• HABARI MPYA

    Saturday, March 14, 2009

    NYOTA VANCOUVER KUMBEBA BARASA WA YANGA


    MSHAMBULIAJI mkongwe wa klabu ya Yanga ya Dar es Salaam, Mike Barasa, amepata ngekewa ya aina yake, baada ya nyota wa klabu ya Vancouver Whitecaps ya Canada, Marlon Alex James, kuamua kumsukia mipango, ajiunge na klabu hiyo.
    Akizungumza na DIMBA mjini Dar es Salaam juzi, James (pichani kulia), aliyeifungia Whitecaps mabao mawili wakati inailaza Simba 2-1, alisema atamsaidia Barasa kwa sababu wanafahamiana kabla ya kukutana hapa.
    “Nazungumza na kocha wangu, kama itashindikana hapa, basi hata timu nyingine ya kule, namjua sana Barasa, ni mchezaji mzuri, nilikuwa nacheza naye Ligi moja Malaysia, tulikuwa timu tofauti,” alisema mchezaji huyo, ambaye alimpa viatu beki wa Yanga, Nadir Haroub ‘Cannavaro’.
    Nyota huyo wa timu ya taifa ya St. Vincent & Grenadines, alisema kwamba baada ya kucheza mechi mbili dhidi ya timu kongwe Tanzania, amegundua kwamba Yanga ni wazuri mno kuliko wapinzani wao wa jadi, Simba.
    Mfungaji bora huyo wa Ligi Kuu ya Malaysia msimu wa 2007/2008, alisema kwamba hajaonyesha cheche zake haswa katika mechi hizo mbili, kwa sababu wamekuja Tanzania wakati wa matayarisho ya kuingia kwenye msimu mpya.
    James, aliyejiunga na Vancouver Desemba 23, mwaka jana akisaini mkataba wa miaka miwili, alisema kwamba mbali na Barasa, pia amevutiwa na soka ya beki Nadir Haroub ‘Cannavaro’ na kiungo Athumani Iddi ‘Chuji’.
    “Kwa sababu nimechukua namba za Barasa, na hawa pia nitajaribu kuwatafutia timu, wanaweza kucheza Canada wakiwa wanalipwa vizuri na kufurahia maisha ya soka,” alisema mpachika mabao huyo, aliyezaliwa Novemba 16, mwaka 1976.
    James amekuwa akiichezea timu ya taifa ya St. Vincent & Grenadines tangu mwaka 1995 na ameifungia mabao 12 katika mechi 55, yakiwemo mabao 10 katika mechi za kuwania kufuzu kwenye fainali za Kombe la Dunia.
    Aliifungia kwa mara ya mwisho timu yake ya taifa, ilipomenyana na Canada mjini Montreal, Juni 20, mwaka jana wakati St. Vincent & Grenadines inachapwa mabao 4-1, katika mchezo wa kuwania kucheza fainali za Kombe la Dunia mwaka 2010 nchini Afrika Kusini.
    Nyota huyo ambaye awali alikuwa mkimbiaji, kisoka aliibukia kwenye klabu ya kwao, Youth Olympians, kabla ya kuhamia MK Land FC na baadaye Kedah FA ya Malaysia, ingawa aliwika zaidi alipokuwa Kedah ya Malaysia pia.
    Akiwa MK Land FC, alifunga mabao 19 kwenye msimu wa Ligi wa 2004 na mengine 22 alifunga msimu wa 2005, hivyo kuchukuliwa na klabu ya FC Tirsense ya Santo Tirso iliyokuwa Daraja la Pili, Ureno, ambako alifunga mabao 24 katika mechi 33.
    Lakini baada ya msimu wa 2006/2007, alirejea Malaysia kujiunga na Kedah FA ambako alifanya vitu vikubwa hadi kupewa tuzo ya Mwanasoka Bora wa Kigeni nchini humo, kutokana na mabao yake 40 aliyofunga msimu huo, kuiwezesha timu hiyo kubeba mataji yote nchini humo, Kombe la FA, Ligi Kuu na Kombe la Ligi.
    Alishinda tena tuzo hiyo baada ya msimu uliofuata kuiwezesha tena Kedah FA kushinda mataji yote hayo 2007/2008. Lakini kilichomtoa nchini humo ni Chama cha Soka Malaysia (FAM) kupiga marufuku wachezaji wa kigeni kwenye Ligi yao.
    Ikumbukwe tayari mchezaji mwingine wa Yanga, Mkenya pia Boniphace Ambani, amefuzu majaribio katika klabu ya Greentown ya Zheijang, China.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: NYOTA VANCOUVER KUMBEBA BARASA WA YANGA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top