• HABARI MPYA

    Saturday, March 28, 2009

    HUYU NDIYE PATRICK PHIRI, KOCHA WA WEKUNDU WA MSIMBAZI


    KATIKA kujiwekea mazingira ya kufanya vizuri kwenye mzunguko wa pili wa Ligi Soka Tanzania Bara, klabu ya Simba imeamaua kumrejesha kocha aliyewahi kukinoa timu hiyo kwa mafanikio miaka ya nyuma, Mzambia Patrick Phiri.
    Phiri, akiwa na Simba, kikosi hicho kiliweza kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu mara mbili kabla ya kuondoka kabla ya msimu baada ya kutofautiana na na uongozi katika suala la maslahi, kwa mara ya kwanza alitua Simba mwaka 2004, akirithi mikoba ya Mkenya, James Aggrey Siang’a, ambaye pia ailing`arisha vilivyo timu hiyo kitaifa na kimataifa.
    Hata hivyo, baada ya kuondoka kwa Phiri, Simba imeshindwa kudumu na makocha licha ya kufanikiwa kupata makocha bora kutoka nchi mbalimbali duniani na kubwa hasa ni msigano baina ya viongozi na makocha hao.
    Baadhi yao, ni pamoja na Trott Moloto wa Afrika Kusini, Neider dos Santos wa Brazil, Nielsen Elias, Milovan Circovic (Serbia) na Krasmir Sminelov Benziski (Bulgaria).
    Baada ya kocha wa mwisho (Benziski), kutimuliwa baada ya kushindwa kuipatia mafanikio katika kipindi chake ikiwemo kushindwa kutwaa kombe la Kagame na kufanya vibaya kwenye mzunguko wa kwanza wa ligi kuu, Phiri akawa chaguo kwa mara nyingine.
    Hivyo, basi baada ya kuhangaika huku na kule iliamua kumrejea tena Phiri ambaye licha ya kukwazwa katika kipindi kile aliridhisha moyo na kuamua kurejea kwa mara nyingine kukinoa kikosi hicho cha Wekundu wa Msimbazi.
    Kocha huyo, Alhamisi iliyopita, alisaini mkataba wa kuinoa timu hiyo kwa miaka miwili ambapo mara baada ya kutua nchini wiki iliyopita, alisema atafanya kadiri awezavyo kuhakikisha timu hiyo inarudi katika uhai wake wa miaka ya nyuma.
    Akizungumza katika hafla ya kusaini mkataba huo, Phiri alisema kwamba anajisikia furaha kurudi Tanzania kuifundisha Simba kwani wakati anaifuatilia timu hiyo akiwa Zambia, alikuwa akisikitishwa alipokuwa akisikia haifanyi vizuri katika mashindano.
    “Nakumbuka nilipokuwa na timu ilikuwa ikifanya vizuri sana na kuweza kupata mafanikio…lakini katika miaka ya hivi karibuni nilikuwa nakisikia timu haifanyi vizuri, hivyo nimekuja kuitengeneza timu yangu ili iwe na uhai kama zamani,” alisema Phiri.
    Hata hivyo, Phiri alisema anahitaji muda kidogo wa kukaa na wachezaji ili kufahamu mapungufu yaliyopo kabla ya kuanza kuyarekebisha makosa, ili kujenga kikosi imara cha ushindi.
    “Nimeikuta timu ikiwa katika nafasi ya sita katika msimamo wa ligi Kuu bara, hivyo natarajia baada ya muda nitakapokaa na kurekebisha kasoro, timu itakuwa katika nafasi nzuri zaidi,” alisema.
    Akijibu swali kwamba ni kwanini anajiunga na Simba ambayo imekuwa ikibadili makocha usiku na mchana, Phiri alisema ni vigumu kwake kuzungumzia matatizo ya makocha wengine.
    “Siwezi kuzungumzia matatizo ya makocha wengine au mtu fulani…nipo hapa kwa ajili ya kuinoa Simba ili ipate mafanikio si vinginevyo,”alisema.
    Kihistoaria, Phiri alizaliwa nchini Zambia, mwaka 1956. Aidha, mbali ya kucheza soka na ndani ya miaka miwili iliyopita, alikuwa kocha mkuu wa timu ya Taifa ‘Chipolopolo Boyz’ akisaidiana na mchezaji wa zamani wa timu hiyo, Kalusha Bwalya, katika fainali za kombe la Mataifa ya Afrika mwaka 2008 huko Ghana.
    Alianza kucheza soka tangu utotoni kabla ya nyota yake kung’ara akiwa kwenye timu ya Ronkana ambayo miaka ya 1970 ilibadilishwa jina na kuwa Nkana Red Devils na mwanzoni mwa karne ya 21 ikabadilishwa tena jina na kuwa Nkana FC, kabla ya kuhamia Red Arrows mwanzoni mwa miaka ya 1980.
    Akiwa na Ronkana, alikiwezesha kutwaa taji la kwanza la kimataifa hivyo kupachikwa jina la utani ‘Mathetician’ kabla ya kuwa mmoja ya wachezaji wa timu ya Taifa iliyoshiriki fainali za Mataifa ya Afrika huko Ghana mwaka 1978.
    Katika kikosi hicho, Phiri alitumika zaidi kama mchezaji wa akiba na alikuwa akipigania kuwa kikosi cha kwanza na katika nafasi ya kiungo akikabana koo na Alex Chola, Evans Katobe, Willie Phiri, Peter Kaumba na Stone Chibwe.
    Kipaji cha Phiri cha kufundisha soka kilianza kujionyesaha alipokuwa anamaliza soka yake katika timu ya Arrows.
    Na Chama cha Soka cha Zambia (ZAF), hakikusita kumpeleka Ujerumani baada ya ushauri toka kwa Ofisa wa michezo wa ZAF wa wakati huo, Boniface Simutowe (ambaye sasa ni kocha wa Profound).
    Aliporejea kutoka Ujerumani, Phiri alipewa jukumu la kukinoa kikosi cha Red Arrows na kocha huyo mdogo hakuwaangusha watu hao waliomuamini kabla ya kuhamia Lusaka Dynamos, ambako aliiwezesha timu hiyo kuwa tishio.
    Sifa za kikosi hicho ni wachezaji kuwa na stamina na nguvu, kuwabana wapinzani bila kuwapa nafasi ya kucheza watakavyo na uchapaji kazi. Uwezo huu wa timu hii ya Phiri ulileta mshtuko mkuu katika Ligi Kuu ya Zambia.
    Baadhi ya nyota waliozalishwa na Phiri wakati akiinoa Dynamos, ni pamoja na Perry Mutapa aliyewahi kukipiga Ureno na Orlando Pirates ya Afrika Kusini, Alex Namazaba na Nsofwa Chaswe ambaye sasa ni marehemu (Malaysia na Israel).
    Mafanikio yake yaliifanya FAZ kumpa ofa ya kukinoa kikosi cha taifa cha vijana wenye umri chini ya miaka 20 mnamo mwaka 1996 ambapo kikosi hicho kilishiriki michuano ya vijana ya Afrika iliyopigwa mwaka 1997 huko Morocco.
    Kikosi hicho kiliondolewa katika hatua ya makundi kwa kufungwa bao 1-0 na Benin, sare ya 2-2 na Ivory Coast kabla ya kutoka tena sare ya bao 1-1 na Mali.
    Kitu cha kustaajabisha ni kwamba kuna wachezaji walikuwemo kwenye kikosi hicho ambao mpaka sasa bado wanasakata kabumbu ya uhakika, wachezaji hao ni Andrew Sinkala anayecheza Ujerumani na Harry Milanzi anayecheza Angola tofauti na wenzao waliokuwa nao katika kikosi hicho Rotson Kilambe,Edward ’Bubble’ Kangwa, Emmanuel Zulu, George Kampembwa, Gift Kampamba, Gerald Sakala na Perry Mutapa Mutapa.
    Baada ya mashindano hayo, Phiri aliondolewa katika timu hiyo na kupewa Benjamin Bwalya ambaye ni kaka mkubwa wa Kalusha, kabla ya Bwalya kufariki mwaka 1998. Hata hivyo, Phiri alirejeshwa tena kukinoa kikosi hicho.
    Aliendelea na kikosi hicho mpaka alipokiacha, akiacha historia ya kukiwezesha kufuzu fainali za kombe la FIFA kwa vijana zilizofanyika nchini Nigeria mwaka 1999 ambako ilikuwa ni mara ya kwanza kwa nchi hiyo kufuzu.
    Katika fainali chini ya nahodha wao, Andrew Sinkala, Zambia iliifunga Honduras mabao 4-3 na kulazimisha sare na mabingwa watetezi, Hispania wakiwa na nyota wa Real Madrid, Iker Casilas na Guti.
    Kikosi cha Zambia kiliundwa na wakali kama Gift na Chintu Kampamba, Milton Tembo, Amon Simutowe,Ronald Mbambara, Chaswe, Zulu na Ian Bakala, hata hivyo walitolewa katika mashindano na Brazil baada ya kufungwa mabao 5-1.
    Phiri akiwa na kikosi cha vijana chini ya miaka 23 ‘Bamfuchile’, kikiongozwa na Moses Sichone, Mutapa na Kilambe walishinda nafasi ya pili katika fainali za All Africa Game, ambako kwa ZAF ilijivunia mafanikio ya tatu kwa michuano ya COSAFA chini ya miaka 20 hayo yalikuwa mafanikio makubwa na ya kukumbukwa na Phiri.
    Phiri, mchezaji wa zamani wa Nkana na Red Arrows, alikuja Tanzania mwaka 2002 na kujiunga na Simba FC baada timu yake kuondolewa katika hatua ya kwanza kwenye Fainali za kombe la Mataifa ya Afrika zilizopigwa nchini Mali.
    Phiri alitangazwa kuchukua nafasi ya Mjerumani, Burkand Ziese kama kocha wa Chipolopolo.
    Hata hivyo, Mjerumani huyo aliiwezesha Zambia kufanya vizuri katika michezo yake ya fainali za Mataifa ya Afrika zilizopigwa Tunisia, lakini bahati haikuwa yao kwani walifungwa na Benin 3-1 katika mechi ya mwisho.
    Kujiunga kwake Simba, kuliiwezesha timu hiyo kufanya vizuri katika mechi yake, hata hivyo alipokwenda kwao kwa mapumziko, alipata ajali ambayo ilimfanya ashindwe kurudi nchini kuendelea kuinoa timu hiyo, nafasi yake ikatwaliwa na Trott Moloto wa Afrika Kusini.
    Baada ya kupata nafuu, Phiri aliazimwa na timu yake ya zamani ya Nkana akipewa cheo cha Mkurugenzi wa Benchi la Ufundi na kipindi hicho kilimpandisha chati zaidi ambako FAZ iliweza kumpa mikoba ya kukinoa kikosi cha Taifa cha Zambia baada ya kuziba nafasi ya Kalusha Bwalya, baada ya muda wake kufika ukomo.
    Kipindi hicho, Phiri alikiandaa kikosi kwa ajili ya ushiriki wa michuano ya Castle COSAFA na ile ya CHALENJI mwaka 2006, hiyo ilikuwa ni mara kwanza kwa Zambia kutwaa taji tangu mwaka 1998.
    Ikiwa imebakiza mechi moja ugenini dhidi ya Afrika Kusini, Bafana Bafana, ambao walikuwa wanaizidi pointi tatu timu ya Phiri, hakika nafasi ya Zambia kufuzu kwenye fainali za Ghana mwaka jana ilikuwa finyu.
    Wakati mashabiki wa soka nchini Zambia wakiwa wamekata tamaa, Phiri aliiongoza timu hiyo kufanya maajabu kwa kuifunga Bafana iliyokuwa inanolewa na Mbrazil, Pereira mabao 3-1 nyumbani kwake, hivyo kukata tiketi ya kucheza fainali za Ghana.
    Je, baada ya kuing`arisha Zambia katika fainali za Ghana, makali hayo yataweza kurejesha moto wa Simba katika mashindano ya kitaifa na kimataifa ambao umefifia? Ni jambo la kusubiri na kuona
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: HUYU NDIYE PATRICK PHIRI, KOCHA WA WEKUNDU WA MSIMBAZI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top