• HABARI MPYA

  Ijumaa, Machi 27, 2009

  NASSIB PRESHA INAPANDA- PRESHA INASHUKA TFF


  SIKU za Ramadhan Nassib (pichani kulia) kuendelea kuwa Makamu wa Pili wa Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) zimeanza kuhesabika baada ya klabu yake ya Villa Squad kuendelea kufanya vibaya kwenye Ligi Kuu YA Vodacom Tanzania Bara inayoelekea ukingoni.
  Rais wa TFF huwa na makamu wawili, lakini makamu wa pili hutakiwa kuwa mwakilishi wa klabu za Ligi Kuu.
  Kwa mujibu Katiba ya TFF kipengele B kanuni ya 31 kifungu cha tatu kinasema kuwa:"...Makamu wa Pili wa Rais au mwakilishi wa klabu ya Ligi Kuu katika Kamati ya Utendaji akipoteza nafasi hiyo kutokana na timu yake kushuka daraja, maana yake mkutano wa mwaka unaofuata utatakiwa kujaza nafasi hiyo kwa kuchagua makamu mwingine au mwakilishi kuziba nafasi hiyo."
  Mkutano wa mwaka wa TFF utafanyika Desemba jambo ambalo linaweza kushuhudia uchaguzi mdogo ukifanyika kuchagua makamu wa pili wa rais mpya wa TFF ambaye klabu yake itakuwa kwenye Ligi Kuu Bara, hivyo kumfanya Nassib kuwa kiongozi aliyekaa muda mfupi zaidi kwa mujibu wa katiba.
  Zikiwa zimebakia mechi tano kwa kila timu kumaliza msimu huu wa Ligi Kuu Bara, Villa Squad imekusanya pointi 14 na ipo katika ukanda wa timu tatu za kushuka daraja.
  Iwapo Villa itashindwa kufanya vizuri katika mechi zake hizo itashuka daraja pamoja na nyingine mbili na kuzipisha timu tatu zilizopanda daraja ambazo ni Majimaji ya Songea, African Lyon na Manyema zote za Dar es Salaam.
  Villa ambayo tayari imefungwa mabao 41 ambayo ni mengi zaidi katika ligi hiyo mwishoni mwa wiki ilipokea kipigo cha mabao 6-2 kutoka kwa Azam jambo ambalo linaashiria kuwa hali si nzuri hata kidogo kwa timu hiyo ya Kinondoni.
  Akizungumza mijini Dar es Salaam jana, Msemaji wa Villa Squad, Idd Godigodi alisema wapo katika harakati za kuhakikisha timu hiyo inafanya vizuri ili kuepukana kushuka daraja.
  "Umakini mdogo wa mabeki wetu ndio hasa unaosababisha tuongoze kwa kufungwa magoli mengi," alisema.
  "Kwa kushirikiana na benchi la ufundi tunajipanga ili kufanya vema katika mechi zote tano zilizobaki ili tuepukana hayo yote yaliopo mbele yetu."
  Villa inashika nafasi ya 11 katika msimamo wa ligi ikiwa na pointi 14 na imebakiza mechi tano ili kukamilisha mechi zake za Ligi Kuu ya Tanzania Bara.
  Timu nyingine ambazo zipo hatarini ni Moro United yenye pointi 15 katika nafasi ya kumi na Polisi Dodoma yenye pointi 12 ikishika nafasi ya mwisho.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: NASSIB PRESHA INAPANDA- PRESHA INASHUKA TFF Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top