• HABARI MPYA

  Ijumaa, Machi 20, 2009

  MBUNGE AZZAN ATOA NASAHA THT

  Ruge na Azzan wakishuhudia mambo ya THT

  WANAFUNZI na jamii kwa ujumla wameaswa kutumia vyema elimu kwa njia ya sanaa ya maigizo inayotolewa na kikundi cha burudani cha Tanzania House of Talent (THT), katika mapambano dhidi ya maradhi ya UKIMWI.
  Mwito huo ulitolewa Dar es Salaam juzi na Mbunge wa Kinondoni, Idd Azzan wakati wa hafla ya kuhitimisha awamu ya kwanza ya programu maalumu ya elimu kwa njia ya maigizo inayotolewa na THT katika shule za msingi na sekondari nchini, kwa udhamini wa kampuni ya simu za mkononi ya Zain Tanzania.
  "Napenda kuipongeza Zain kwa kuidhamini THT ili kuelimisha wanafunzi kujikinga na UKIMWi, na nawaasa mtumie maigizo haya kupanua wigo wa maarifa ya mapambano dhidi ya maradhi ya UKIMWI," alisema Azzan aliyekuwa mgeni rasmi katika hafla hiyo iliyokutanisha wanafunzi wa shule mbalimbali za Dar es Salaam, huku kauli mbiu ikiwa ni 'Fikiria mara mbili'.
  Awali, Mkurugenzi wa THT, Ruge Mutahaba alisema kikundi hicho kimetembelea shule 27 za Dar es Salaam kutoa elimu ya UKIMWI, na akabainisha kwamba awamu ya pili kutembelea shule za mikoani inatarajiwa kuanza Aprili, na akaishukuru Zain, walimu wa shule hizo na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi kwa kuwaunga mkono.
  Zain ilikipatia kikundi cha THT udhamini ikiwa ni pamoja na basi kwa ajili ya kutoa elimu kupitia sanaa na maigizo kuelimisha mapambano dhidi ya UKIMWI katika shule za msingi na sekondari nchini.
  Meneja wa Huduma za Jamii wa Zain Tanzania, Tunu Kavishe alisema Zain ilitoa sh. milioni 35 katika mradi huo wa THT ili kusaidia kuelimisha wanafunzi na kizazi kipya kwa ujumla katika nyanja mbalimbali ikiwa ni pamoja na kujikinga na maambukizo ya maradhi ya UKIMWI.
  Rebecca Young, Meneja wa THT alisema: "Tunaona fahari kwa Zain kujikita kusaidia programu yetu na kutupatia pesa za kuendeleza programu yetu. Sanaa imedhihirisha ni njia bora ya kufikisha ujumbe kwa jamii, na THT ina uwezo wa kutumia njia hiyo kufikisha ujumbe kuhusu mada mbalimbali kwa njia ya sanaa jukwaani," alisema.
  THT wanatoa elimu hiyo kwa njia ya sanaa ikiwa ni pamoja na ujumbe kupitia muziki, dansi na ngoma. Kikundi cha THT kilianzishwa mwaka 2005 na kinaundwa na vijana wapatao 45 wenye umri kati ya miaka 14 na 24. Kundi hilo la vijana limekuwa likitoa burudani maridhawa katika matukio mbalimbali nchini.Mwisho...
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: MBUNGE AZZAN ATOA NASAHA THT Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top