• HABARI MPYA

  Jumanne, Machi 24, 2009

  KASEJA AIBEBESHA YANGA UBINGWA


  Kaseja alipokuwa akisaini kuichezea Yanga


  Mwanza, Tanzania
  JUMA Kaseja Juma, kipa aliyedakia Simba kwa miaka saba tangu mwaka 2002 kabla ya kuhamia Yanga msimu huu, jana alikuwa kila kitu kwenye Uwanja wa CCM Kirumba mjini hapa, wakati timu yake inawalaza wenyeji Toto Afrika mabao 2-1 na kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, ikiwa imebakiza mechi tano.
  Kaseja jana aliifungia Yanga bao la kuongoza dakika ya 22 baada ya kupiga mpira mrefu kutoka kwenye lango lake na wakati kipa wa Toto, Msafiri Abdallah akitaka kuudaka aliambulia kuuparaza ukampita na kudondokea nyavuni. Lilikuwa bao la kihistoria, katika soka ya Tanzania, alilofunga kipa huyo ambaye baadaye alipangua mkwaju wa penalti, uliopigwa na Said Dilunga.
  Hiyo inakuwa mara ya 15 kwa Yanga, kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Bara iliyoanzishwa mwaka 1982 wakati Pan Afrika ndio walipokuwa mabingwa wa kwanza wa ligi hiyo, wakifuatiwa na Yanga mwaka 1983.
  Mwaka 1984 walikuwa ni Simba, 1985 Yanga, 1986 Tukuyu Stars ya Mbeya, 1987 Yanga,
  1988 Coastal Union ya Tanga, 1989 Yanga, 1990 Simba, 1991 Yanga, 1992 Yanga, 1993 Yanga, 1994 Simba, 1995 Simba, 1996 Yanga, 1997 Yanga, 1998 Yanga, 1999 Mtibwa Sugar ya Morogoro, 2000 Mtibwa Sugar tena, 2001 Simba, 2002 Yanga, 2003 Simba, 2004 Simba, 2005 Yanga, 2006 Yanga, 2007 Simba (Ligi ndogo), 2008 Yanga na 2009 pia ndio hao hao watoto wa Jangwani.
  Dalili za Yanga kibuka na ushindi kwenye mchezo huo, zilianza mapema
  baada ya Jerry Tegete kuukwamisha mpira nyavuni, lakini mwamuzi alisema mfungaji alikuwa ameotea.
  Yanga iliendelea kulisakama kama nyuki lango la Watoto wa Kishamapanda na dakika 19 ilifanikiwa kupata penalti, ambayo hata hivyo mkwaju wa kiungo Nurdin Bakari ulipanguliwa na kipa Msafiri.
  Kaseja alifunga bao lake baada ya kudaka mpira uliolekezwa golini kwake na kuwaashiria wachezaji wenzake kusogea mbele. Kama vile alimuona golikipa wa Toto, Msafiri Abdalah upande wa pili, alipiga mpira mrefu uliodunda ndani ya eneo la hatari la wapinzani wao na kipa huyo alipojaribu kuurukia, aliuparaza na kuubariki kuingia wavuni, kuwapa goli la kwanza Yanga ambao jana walicheza bila ya wachezaji wake watatu wa kimataifa wa Kenya waliorejea nyumbani kuichezea timu yao ya taifa, Harambee Stars. Hao ni George Owino, Ben Mwalala na Boniphace Ambani.
  Kana kwamba hiyo haitoshi, Kaseja alidaka penati iliyotolewa kwa Toto katika kipindi cha pili, jambo lililozuia wapinzani hao kupata bao la kusawazisha.
  Dalili za Yanga kuibuka na ushindi katika mchezo huo zilianza mapema, baada ya kupata bao dakika ya nane tu ya mchezo, lakini mwamuzi wa mchezo huo alikataa bao hilo kwa madai kwamba wachezaji wa Yanga walikuwa wameotea.
  Dakika ya 19, Yanga walipata penalti baada ya mlinzi wa kulia wa Toto, Ramadhan Haruna kuunawa mpira ndani ya eneo la hatari, akiwa katika harakati za kuokoa. Toto walilalamikia adhabu hiyo, lakini mwamuzi alishikilia uamuzi wake.
  Hata hivyo, mlinda mlango wa vijana hao wa Mwanza, Msafiri Abdalah alichupa na kupangua mkwaju huo uliopigwa na Nurdin Bakari.
  Toto walisawazisha katika dakika ya 26, baada ya mchezaji wa zamani wa wababe hao wa Jangwani, Hussein Sued kufunga kiufundi baada ya kumlamba chenga beki Nadir Haroub ‘Cannavaro’ na kumchambua vizuri Kaseja.
  Hata hivyo, furaha ya Toto haikudumu sana, kwani mpira wa adhabu ndogo uliopigwa na mshambuliaji mwingine wa kimataifa wa Kenya Mike Barasa, katika dakika ya 32, ulikwenda moja kwa moja wavuni, licha ya Msafiri kujaribu kuupangua.
  Hilo lilikuwa bao la kwanza Barasa anaifungia Yanga kwenye ligi hiyo tangu ajiunge kwenye usajili wa dirisha dogo Desemba mwaka jana, akitokea Malaysia.
  Bao lingine ambalo Barasa ameifungia Yanga, ilikuwa kwenye mechi ya kirafiki dhidi ya Vancouver Whitecaps Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam wakati timu hiyo inashinda 3-0.
  Hadi mapumziko, timu hizo ‘ndugu’ zilikwenda mapumziko kwa matokeo hayo hayo.
  Kipindi cha pili kilianza kwa kasi na Toto walipata penati baada ya dakika 61, baada ya Nahodha Freddy Mbuna kumkwatua Hussein Sued aliyekuwa akienda kumuona Kaseja. Lakini Kaseja, mwenye sifa za kuokoa mikwaju ya penati, aliupangua mkwaju huo.
  Wakati huo huo, mwandishi wetu kutoka Mbeya, Felix Mwakyembe anaripoti kuwa mchezo kati ya Kagera Sugar na wenyeji Prisons, uliokuwa ukipigwa katika uwanja wa Sokoine, uliahirishwa baada ya dakika 22 kutokana na kujaa maji yaliyosababishwa na mvua kubwa iliyokuwa ikinyesha.
  Hadi mchezo huo unavunjwa, timu hizo zilikuwa sare kwa kufungana bao 1-1, Prisons ikiwa ya kwanza kupata bao katika dakika ya nne, mfungaji akiwa ni Shaaban Mtupah, lakini Hassan Haruna aliisawazishia Kagera katika dakika ya 18.
  Baada ya maji kuwa mengi uwanjani, mwamuzi wa mchezo huo aliwasiliana na kamisaa wake, ikiwa ni pamoja na viongozi wa timu zote mbili na wale wa Chama cha soka mkoa wa Mbeya na kuamua kuuvunja mchezo huo ambao utachezwa tena leo.
  Katika mchezo mwingine wa ligi hiyo, uliofanyika Uwanja wa Uhuru, zamani Taifa mjini Dar es Salaam, Azam FC iliibuka na ushindi wa 6-2 dhidi ya Villa Squad. Kiungo wa zamani wa Moro United na Simba, Nsa Job alifunga mabao matano peke yake wakati lingine lilifungwa na mshambuliaji wa kimataifa wa Uganda, Dan Wagaruka.

  ORODHA YA MABINGWA WA BARA:
  1982 - Pan African
  1983 - Yanga
  1984 – Simba
  1985 - Yanga
  1986 - Tukuyu Stars
  1987 - Yanga
  1988 - Coastal Union
  1989 - Yanga
  1990 - Simba
  1991 - Yanga
  1992 - Yanga
  1993 - Yanga
  1994 - Simba
  1995 - Simba
  1996 - Yanga
  1997 - Yanga
  1998 - Yanga
  1999 – Mtibwa Sugar
  2000 – Mtibwa Sugar
  2001 - Simba
  2002 - Yanga
  2003 - Simba
  2004 - Simba
  2005 - Yanga
  2006 - Yanga
  2007 - Simba (Ligi ndogo)
  2008 - Yanga
  2009 – Yanga
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: KASEJA AIBEBESHA YANGA UBINGWA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top