• HABARI MPYA

  Monday, March 09, 2009

  NGASSA ANA USONGO NA AL AHLY


  WINGA mahiri wa klabu ya Yanga, Mrisho Khalfan Ngassa (KULIA) amesema kwamba huu ndio wakati wa Yanga `kufuta uteja` wa kufungwa na timu za Waarabu kwa kuhakikisha kuwa wanaibuka na ushindi katika mechi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Al Ahly ya Misri.
  Yanga na Al Ahly wanatarajia kukutana Machi 15 jijini Cairo na baada ya wiki mbili kurudiana hapa jijini Dar es Salaam.
  Akizungumza na Nipashe jana, Ngassa alisema kuwa wamejiandaa kufanya vizuri katika mchezo huo na wanaahidi kwamba kila mchezaji atakayepangwa atacheza kwa bidii ili kutimiza malengo.
  Ngassa alisema kuwa wanafahamu kwamba licha ya kuipa matokeo mazuri timu yao na kujiweka katika mazingira mazuri ya kusonga mbele, pia mechi hiyo ni nafasi nyingine kwa wachezaji wa Tanzania kutangaza vipaji vyao.
  Alisema kuwa kila siku anapomaliza mazoezi, akili yake inawaza ni jinsi gani atakuwa anawapenya mabeki wa Al Ahly na kupeleka mashambulizi katika lango la wapinzani hao ili kutafuta mabao.
  ``Hakuna jambo lisilowezekana katika dunia ya leo, inaweza kutokea kama ilivyokuwa kwa Sudan, wengi walisema kuwa mwisho wa safari ya Stars (timu ya taifa) lakini tuliifunga na tukafuzu kucheza CHAN,`` alisema Ngassa.
  Aliongeza kuwa, jambo linalotakiwa hivi sasa ni kuomba wachezaji wote wawe katika hali ya usalama na wale watakaopangwa kuweza kujituma vyema.
  Alisema kuwa wachezaji wa Al Ahly wanambinu zao na Yanga pia wamepanga mikakati yao dakika 90 ndio zitakuwa mwamuzi wa yote.
  Katika sehemu ya maandalizi ya kuwavaa Waarabu hao, Yanga leo inacheza mechi ya kirafiki ya kimataifa na klabu ya Vancouver Whitecaps kwenye Uwanja wa Taifa, jijini, Dar es Salaam.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: NGASSA ANA USONGO NA AL AHLY Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top