• HABARI MPYA

  Jumamosi, Machi 14, 2009

  YANGA WAPOKEWA KIFALME MISRI

  Wachezaji wa Yanga wakiwa Cairo baada ya kuwasili


  Majuto Omary, Cairo
  WAWAKILISHI wa Tanzania katika Ligi ya Mabingwa Afrika, Yanga, imepata mapokezi ya aina yake ambayo yameandika historia ilipowasili juzi usiku, kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Cairo.
  Mapokezi hayo yaliyoongozwa na msaidizi wa balozi wa Tanzania nchini Misri, Jestas Nyamanga aliyeandaa basi maalum kwa ajili ya timu hiyo aliliacha lile la wenyeji, Al Ahly likiwabeba mashabiki wengi waliojitokeza kuilaki timu hiyo.
  Mashabiki hao kila mmoja akiwa amebeba bendera ya Tanzania walikuwa wakiimba nyimbo zikiwamo za kuwatia moyo na hamasa wachezaji wa Yanga ambao awali hawakujua kile kilichotokea nje.
  Wachezaji hao wa Yanga waliwasili na kusikia kelele ambazo waliamini zilikuwa za mashabiki wa Al Ahly zilizoandaliwa ili kuwavunja moyo.
  "Kumbe ni Watanzania wenzetu, kweli hii ni historia kupokewa na mashabiki wengi kiasi hiki, pongezi kwa balozi na wafanyakazi wote wa ubalozi waliofika hapa," alisema meneja wa timu hiyo, Kenneth Mkapa.
  Kwa upande wake, mwenyekiti wa Yanga, Imani Madega alisema kuwa wamefarijika na mapokezi hayo na kazi iliyopo mbele yao ni kushinda tu.
  Wengi wa Watanzania waliofika kwenye mapokezi hayo ni wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Azhar na Watanzania wengine wanaoishi na kufanya kazi nchini humu.
  Msafara wa timu ya Yanga ulikuwa wa magari takribani 12, ukiongozwa na magari mawili ya polisi hadi hoteli ya Royal Marshal mahali ilikofikia .
  Baada ya kufika hapo majira ya saa 6:30 usiku kwa saa za Tanzania, mkuu wa msafara, wakili Alex Mgongolwa alipinga uamuzi wa kuilaza timu hiyo kwenye hoteli hiyo kwa kuwa ina hadhi ya chini.
  Baada ya mabishano ya muda mrefu, uongozi wa Al Ahly, chini ya mratibu wao, Ibrahim Saad walikubaliana na Mgongolwa kuwa watalala kwa usiku mmoja na baadaye kuhamia hoteli nyingine kubwa na yenye hadhi kama Kilimanjaro Kempinsky au Movenpick, zote za Dar es Salaam.
  Saad aliitetea hoteli hiyo ya Royal Marshal akieleza kuwa imepitishwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF) na ndiyo maana wao wameandaa hoteli hiyo kwa ajili ya malazi ya Yanga.
  Baada ya mabishano hayo kudumu kwa muda mrefu, uongozi wa timu ya Al Ahly ulimfuata Mgongolwa usiku wa manane kuzungumzia suala hilo, lakini hali ilikuwa ngumu na kikao kufanyika jana asubuhi na makubaliano kadhaa kufikiwa.
  Katika makubaliano hayo iliafikiwa kuwa Yanga iendelee kukaa hapo na wao Al Ahly wakifika Dar es Salaam watakaa kweye hoteli yoyote watakayopangiwa na wenyeji wao bila kugoma, ili mradi iwe imeidhinishwa na CAF.
  Pia, kama Yanga watataka kuhama hapo, wao (Ahly) wakifika Dar es Salaam watakaa kwenye hoteli kubwa kama Movenpick au Kilimanjaro Kempimsky.
  Baada ya masharti hayo, Madega na kocha mkuu, Dusan Kondic walikubali kukaa hapo ambapo ni mwendo wa dakika 15 hadi kufika kwenye uwanja wa mazoezi jijini Cairo.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: YANGA WAPOKEWA KIFALME MISRI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top