• HABARI MPYA

  Monday, March 09, 2009

  WAKILI MPENZI WA YANGA AHOJIWA NA POLISI, NI KUHUSU WIZI WA 'FWEZA' ZA BARCLAYS

  WAKILI maarufu wa kujitegemea na mpenzi wa klabu ya Yanga ya Dar es Salaam, Theonist Rutashoborwa anashikiliwa na jeshi la Polisi tangu leo asubuhi kwa ajili ya kuhojiwa juu ya wizi wa fedha katika benki ya Barclays.
  Kamanda wa Polisi, Kanda Maalum Dar es Salaam, Suleiman Kova amesema leo mchana katika mkutano na Waandishi wa Habari kwamba, jeshi lake limemchukua kwa mahojiano Rutashoborwa maarufu kama Rutta katika muendelezo wa uchunguzi wa kesi hiyo.
  Alisema kwamba katika kumhoji kwao, ndio watajua kama wakili huyo ataingia kwenye eneo lipi katika kesi hiyo, kama shahidi au muhusika kwa maana ya kwamba maelezo yake na vyanzo vyao ndio vitatoa jibu.
  Hata hivyo, kulikuwa kuna habari kwamba mipango ya kumtolea dhamana Rutta iwapo polisi itamtia hatiani ilikuwa imekwishapangwa na bongostaz inaendelea kufuatilia juu ya matokeo ya sakata hilo.
  Tayari watuhumiwa wengine wawili, akiwemo Mkurugenzi Mtendaji wa Dar es Salaam Cement, mfanyabiashara maarufu nchini, Merey Ally Merey anayefahamika zaidi kama kama Merey Balhaboub (41) na Abdallah Said Abdallah (48) wamekwishafikishwa mahakamani kwa tuhuma hizo.
  Walipandishwa kzimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam.
  Merei, ambaye pia ni mdau mkubwa michezo na Abdallah, waliunganishwa kwenye kesi hiyo pamoja na washitakiwa wengine saba, ambao jana hawakuwapo mahakamani wakidaiwa kula njama na kuiba zaidi ya dola za Marekani milioni moja.
  Washitakiwa hao waliunganishwa na watuhumiwa wengine katika mashitaka ya kwanza, ya pili, tisa na 10 ya kula njama, kugushi, huku katika kosa la 11 na 12 ya wizi, yakiwahusu washitakiwa wa nane na tisa, Merey na Abdallah.
  Akiwasomea shitaka la kwanza linalowakabili, Mwendesha Mashitaka Mkuu, Charles Kenyela, alidai kuwa Oktoba 19, mwaka jana, washitakiwa hao na washitakiwa wengine saba ambao wako nje kwa dhamana, walikula njama za kuiba dola za Marekani 1,263,000, mali ya Benki ya Barclays.
  Mbele ya Hakimu Mkazi Walyalwande Lema, katika shitaka la tisa Merey na Abdallah, Oktoba 27, mwaka jana walidaiwa kughushi ujembe wa kasi wenye namba 000305 kupitia akaunti namba 00180093 uliokuwa akienda Kampuni ya Mafuta ya Oilcom kwa lengo la kuhamisha dola za Marekani 700,769, wakidai ulikuwa halali.
  Kenyela alidai kuwa katika shitaka la 10 lililotokea Oktoba 27, mwaka jana jijini Dar es Salaam, washitakiwa hao walighushi ujembe wa kasi kwa lengo la kuiba dola za Marekani 299,974.
  Shitaka la 11 na 12 linawahusu washitakiwa wa nane na tisa, Merey na Abdallah, ambako ilidaiwa kuwa Oktoba 30, mwaka jana, kwa nyakati tofauti katika Benki ya Barclays, Tawi la Ohio, waliiba jumla ya dola za Marekani 1,000,943 mali ya benki hiyo.
  Washitakiwa hao wanaotetewa na Mawakili wawili, Martin Matunda na Walter Chipeta, walikana kuhusika na mashitaka yote na kudhaminiwa kwa hati ya mali yenye thamani ya Sh milioni 900.
  Washitakiwa hao walidhaminiwa kwa masharti yaliyowekwa na Mahakama Novemba 13, mwaka jana, ambayo ni kuwa na wadhamini wawili kila mmoja, waliotakiwa kusaini bondi ya Sh milioni 40, kutoa fedha taslimu Sh milioni 78 na au kuweka mali yenye thamani hiyo, kutotoka nje ya jiji la Dar es Salaam bila kibali cha mahakama na kuwasilisha hati zao za kusafiria mahakamani.
  Merey, maarufu katika michezo kwa jina la Balhabou, alikuwa mmiliki wa timu ya Moro United akiichukua kutoka madaraja ya chini ilikokuwa ikifahamika kama Zaragoza na kuipandisha daraja.
  Amewahi kuwa mlezi wa Chama cha Waandishi wa Michezo nchini (TASWA).
  Washitakiwa hao walidhaminiwa na Ipyana Mwandemba, dereva wa Ubalozi wa Comoro nchini, Said Awadh, anayefanya kazi Ubalozi wa Comoro, Sahau Kambi, ambaye ni mshauri wa Balozi wa Comoro nchini na dereva wa Balozi huyo, Paul Fernandez.
  Washitakiwa wengine katika kesi hiyo ni Winford Mwang’onda (34), Shubira Mutungi (24), Neema Saria (24), Upendo Mushi (30), Margaret Longway (31), Emmanuel Mukono (40) na Ramadhani Khamis (36). Kesi hiyo itatajwa April 29, mwaka huu.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: WAKILI MPENZI WA YANGA AHOJIWA NA POLISI, NI KUHUSU WIZI WA 'FWEZA' ZA BARCLAYS Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top