• HABARI MPYA

    Saturday, March 14, 2009

    FEROOZ, NATURE WAIREJESHA BONGO FLEVA DIAMOND JUBILEE




    ENZI za mashabiki wa muziki wa Bongo Fleva kukutana katika ukumbi wa Diamond Jubilee, Dar es Salaam kushuhudia wasanii wa muziki huo wakifanya vitu vyao, zinatarajiwa kuanza kurejea tena Ijumaa wiki hii, (Machi 20, mwaka huu).
    Katika usiku huo, vijana wawili vipenzi vya wapenzi wa Bongo Fleva, Feruzi Mrisho maarufu kama Ferooz na Juma Kassim anayejulikana zaidi kwa jina la utani, Sir Nature watakuwa wakizundua albamu zao.
    Kwa Nature, siku hiyo atakuwa akitambulisha albamu yake ya tano, iitwayo Tugawane Umasikini, inayofuatia vigongo vinne alivyotanguliza mkali huyo, Nini Chanzo, Ugali, Ubinadamu Kazi na Zote History.
    Nature ambaye kwa sasa anatamba na kundi lake la Wanaume Halisi, kutoka kwenye albamu yake mpya, ametambulisha nyimbo tatu ambazo ni Ulevi, Africa Number One na Mzamiaji alioimba na kundi lake, Wanaume Halisi.
    “Katika wimbo huu Mzamiajo yupo pia mtu anaitwa JB wa kundi la Mabaga Fresh, ambao wamejiunga na sisi (Wanaume Halisi,”alisema nature katika mahojiano na BINGWA juzi mjini Dar es Salaam.
    Kwa sasa Nature amejichimbia na kundi lake, Halisi wilayani Temeke kila siku jioni wakijifua kwenye Uwanja wa TCC, Chang’ombe kwa ajili ya uzinduzi wao, Machi 20 ndani ya Diamond Jubilee.
    Wapenzi wa muziki huo mjini Dar es Salaam wana hamu ya kumuona nature akisema nao jukwaani, kwani katika kipindi ambacho amewapotea machoni yamepita mengi, ikiwemo sakata la kuzushiwa kubaka msichana mwanafunzi.
    Sakata hilo liliibuka mwishoni mwa mwa jana na ilidaiwa Nature aliwahi kushikiliwa na kiuto cha Polisi, Mbagala anakoishi akituhumiwa kuwa na uhusiano ya kimapenzi na mwanafunzi anayedaiwa kuwa chini ya umri wa miaka 18.
    Kamanda wa Polisi Temeke, Emmanuel Kandihabi aliwahi kukaririwa akisema ni kweli Nature alifikishwa Polisi kwa tuhuma hizo na baadaye kujachiwa kwa dhamana.
    Lakini Nature alipozungumzia sakatak hilo, alisema hajawahi kukamatwa na wala hajui chochote kuhusu tukio hilo na amekuwa nyumbani kwake kwa siku zote ambazo ilielezwa alikuwa Polisi akisistiza: “Nipo salama kabisa na sijawahi kukamatwa na polisi mahala popote,”.
    Kama lilivyo jina la albamu yake iliyopita, Zote History basi kwa wakati huo, sakata hilo pia ni historia kikubwa ni uzinduzi wa albamu yake ya tano, Tugawane Umasikini.
    Kihistoria Nature alizaliwa mwaka 1980 na kimuziki aliibuka mwaka 1999, baada ya kushirikishwa na kundi la Mabaga kwenye wimbo Mtulize.
    “Vesi langu baya halifagiwili, kisa kampani yangu viziwi”. Ni sehemu ya mashairi ya Nature katika mwimbo huo wa Mabaga Mtulize, ambayo kwa sauti yake ya staili yake ya kughani, haikuchukua muda akaiteka hadhira.
    Ruge Mutahaba wa Clouds FM, aliniagiza nimtafute kijana huyo nimpeleka Clouds ili wamsaidie kimuziki.
    Nilifanikisha zoezi hilo na baada ya Nature kufika kwa Ruge alisajiliwa kwenye kampuni yake ya kuinua vipaji, Smooth Vibes na kumpeleka kwa Master Jay, ambaye wakati huo alikuwa akitayarisha albamu ya kwanza ya Lady Jaydee iliyokwenda kwa jina Machozi.
    Hata hivyo, baadaye nilipokutana na Nature alilalamika kuhusu Master Jay: “Jamaa ananizungua, anasema eti mimi bado sana, lakini kua wimbo mmoja nimefanya Jaydyee,”aliniambia Nature.
    Ni wakati huo huo, P Funk naye alikuwa anatafuta wasanii kwa ajili ya kuanzisha lebo yake, Bongo Records hivyo zali likamuangukia tena Nature kwania alikuwa miongoni mwa wasanii walipokwenda kuasisi lebo hiyo sambamba na Solo Thang na Jay Moe.
    Hapo sasa ndipo historia rasmi ya kimuziki ya Nature ilipoanzia kwani alifyatua nyimbo mfululizo kuanzia Hili Game, Jinsi Kijana hadi kutoa albamu yake ya kwanza, Nini Chanzo.
    Hakika Nini Chanzo ulikuwa mwanzo mzuri wa safari ya kimuziki ya Nature kwani hivi sasa kama litatoka swali, nani mwanamuziki aliyefika mbali zaidi kati ya wote nchini, bila shaka hata baada ya kukuna kichwa sana, jibu litakuwa Nature tu.
    Nature ndiye mwanamuziki pekee wa Tanzania hadi sasa, aliyeweza kuingia kwenye kinyang’anyiro cha tuzo za muziki za MTV Ulaya, hiyo ilikuwa ni mwaka 2006 wakati tuzo hizo zilipotolewa mjini Copenhagen, Denmark.
    Lakini Nature alikwama kwenda kuhudhuria utoaji wa tuzo hizo uliofanyika Novemba 2, mwaka huo kutokana na sababu ambazo hadi sasa hazijafahamika, ingawa hicho ndio kilkuwa chanzo cha mwanamuziki huyo kujiengua kwenye kundi la Wanaume Family TMK na kuasisi Wanaume Halisi.
    Nature alidai Meneja wa Wanaume Family, Said Fela ndiye aliyesababisha akose safari hiyo, lakini bosi wake huyo wa zamani naye alimtupia lawama msanii huyo kwamba alikwenda kustarehe Kenya na kusahau kuhusu safari hiyo.
    Lakini pia Nature kupitia wimbo wake, Mugambo amewahi pia kushinda tuzo ya Channel O Spirit of Africa.
    Nature amewahi kutajwa kuwania tuzo nyingine kubwa za muziki Afrika kama MTV Afrika na KORA, ambako kote pamoja na kutoka kapa, lakini alijijengea hadhi kubwa kwenye ulimwengu wa muziki.
    Albamu Nini Chanzo aliitoa mwaka 2001, wakati Ugali ilikuja mwaka 2003, Ubinadamu Kazi mwaka 2005, Zote History mwaka 2006 na sasa mashabiki wote wa Nature wanazungumza lugha moja, Tugawane Umasikini mwaka 2009.

    FEROOZ WA DAZ NUNDAZ...
    Baada ya kimya cha muda mrefu, msanii nyota wa muziki wa Bongo Fleva, Ferooz Mrisho anatarajiwa kuzindua albamu yake ya pili, Sauti na Vyombo Machi 20, mwaka huu kwenye ukumbi wa Diamond Jubilee, Dar es Salaam.
    Ferooz ni msanii aliyepata mafanikio makubwa baada ya albamu yake ya kwanza, Safari iliyoongozwa na wimbo, Starehe kiasi cha kununua bonge la gari, Jeep, anasema kwamba yuko tayari kufanya vitu vya nguvu Machi 20.
    "Nakuja kiutu uzima mtu wangu, niko sawa sawa mpaka basi, watu waje kwa wingi Diamond,"alisema Ferooz aliyezaliwa miaka 27 iliyopita alipozungumza na BINGWA.
    Hata hivyo, ukimya wake tangu atoe albamu hiyo mwaka 2005 ulizua gumzo kubwa, kwamba amecheza na maisha na amefilisika kiasi cha kuuza hata gari yenyewe.
    Hata hivyo katika mahojiano haya, Ferooz anasema kwamba kimya chake kilikuwa ni staili yake tu kwamba aliipa nafasi albamu yake ya kwanza, Safari ambayo anajivunia mfanikio yake.
    “Nashukuru, Safari imefanya vizuri sana na ndio maana sikuona sababu ya kuingiza kazi nyingine haraka sokoni,”anasema.
    Anazitaja baadhi ya nyimbo zilizomo kwenye albamu hiyo kuwa ni Sauti na Vyombo yenyewe, Rusha Kila Kipindi aliomshirikisha Dully Sykes, Wakiibana Sanaa na Mr. Policeman ambayo imekuwa ya kwanza kuitambulisha kwenye vituo vya Radio nchini.
    Lakini pia Ferooz anasema mgogoro uliolikumba lake, Daz Nundaz kwa kiasi nao ulichangia kumchelewesha kutoa albamu mpya.
    “Baada ya kutoa albamu yangu ya kwanza, tulipanga Daz Nundaz kama kundi tutoe albamu ya pamoja, ambayo ingekuwa ya pili baada ya Kamanda, kwa bahati mbaya tukiwa katika maandalizi ya albamu hiyo ikaibuka mizozo ya kijinga jinga, tukapoteza malengo," anasema.
    Ferooz alikuwa msanii wa kiongozi wa kundi Daz Nundaz lililoibuka mwaka 1999 pia, likiwa linaundwa na nyiota wengine kama Daz Baba, Critic, La Rumba na Sajo.
    Wimbo Maji ya Shingo waliourekodi kwenye studio za FM chini ya mtaalamu Mika Mwamba enzi hizo ndio wa kwanza kulitambulisha kundi hilo.
    Hatimaye Daz wakafanikiwa kutoa albamu iliyokuwa na nyimbo kali tupu, Kamanda ambayo iliwahi kusifiwa hadi Wabunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
    Hata hivyo si Mika Mwamba aliyewapeleka sokoni Daz Nundaz, bali walichukuliwa na P Funk katika mradi wa Bongo Records na huko ndiko walipokamilishia albamu yao, Kamanda.
    Baada ya mafanikio ya Kamanda akiwa na Daz Nundaz, ndipo walipokubaliana kila mmoja kutoka wasanii wa kundi hilo, atoe albamu yake.
    Hata hivyo, walitoka wasanii wawili tu, yeye na Daz Baba, lakini wengine ambao mwishoni ilikubaliwa watoe albamu na kundi hilo, walikwama.
    “Ndio kama hivyo, migogoro bwana, watu tulishindwa kuelewana, lakini sasa mimi kama Ferooz naangali mbele, anayecheza shauri yake,”anasema.
    Ferooz pia amewahi kushinda tuzo kadhaa za muziki ikiwemo ya wimbo bora wa mwaka 2004 katika tuzo za muziki Tanzania, maarufu kama tuzo za Kili, kupitia wimbo wake Starehe aliomshirikisha Profesa Jay.
    Tuzo nyingine kubwa aliyoshinda msanii huyo ni ya BBC Tanzania kama msanii bora wa kiume mwaka 2005.
    Naam, hao ndio wasanii watakaoirejesha Bongo Fleva Diamond Jubilee, baada ya takriban mwaka mzima wa kuadimika kwa matamasha ya muziki huo kwenye ukumbi huo. Bila shaka, itakuwa siku nyingine ya furaha kwa wapenzi wa muziki huo.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: FEROOZ, NATURE WAIREJESHA BONGO FLEVA DIAMOND JUBILEE Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top