• HABARI MPYA

  Friday, March 20, 2009

  HUYU NDIYE SYLLERSAID MZIRAY...


  KWA miaka mitatu, tangu mwaka 1997, klabu ya Simba ilikuwa katika hali mbaya kisoka ilipoteza makali yake na kuanza kukosa nafasi za kucheza michuano ya Afrika hadi mwaka 2001 ilipopata tiketi ya kushiriki michuano ya Kombe la Washindi.
  Licha ya makocha tofauti kupewa jukumu la kuifundisha timu hiyo, Simba iliambulia patupu katika kipindi chote hicho.
  Ni orodha ndefu ya makocha, wakiwamo Athumani Juma Kalomba, Mohammed Kajole na Nzoyisaba Tauzany (wote sasa marehemu) na Abdallah Kibadeni, ambao walipewa jukumu la kuina timu hiyo na hawakuweza kuirejeshea makucha yake.
  Nani aliifanya Simba ipate nafasi ya kushiriki Kombe la Washindi mwaka huo? Alikuwa ni Syllersaid Kahema Mziray (pichani kulia), kocha mzoefu na mwenye rekodi ya kujivunia katika soka ya Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla.
  Mziray aliingia mkataba wa kuinoa Simba kwa ajili ya michuano ya Kombe la Chama cha Soka Tanzania (FAT) sasa shirikisho (TFF) na baadaye Kombe la Nyerere, ambalo wakati huo lilikuwa linatoa mwakilishi wa Kombe la Washindi.
  Mziray anasema siri ya mafanikio ya Simba wakati huo ilikuwa ni utendaji wake bora wa kazi, ambao aliufanya kwa umakini.
  “Nawajibika kufahamu ninafundisha timu ya aina gani, yenye wachezaji wa aina ipi,” anasema.
  “Hapo ndipo ninaamua tucheze mfumo upi, ili tupate ushindi.”
  “Hilo ndilo linalofanya timu nyingi ninazozifundisha ziwe tishio.”
  Kwa sababu hiyo, mashabiki wa Simba, walimfananisha Mziray na mwokozi, kutokana na kujenga msingi wa amani na upendo ndani ya klabu.
  Lakini Mziray si mali kwa Simba tu, watani wao wa jadi, Yanga, nao walishaonja matunda ya mtalaamu huyo, ambaye kipaji chake katika ufundishaji, kilianza kuonekana tangu mwaka 1986 wakati alipochukuliwa na Simba.
  “Ilikuwa ni mara ya kwanza kwangu kufundisha timu,”anasema Mziray.
  Enzi hizo, Mwenyekiti wa Simba alikuwa Emmanuel Makaidi na Katibu Mkuu Jimmy David Ngonya na jukumu la kwanza walilompa Mziray ilikuwa kwenda na timu hiyo katika michuano maalumu ya kirafiki nchini Kenya.
  “Nasikitika nilianza vibaya kazi, timu ilikuwa na wachezaji wengi wapya, walikuwa hawajazoeana. Sasa tulifungwa mabao mengi mno,” alikiri Mziray.
  Mziray anasema katika michauno hiyo, ambayo walialikwa na Re-Union, mechi ya kwanza walifungwa mabao 5-0 na AFC Leopards ya pili walifungwa 2-0 na wenyeji wao, kabla ya kucharazwa 5-0 tena na Gor Mahia.
  “Baada ya hapo, tulirejea na kuanza kurekebisha timu. Michuano ya pili kushiriki ilikuwa ni Kombe la FAT, ambayo pia tulikwenda kufungwa bao 1-0 na Tukuyu Stars mjini Mbeya na kutolewa,” anasema.
  “Msimu uliofuata, timu ilianza kuiva na tulipokwenda kushiriki michuano ya Kombe la Nyerere, tulifanikiwa kufika fainali ambako tulifungwa na Pamba bao 1-0,” anasema Mziray.
  Hata hivyo, wakati Simba inaanza kuiva, Mziray aliondoka. “Niliondoka Simba kwa sababu nilikuta ina mipira miwili tu. Nilipoomba niongezwe mipira Ngonya alinijibu ovyo”, anasema.
  “Ngonya alinambia Tukuyu Stars imekuwa bingwa mwaka huo (1986) ikiwa na mpira mmoja, itakuwa Simba yenye mipira miwili ishindwe kufanya vizuri? Nikasema kazi hii siiwezi, nikaondoka,”anasema.
  Baada ya kuondoka Simba, Mziray alijiunga na African Sports ya Tanga ambayo mwaka 1988 ndiyo ilikuwa imepanda ligi Daraja la kwanza (sasa ligi kuu).
  Hapo ndipo uwezo wa Mzirary ulipoanza kuonekana kutoka msimu huo, Sports ilitwaa ubingwa wa Tanzania na kupata tiketi ya kushiriki michuano ya Klabu Bingwa Afrika. Hata hivyo, baada ya mafanikio hayo, Mziray aliihama Sports kwa kulazimika.
  “Nilipewa kazi naWizara ya Elimu na Utamaduni, hivyo nikawa mshauri mkuu wa ufundi ndani ya Chama cha Soka Tanzania,” anasema.
  Mziray anasema kwamba kutokana na ushauri wake kutofanyiwa kazi aliamua kuzikimbia ofisi za FAT na kurejea kufundisha. “Nilishauri tuweke mpango wa soka la vijana, haukutekelezwa,”anasema.
  Mwaka 1986 alichukuliwa na timu iliyokuwa ikimikiwa na Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) Pilsner ya Dar es Salaam ambayo msimu huo ilikuwa imepanda daraja.
  Licha ya ugeni wake, Mziray aliiwezesha kushika nafasi ya tatu katika ligi za Bara na kupata tiketi ya kucheza iliyokuwa Ligi ya Muungano.
  Baada ya kuthibitisha tena uwezo wake, Mwenyekiti wa Simba Juma Salum Muhovuge (sasa marehemu), alimrejesha Mziray Msimbazi mwaka 1990. Nilikuwa nasaidiana na King (Abdallah Kibadeni), anasema.
  Huku akiwa ameshaiwekea mazingira mazuri ya kutwaa ubingwa wa Bara, Mziray aliikacha tena Simba na kwenda Yanga, kisa kilikuwa na nini?
  Mwaka 1990 nilipewa jukumu la kuinoa timu ya Mkoa wa Dar es Salaam, Mzizima United iliyokuwa kwenye michuano ya Kombe la Taifa Arusha”, anakumbuka. “Sasa tukiwa kule Yanga ilikuja kucheza mechi ya kirafiki na Taifa Stars.
  Katika Yanga nilikuwa na wachezaji wangu sita wa Mzizima, sasa katika mechi hiyo Stars ilikuwa na makocha wawili, Yanga haina kocha. “Nikaombwa na viongozi wa Yanga niwasaidie kwenye mechi hiyo tu.
  Kwa kuwa kulikuwa na wachezaji wangu si busara kutowasaidia, nikakalia benchi la Yanga tukacheza tukatoka 0-0.
  Kesho yake gazeti moja liliandika Stars, Yanga zatoka sare suluhu Mziray akalilia benchi la Yanga.
  Sasa ile ikapokelewa vibaya na mashabiki wa Simba niliporejea Dar es Salaam vilianza visa nikaamua kupumzika.
  Anasema kwamba Katibu Mkuu wa Simba enzi hizo Abdul Yussuf Hazali alitangaza kwenye vyombo vya habari kwamba yeye (Mziray) atakuwa kocha wa timu B.
  Sasa nikaamua kukaa mwezi mmoja bila kufanya kazi. Yanga wakanifuata kuomba niwafundishe”, anasema.
  Kwa kuwa walinipa mshahara mnono kuliko Simba, nikakubali. Yanga walinipa Sh 70,000, Simba walikuwa wananilipa 50,000.
  Nikiwa Yanga tulicheza na Simba katika michuano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati.
  Niliifunga Simba mara 10 mara moja iliweka kwapani mpira (1992) mara moja ikatufunga kwa penalti Zanzibar, anasema,
  Hata hivyo Mziray anasema kwamba katika maisha yake ya soka, mwezi kuisahau mechi ya Yanga na Simba Zanzibar, kwa sababu alipata misukusuko ya kihistoria.
  Anadai kwamba kabla ya mchezo huo wa fainali ya klabu Bingwa Afrika Mashariki na kati mwaka 1992 mwamuzi na wafadhili wa Simba walimfuata kutaka kumpa hongo ili aihujumu Yanga, lakini yeye alikataa.
  “nikaenda kumwambia mfadhili Mkuu wa Yanga Abbas Gulamali, akaniambia chukua tu pewa hiyo, akakataa”, anasema.
  “Yule mwamuzi na wafadhili wakaja kuniambia: hata usipochukua fedha, lazima ufungwe kwa kuwa wachezaji wako wameshachukua fedha”, anasema.
  Mziray anasema kwamba katika dakika ya nne tu ya mchezo, beki wake tegemeo, Kenneth Pius Mkapa alipewa kadi nyekundu aliyoiita haramu: “Hadi leo sielewi kwa nini Mkapa alipewa red card,” anasema.
  Mziray anasema baada ya Mkapa kutolewa nje Simba walipata bao kipindi cha kwanza na Yanga walifanikiwa kusawazisha kipinbdi hicho hicho.
  Anasema kwamba mchezo ulikwenda hadi dakika za nyongeza na kipindi cha kwanza cha dakika hizo, yeye alipata pigo kubwa. Ni pigo gani?
  Niliona uonevu umezidi, nikasimama kumkaripia mwamuzi, kwa hasira nilipigiza chupa ya maji chini, Hafidh Ally akawambia Polisi waje wanitoe nje ya Uwanja, wakaja kunitoa.
  Kibaya zaidi ilizushwa eti mimi nilimpiga refa na chupa ya maji, Wallahi sikumpiga chupa refa, bali niliipigiza chini.
  Baada ya kupata adhabu hizo, Mziray anasema kwamba akaamua kuhamia Pan African, ambayo aliikuta daraja la pili na kuipandisha Daraja la Kwanza, (sasa Ligi Kuu). Hata hivyo, haikufanya vizuri kama ilivyokuwa kawaida ya kocha huyo, ingawa timu hiyo ilikuwa na vipaji vingi kama Shaaban Ramadhan, Bakari Malima, Ally Yussuf ‘Tigana’, Thomas Mashalla na wengineo.
  “Ile timu ina matatizo sana, haiwezi kuendelea milele. Watu wanaigeuza kitega uchumi, anasema Mziray ambaye mwishoni mwa mwaka 1993 aliacha kufundisha klabu.
  Mziray alikuja kuibuka tena mwaka 1997, alipokuwa Tanzania Stars, ambapo aliiwezesha kubeba kombe la Nyerere na kupata tiketi ya kucheza Kombe la Washindi 1998.
  “Nilipokuwa na timu ile, tuliitoa Bata Bullets ya Malawi, nikapata udhuru wa kwenda kusoma nje nyuma yangu, ilitolewa na Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini,” anasema Mziray ambaye ni Mhadhiri wa Idara ya Viungo Michezoni katika kitivo cha Elimu cha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
  Baada ya hapo, alipotea kabla ya kuibuka na Simba kwa muda katika Ligi Kuu ya soka Tanzania Bara mwaka 2000, enzi hizo ikidhaminiwa Safari Lager akiwa na Kibaden tena na kuiwezesha kuifunga Yanga mabao 2-1.
  “Nikaenda kusoma tena nje, nikiwa huko nasikia Simba ilifungwa na Yanga 2-0 kwenye mchezo wa marudiano,” anasema.
  Baada ya kurejea, ndipo alipoombwa kuifundisha katika Kombe la FAT. Katika michuano hiyo, Simba ilikutana na Yanga katika robo fainali na kufanikiwa kuing’oa kwa mikwaju ya penalti.
  Mwaka 2004, Mziray alipewa tena jukumu la kuinoa Yanga baada ya kufukuzwa kwa aliyekuwa kocha wa timu hiyo, Jean Pollycarpe Bonganya. Lakini msimu wa Ligi ulipomalizika, naye aliachana na timu hiyo.
  Katika ujio wake wa 2004, kituko cha kukumbukwa kwa mziray ilikuwa ni kwenye mechi ya Ligi Kuu dhidi ya watani wa jadi, Simba ambayo ilichezwa siku ya mchezo wa kiungwana ya FIFA (FIFA Fair play Day).
  Siku hiyo, Mziray aliivua fulana ya FIFA Fair Play na kuitupilia mbali baada ya kukerwa na kitendo cha mwamuzi kuiuma Yanga kwenye mchezo huo uliomalizika kwa sare ya 2-2.
  Mziray alichukuliwa tena na Simba msimu huu alipochukuliwa maalum kwa ajili ya mchezo mmoja tu dhidi ya Yanga, Oktoba 26, mwaka jana.
  Wakati huo Simba ilitoka kufungwa 4-1 na Toto Afrika mjini Mwanza, uongozi na imani tena na Krasmir Bezinski kutoka Bulgaria kama anaweza kuiongoza timu hiyo kwenye mchezo dhidi ya watani wa jadi, Yanga.
  Hivyo ikamuomba Mziray awasaidie, na kweli alifanikiwa kuibadilisha Simba hatimaye ikatoa upinzani kwa Yanga na kufungwa 1-0 kwa taabu.

  MZIRAY NA TIMU ZA TAIFA:
  Kwa mara ya kwanza ilikuwa mwaka 1990, wakati aliposaidiana na Mansour Magram (sasa marehemu) katika michuano ya Challenge mjini Zanzibar na kutolewa na Uganda katika hatua ya Nusu Fainali. Lakini Bara ilishika nafasi ya tatu kwa kuifunga Zanzibar 2-1.
  Mwaka 1994 alipewa tena timu hiyo na kufanikiwa kuibebesha Kombe la Challenge nchini Kenya. Hiyo ilikuwa ni baada ya kulisaka taji hilo kwa miaka 20.
  Hiyo ni kwa upande wa timu ya Bara, mwaka 1998 alipewa jukumu la kuokoa jahazi katika hatua ya awali ya Kombe la Mataifa ya Afrika, baada ya Hafidh Badru kususa.
  “Nilipewa timu siku mbili kabla ya mechi Dar, tukafungwa bao 1-0 na Burundi na kutolewa,” anasema. Mwaka 1999, alipewa jukumu tena la kuinoa Taifa Stars, iliyoshiriki michuano ya CECAFA Castle mjini Nairobi, Kenya ambako ilishika nafasi ya tatu, baada ya kuifunga Ghana 3-2.
  Mziray ni kocha msomi na mtumishi wa Serikali tangu mwaka 1981 alipokuwa Afisa Lugha na Sanaa katika iliyokuwa Wizara ya Utamaduni na Michezo. Mwaka 1986 alipandishwa cheo na kuwa Mtaalamu wa Soka Wizarani.
  Kama ilivyo kwa binadamu wengine, Mziray amepitia matatizo mengi ya kijamii. Ikiwamo kufiwa na mke wake wa kwanza. Anna mnamo mwaka 1997.
  “Sipendi kuzungumza sana hili utanirejesha kwenye majonzi, lakini nashukuru Julai 31, 1999 nimeoa mke mwingine (Gaudencia),” anasema.
  Mipango yake ya baadaye ni kuanzisha Chuo cha Soka, ili kuinua mchezo huo hapa nchini “Bila youth program hatuwezi kufanikiwa,” anasema.
  Mziray ambaye ni baba wa watoto wane: Miriam, Emmy, Robert na Lillian, alizawaliwa Novemba 11 mwaka 1957.
  Alipata elimu ya msingi katika shule saba kutokana na kuhamahama shule hizo ni Ifunda (Iringa), Lpw Academic (Iringa) Mpechi (Njombe), Songwe (Mbeya) Butimba (Mwanza) Lukajunge Karagwe) na kumalizia Wami (Morogoro) mwaka 1973.
  Elimu ya sekondari alipata kwenye shule ya Malangali (Iringa) kable ya kwenda kidato cha sita kwenye Shule ya Mirambo mkoani Tabora.
  Alipomaliza masomo ya sekondaru Mziray alikwenda Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kambi ya Makutupora mkoani Dodoma.
  Mwaka 1981, alikwenda kusoma nchini Bulgaria katika chuo kimoja mjini Sofia, ambako mwaka 1986 alipata Shahada ya Pili ya Viungo na Utamaduni.
  Mwaka 1996 na 1997, alikwenda Norway na 2000 alikwenda Finland akiwa mwanafunzi wa Chuo cha Vuebamaki.
  Mwaka 2001, Mziray alipewa tena jukumu la kuinoa Stars kwa ajili ya michuano ya Kombe la CECAFA Castle mjini Mwanza, akisaidiwa na Charles Boniface Mkwasa ambao wote walikuwa chini ya Mjerumani, Burkhad Pape, aliyekuwa Mshauri wa Ufundi.
  Timu hiyo ilitwaa Kombe hilo, ikiifunga Uganda kwenye fainali mabao 3-0.
  Mziray anawataja wanasoka wanaosuuza roho yake kuwa ni kipa wa zamani wa Yanga, Sahau Kambi, Iddi Pazi na Mohamed Mwameja.
  Wengine ni beki wa zamani, Kenneth Mkapa na mlinzi George Masatu wakati mawinga ni Justin Mtekere (sasa marehemu), Abbas Mchemba, Shekhan Rashid, Hamisi Tobias Gaga (marehemu).
  “Washambuliaji bado sijaona kama (Zamoyoni), Mogella na (Victor) Mkanwa katika hawa nyota wenu wa leo,” anasema.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: HUYU NDIYE SYLLERSAID MZIRAY... Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top