• HABARI MPYA

  Jumamosi, Machi 28, 2009

  AKINA OWINO HOI KWA WAARABU NYUMBANI

  George Owino wa Yanga akiichezea timu yake ya taifa, Kenya dhidi ya Tanzania, hapa anamtoka kiungo wa Yanga, Mrisho Ngasa aliyeanguka chini, mbele ya benchi la Tanzania. Hii ilikuwa kwenye michuano ya Challenge na mechi hii hii ya Nusu fainali ambayo Taifa Stars ilifungwa na Harambee Stars 2-1, ilichezwa kwenye Uwanja wa Nelson Mandela, eneo la Namboole mjini Kampala, Uganda, Desemba mwaka jana.

  NAIROBI, Kenya
  TIMU ya Taifa ya soka ya Kenya, Harambee Stars jana ilishindwa kufurukuta kwenye uwanja wake wa nyumbani wa Nyayo baada ya kuchapwa mabao 2-1 na Tunisia katika mechi ya Kundi B ya michuano ya awali kusaka tiketi ya Kombe la Dunia 2010.
  Katika mechi hiyo, wageni Tunisia ndio waliokuwa wa kwanza kupata bao katika dakika ya tano ya mchezo huo mfungaji akiwa ni Ammar Jemal bao ambalo lilidumu kwa kipindi chote cha kwanza.
  Kipindi cha pili, Kenya ikishangiliwa na mashabiki wa nyumbani ilisawazisha bao hilo kupitia kwa mchezaji wa kimataifa wa Auxerre ya Ufaransa, Dennis Oliech na kuamsha shamrashamra za mashabiki.
  Hata hivyo furaha hizo zilikuwa za muda mfupi kwani dakika mbili baadaye, Tunisia waliongeza bao la pili kupitia kwa Issam Jomaa
  Harambee iliwakilishwa na Noah Ayuko, Musa Otieno, George Owino, Pascal Ochieng, John Mwangi/Victor Wanyama, Hillary Echesa/Boniface Ambani, Francis Ouma/Patrick Oboya, Dennis Oliech, MacDonald Mariaga, Mulinge Ndeto na Robert Mambo.
  Wachezaji wa akiba ambao hawakucheza ni Joseph Shikokoti, Peter Opiyo, Jockins Atudo na David Okelo.
  Timu nyingine katika kundi hilo ni Msumbiji na Nigeria ambazo zinatarajia kuumana leo mjini Maputo.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: AKINA OWINO HOI KWA WAARABU NYUMBANI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top