• HABARI MPYA

    Friday, March 20, 2009

    NGASSA AITWA WEST HAM UNITED


    WINGA machachari wa klabu ya Yanga ya Dar es Salaam, Mrisho Khalfan Ngassa (pichani kulia) amesema kwamba baada ya mchezo wa marudiano dhidi ya Al Ahly ya Misri, Raundi ya Kwanza Ligi ya Mabingwa Afrika, atakwenda Uingereza kufanya majaribio katika klabu ya West Ham United ya nchini humo.
    Akizungumza jana mjini Dar es Salaam, Ngassa alisema kwamba alipewa taarifa hizo juzi na wakala wake, Yussuf Bekhresa kwamba anatakiwa na klbau hiyo ya Ligi Kuu ya England.
    “Nashukuru, nimepata nafasi nyingine, nadhani baada ya mechi ya marudiano na Al Ahly nitakwenda West Ham kujaribu bahati yangu tena,”alisema winga huyo aliyejiunga na Yanga msimu wa 2006/2007, akitokews Kagera Sugar ya Bukoba.
    Habari zaidi zinasema kwamba juzi, Bakhresa alikuwa kwenye mazungumzo na uongozi wa Yanga kuhusu suala hilo na imeelezwa tayari wamefikia maafikiano.
    Hata hivyo, juhudi za kumpata Mwenyekiti wa Yanga, Imani Madega na wakal huyo jana kuzungumzia mpango huo, hazikuweza kufanikisha hadi tunaingia mitamboni.
    Bakhresa ndiye wakala aliyempatia nafasi ya kwanza ya klwenda Ulaya Ngassa, nchini Norway katika klabu ya Lov Ham, inayoshiriki Ligi Daraja la Pili nchini humo ambako hata hivyo alishindwa kwenda kutokana na uongozi wa klabu yake kugoma.
    Wakati Ngassa alipopata ngekewa ya Norway mapema mwaka huu, Madega alikaririwa na vyombo vya habari akisema kwamba wasingemruhusu Ngassa kwenda Norway kwa kukurupuka, kwani walitaka kufanya mambo kwa uhakika. Alisema Lov Ham ilituma barua ya kumtaka Ngassa kwenda kufanya majaribio ya wiki moja na wakati huo huo imetangaza dau la dola za Kimarekani 50,000 kumnunua, jambo ambalo liliwakanganya.
    Mbali na Norway, Mwenyekiti wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT) Iddi Kipingu aliwahi kukaririwa akisema kwamba alituma DVD za mchezaji huyo katika klabu mbalimbali Ufaransa na Marseille ya huko ilivutiwa naye hivyo kuonyesha nia ya kumuita kwa majaribio.
    Hata hivyo, Kipingu aliyesema anafanya jitihada za kuwatafutia timu Ulaya wachezaji wengine pia wa Tanzania, alisema mawasiliano yanaendelea baina yake na klabu hiyo kuhusu Ngassa.
    Ngassa, mtoto wa kiungo wa zamani wa klabu ya Pamba ya Mwanza na Simba ya Dar es Salaam, Khalfan Ngassa aliyewika mwishoni mwa miaka ya 1980 hadi mwanzoni mwa miaka ya 1990 ambaye kwa sasa ni kocha, alizaliwa Mei 5, mwaka 1989 mjini Mwanza, alikokulia.
    Akiwa na umri wa miaka 17, Ngassa tayari alianza kucheza Ligi Kuu ya Tanzania, inayodhaminiwa na Vodacom katika klabu ya Kagera Sugar ya Bukoba.
    Ni mwaka 2006, baada ya kung’ara kwenye michuano ya Kombe la Tusker na kuiwezesha Kagera kutwaa taji hilo, wakiifunga Simba kwenye fainali, ndipo alipochukuliwa na Yanga.
    Baada ya kuchezea timu za vijana tangu mwaka 2005, mwaka 2006 aliitwa kwenye kikosi cha timu ya taifa ya Tanzania Bara, kilichoshiriki michuano ya Kombe la Challenge nchini Ethiopia.
    Mapema mwaka jana alipandishwa kwenye kikosi cha wakubwa na moja kwa moja akawa kipenzi cha kocha Mbrazil, Marcio Maximo kutokana na nidhamu na kujituma kwake uwanjani.
    Baada ya kupoteza nafasi ya kucheza Norway, je winga huyo atafanikiwa West Ham? Bila shaka hilo ni jambo la kusubiri na kuona huku tukimuombea dua njema kijana huyo mwenye kipaji afanikiwe.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: NGASSA AITWA WEST HAM UNITED Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top