• HABARI MPYA

  Saturday, March 07, 2009

  AMBANI AITWA DROGBA CHINA

  Ambani wa tatu kutoka kushoto, akishangilia na wenzake Yanga


  KOCHA wa klabu ya Greentown FC ya Zheijang, China, Zhou Suian amemfananisha mshambuliaji wa klabu ya Yanga ya Dar es Salaam, Boniphace Ambani na Didier Drogba wa klabu ya Chelsea ya England.
  Hakuna kingine kilichomfanya kocha huyo Mchina, kumfananisha mpachika mabao raia wa Kenya na mshambuliaji wa kimataifa wa Ivory Coast, zaidi ya uwezo wake wa kuwatungua makipa aliouonyesha kuanzia kwenye mazoezi hadi kwenye mechi.
  Ambani alikuwa China kwa majaribio ya kujiunga na klabu hiyo tangu Jumatatu, baada ya kuondoka nchini Jumapili jioni na mbali na kufanya mazoezi, pia aliichezea mechi mbili za kirafiki Jumanne na Ijumaa.
  Akizungumza kwa simu kutoka China jana, Ambani alisema mara baada ya kufika tu kwenye klabu hiyo, inayotumia Uwanja wa Yellow Dragon Sports Center, wenye uwezo wa kumeza mashabiki 51,000 Ambani alisema kwamba alikubalika mno mbele ya wachezaji wa timu hiyo.
  “Hii timu ina wachezaji wa Misri wawili wote washambuliaji (Salah Hosny na Mohsen Abugreisha), Mbrazil mmoja (Erivaldo) mshambuliaji pia na mmoja kutoka Algeria (Karim Benounes) yeye ni kiungo na beki kutoka Bulgaria (Yordan Varbanov).
  Wengine wote waliobaki ni Wachina, kwa ujumla timu nzima wamenikubali sana, baada ya ile mechi ya pili, wakala wangu aliyenileta huku, akaniambia, hongera Ambani, umepita, jamaa wamekukubali sana hadi mwenye timu.
  Akaniambia yule kocha, (Zhou Suian) alimfuata akamuambia: “ Asante, umetuletea mshambuliaji wa nguvu kama Drogba,”alisema Ambani ambaye anatarajiwa kurejea kesho mjini Dar es Salaam.
  “Naelekea Uwanja wa ndege wa Guangzhou, kupanda ndege hadi Shanghai, ambako nitalala kwa usiku moja kabla ya kupanda ndege kurejea Dar es Salaam. Nitakuwa huko Machi 9, saa 9 jioni,”alisema Ambani.
  Alipoulizwa kama alizungumza chochote na Wamisri wa timu hiyo, Ambani alisema: “Ndio, nimezungumza nao, nimewaambia nimetokea wapi, nikawaambia nitaichezea kwanza klabu ya huko mechi na Al Ahly ndio nirudi tena China,”alisema.
  Ambani mwenye shauku ya kutua haraka Dar es Salaam ili aungane na wenzake kwa maandalizi ya mechi dhidi ya Ahly, alisema kwamba yuko fiti na anataka aondoke Yanga akiwaachia mashabiki wa klabu hiyo zawadi nono.
  “Ninarudi, mashabiki wa Yanga ninawapenda sana, kwa sababu wamekuwa wakiniunga mkono kipindi chote nikiwa huko, nitapigana kwa uwezo wangu wote niwape matokeo mazuri kwenye mechi na Ahly,”alisema.
  Zheijang inataka kumchukua Ambani kuongeza makali yake msimu ujao, kwani kwa sasa tayari imekwishakosa nafasi ya kucheza Ligi ya Mabingwa Asia, ikiwa inashika nafasi ya tisa kwenye ligi hiyo inayoshirikisha timu 16. Ina pointi 39 na imebakiza mechi mbili ingawa haimo kwenye hatari ya kushuka daraja.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: AMBANI AITWA DROGBA CHINA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top