjani, uhamasishaji pamoja na ya ufungaji bora, tuzo ambayo ilikwenda kwa mshambuliaji chipukizi, Mbwana Samatta.
  Samatta alikuwa gumzo katika michuano ya Ligi Daraja la kwanza iliyomalizika hivi karibuni, baada ya kufunga mabao 13 na hivyo kuanza kuwindwa na timu kubwa, ikiwamo Simba.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: MO DEWJI ATAMBA KUFANYA MAKUBWA AFRICAN LYON Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top