• HABARI MPYA

  Jumamosi, Machi 28, 2009

  YANGA WAIANGUSHA SIMBA DAR


  YANGA jana ilishindwa kulipa kisasi kwa Kagera Sugar ya Bukoba, baada ya kulazimishwa sare ya 1-1 kwenye Uwanja wa Uhuru, zamani Taifa, mjini Dar es Salaam, katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
  Kagera imeifunga Yanga mara mbili mfululizo, kwanza ni kwenye mechi ya marudiano ya Ligi Kuu msimu uliopita na pili ni kwenye mechi ya kwanza ya msimu huu mjini Bukoba.
  Hata hivyo, Yanga ambayo tayari imekwishatwaa ubingwa wa msimu huu, imetimiza pointi 47, wakati Kagera imebakia kwenye nafasi ya tatu, licha ya kufikisha pointi 28, kwani Mtibwa imeshika nafasi ya pili kwa wastani wake mzuri wa mabao ya kufunga na kufungwa na Prisons imeishusha Simba hadi nafasi ya tano.
  Hadi mapumziko, hakuna timu iliyofanikiwa kupata bao. Yanga ilicheza dakika zote 45 za kipindi cha kwnza wakiwa pungufu, kutokana na Nahodha Freddy Mbuna kutolewa nje kwa kadi nyekundu, baada ya kwenda kumpiga shabiki.
  Mwamuzi wa mchezo huo, Nassib Mabrouk kutoka Mwanza, alimpa kadi nyekundu Mbuna mara tu baada ya kupuliza kipyenga cha mapumziko, kutokana na beki huyo wa kulia kuruka uzio wa Uwanja na kwenda kumpiga shabiki. Ilidaiwa shabiki huyo wa Simba, alimtukana Mbuna baada ya kukosa bao akiwa yeye na kipa.
  Katika mchezo huo, Yanga ilikuwa ya kwanza kupata bao dakika ya dakika ya 79, mfungaji akiwa ni Athumani Iddi ‘Chuji’, baada ya kuupiga mpira kiutaalamu akimchambua Odo Nombo.
  Chuji alifunga bao hilo, baada ya kupokea pasi ya Mrisho Ngassa, aliyemnyanyasa beki Said Mourad kwa chenga za maudhi. Mashabiki wa Simba walisimama na kushangilia, bao hilo, wakati Yanga walikuwa wakiwabeza kwa kuimba; “Tumewabeba”.
  Hata hivyo, bao hilo halikudumu sana, kwani dakika ya 87, Abdallah Juma aliyeingia kuchukua nafasi ya Paul Kabange aliisawazishia Kagera, baada ya kuunasa mpira uliopigwa na Nurdin Bakari na kwenda kumchambua kipa Juma Kaseja.
  Baada ya bao hilo, mashabiki wa Simba walikuwa kimya wakati wa Yanga walikuwa wakiwabeza; “Mbona hampigi kidedea”.
  Kutokana na utani wao wa jadi, Simba inapofungwa Yanga hushangilia na Wekundu wa Msimbazi pia hubezwa pia na wana Jangwani wanapofungwa. Lakini jana, Simba walilazimika kuishangilia Yanga kutokana na kutaka Kagera ifungwe, kwa sababu zinawania pamoja nafasi ya pili.
  Kikosi cha Yanga jana kilikuwa; Juma Kaseja, Freddy Mbuna, Abubakar Mtiro, Nurdin Bakari/Razak Khalfan, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Castory Mumbara, Mrisho Ngassa, Geoffrey Boniface, Athumani Iddi, Jerry Tegete/Nsajigwa Shadrack na Kiggi Makasy/Shamte Ally.
  Kagera; Odo Nombo, Shaabani Ibrahim, Hamisi Athumani, Said Mourad, Bakari Omar, David Charles, George Nketto, Paul Kabange/Abdallah Juma, Mike Katende/ Shija Mkina, Themi Felix na Paul Ngway/John Mwange.
  Katika mchezo mwingine, Mtibwa Sugar ya Morogoro iliibuka na ushindi wa 2-1 dhidi ya Villa Squad ya Kinondoni, ambayo nayo imezidi kujichimbia kaburi kuelekea kushuka daraja.
  Mtibwa ilitangulia kupata bao dakika ya tano, mfungaji akiwa ni Shaaban Nditi, kabla ya Lameck Dayton kusawazisha dakika ya 28, lakini dakika ya 77 Omar Matuta ‘Wanchope’ aliifungia Mtibwa bao la ushindi, baada ya kuuwahi mpira uliotemwa na kipa, kufuatia shuti kali la Abdallah Juma.
  Mtibwa sasa imetimiza pointi 28 na kupanda hadi nafasi ya pili, ikiwa mbele ya Kagera na Prisons ambazo zote zina pointi 28 kila moja, lakini yenyewe iko juu kwa wastani wake mzuri wa mabao ya kufunga na kufungwa.
  Katika mchezo mwingine kwenye Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya, wenyeji Prisons waliibuka na ushindi wa 1-0 dhidi ya Polisi ya Dodoma. Bao pekee kwenye mchezo huo lilitiwa kimiani na Ismail Suleiman ‘Suma’ dakika ya 38 kwa njia ya penalti. Mwamuzi Peter Mujaya wa Pwani, alimtoa nje kwa kadi nyekundu beki wa Prisons, Henry Mwalugala dakika ya 55, baada ya kumchezea rafu kiungo wa Polisi, Bantu Admin.
  Kwa matokeo hayo, Prisons imetimiza pointi 28 baada ya kucheza mechi 18, hivyo kuingia kwenye orodha ya timu zinazowania nafasi ya pili, sambamba na Simba, Kagera na Mtibwa Sugar.
  Polisi imeendelea kuporomoka ikiwa inashika mkia kwa kubaki na pointi zake 12, baada ya kucheza mechi 18 pia. Ligi hiyo inatarajiwa kuendelea leo kwa mchezo kati ya Azam FC na Simba, Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: YANGA WAIANGUSHA SIMBA DAR Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top